April 24, 2014

 
PUNDE AKIMPA TUZO TAMBWE
Na Saleh Ally
LIGI Kuu Bara msimu wa 2013-14 imefikia tamati kwa Azam FC kuweka rekodi mpya ya kuwa moja ya timu ambazo si Yanga wala Simba ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Walichokifanya Azam FC ni moja ya rekodi ambazo zinaweza kuwa na hamasa ya kuongeza tamaa na hali ya kujiamini kwa timu nyingine kwamba soka linaweza kuwa la ushindani zaidi nchini na wanaoweza kupata ubingwa au mafanikio si Yanga au Simba pekee.

Lakini wakati ligi imemalizika, burudani ilikuwa ni ile mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga ambao walikuwa wanafunga msimu na kama kawaida, wanapokutana inakuwa ni burudani. Siku ya mechi hiyo iliyokuwa ni ya kufunga msimu, mshambuliaji Amissi Tambwe wa Simba ambaye ameibuka kuwa mfungaji bora alituzwa.
TAMBWE KAZINI

Tambwe raia wa Burundi, alipokea tuzo yenye thamani ya Sh 50,000 tu ambayo amepewa kutokana na uwezo aliouonyesha wa upachikaji mabao, kwani amefunga 19 na ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-14.
Mrundi huyo hakupewa tuzo hiyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala wadhamini wa ligi hiyo, Vodacom. Tuzo hiyo imetolewa na William Punde, mkazi wa Mburahati jijini Dar es Salaam ambaye ni mlemavu lakini mpenda michezo na shabiki wa Simba.
Punde alimkabidhi Tambwe tuzo aliyoitengeneza kwa gharama ya Sh 50,000 huku akisema kama angeiuza, basi angepata kuanzia Sh 150,000 hadi 200,000. Lakini aliona amzawadie Tambwe na kama haitoshi ana zawadi kwa ajili ya mabingwa wapya, Azam FC.
Shabiki huyo wa Simba ni fundi seremala katika kampuni ya Auto Make maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam na anavutiwa zaidi na kazi ya sanaa ndiyo maana aliamua kutumia fedha yake kuchonga zawadi hiyo kwa Tambwe akiamini kukubali kazi za watu ni jambo jema.
Punde baba wa watoto wawili, Jesca William (16) na Frank William (10) ambao amewapata akiwa na mkewe Lucy Mathayo, amekuwa akishiriki kwenye mambo ya michezo kupitia ‘chama’ lake la Milambo la Mburahati, lakini kuna timu ya watoto ya Mburahati United.
Kwa nini Tambwe?
Niliamua kumpa tuzo Tambwe kwa kuwa amefanya kazi kubwa, ameonyesha uwezo na kweli alistahili kwa kuwa amejituma. Anayefanya vizuri ni mtu ambaye anatakiwa kupongezwa kutokana na alichokifanya, huo ndiyo ulikuwa uamuzi wangu.
Unafaidika?
Faida ni kuridhisha nafsi yangu, lakini pia kutoa somo kwamba hata mimi, licha ya kuwa mlemavu bado ninaweza kusaidia na si kusaidiwa tu. Pia ninaweza kuwa nina mchango wangu pamoja na kwamba sina kipato kikubwa lakini lengo ni kuonyesha mapenzi na nia yangu ya kukuza kitu.
Tuzo:
Niliamua kutengeneza tuzo hiyo yenye mfumo wa kiatu pamoja na mpira kwa kuwa nimeona baadhi ya tuzo kubwa duniani. Niliitengeneza kwa siku kadhaa na pia nilifanya kwa umakini mkubwa kwa kuwa ninaamini itanitangaza.
Watu kukubali kazi zako inachukua muda, lakini ubora unaweza kukufanya ukubalike. Mimi ni shabiki wa Simba, hivyo nilimtengenezea tuzo Tambwe kwanza kanifurahisha, lakini pia mchango wake kama nilivyosema. Pia niliangalia ubora kwa lengo la kujitangaza kikazi.
Hii si mara yangu ya kwanza kutoa tuzo kwa mtu au watu, nimekuwa nikifanya hivyo. Nakumbuka mwaka 2010, nilimtengenezea tuzo msanii Mrisho Mpoto na nilikuwa ninampongeza kuanzisha mashindano ya mashairi na mwanangu pia ni msanii mzuri sana.
Ubora:
Naweza kutengeneza tuzo yenye ubora zaidi ya hapo, lakini inategemea na vifaa ninavyotumia. Unajua ubora zaidi wa vifaa unaongeza kitu kuwa na thamani zaidi. Sasa mimi pia inategemea na kipato changu, lakini ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba ninatengeneza vifaa ambavyo ni bora.
Ulemavu:
Kweli kuna wale walemavu wanaamini sisi ni watu wa kusaidiwa tu, inapobidi si vibaya. Lakini kujiamini ni kitu bora sana kwa kuwa tunaweza kufanya mambo makubwa. Nayakumbuka sana majina ya (Reginald) Mengi ambaye amekuwa akitueleza kwamba tujiamini kwa kile kiungo ambacho kinafanya kazi na kukitumia.
Hivyo mimi ninajua nina viungo vipi viko kamili na vinaweza kunisaidia na kufanya mambo makubwa. Ninajiamini ninaweza kufanya mambo makubwa ndiyo maana nimekuwa si muoga na ninataka kufanya mambo ambayo huenda yatawashangaza wengi licha ya kwamba bado kipato changu hakipo juu.
Punde anasema ataendelea kusaidia kila atakapoona anaweza kufanya hivyo kwa lengo la kutimiza nia na mapenzi yake. Lakini baadaye anataka kuwa msanii wa kimataifa ambaye ikiwezekana atakuwa akichonga tuzo kubwa-kubwa ambazo watapewa wachezaji nyota kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika na ikiwezekana dunia nzima.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic