UMESIKIA
gumzo kuhusiana na wachezaji wapya wa Yanga, hasa wale raia wa Brazil, Geilson
Santana maarufu kama Jaja na Andrey Coutinho?
Jamaa hawa
ndiyo wamekuwa gumzo zaidi huku mashabiki wa Yanga wakiwa na hamu kubwa kuwaona
wakiwa wanapambana uwanjani kuisaidia Yanga kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara
na michuano ya kimataifa.
Hakuna hata
mmoja kwa Watanzania ambaye amewahi kuwaona Jaja na Coutinho wakicheza mechi ya
kirafiki au ya mashindano.
Lakini
katika mazoezi ya Yanga yanayoendelea kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya
Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam, hakuna ubishi inaonyesha kuwa ni wachezaji
ambao kama watajituma, basi watatoa upinzani kwa wengine watakaokutana na Yanga
na wanaweza kuwa msaada kwa kikosi hicho kinachoongozwa na Mbrazili mwenzao,
Marcio Maximo.
Awali
walionekana kama vile wazembe, lakini mazoezi yanavyoendelea, wanaonekana
kubadilika na kufanya vizuri zaidi. Hata hivyo wakati watakapoanza kucheza
mechi, bado pia watalazimika kuzoea mambo kadhaa kwa kuwa kuna mambo mengi kwao
ya kujifunza kupitia Ligi Kuu Bara.
Wakati yote
hayo yanasubiriwa, kuna mambo kadhaa ya kuangaliwa mapema ambayo nitagusa pande
mbili, kuanzia kwa kocha na wachezaji wenyewe na hasa wale wazalendo.
Tanzania ina
vipaji vingi sana katika kila mchezo na soka ni mmojawapo. Hakuna anayeweza
kukataa kuhusiana na uwezo wa wachezaji kama vile Jerry Tegete ambaye amekuwa
msaada mkubwa kwa Yanga kabla ya kuanza kuyumba taratibu msimu uliopita.
Umri bado
unamruhusu Tegete, kwa kuwa hajafikisha miaka 27 ambayo ungeweza kuhesabu
kwamba anaanza kuinama kwenda ukingoni, maana yake ana nafasi kubwa ya
kurekebisha alichokosea na kufanya vizuri msimu ujao.
Tegete,
Said Bahanuzi na Hussein Javu bado ni sehemu ya wachezaji
wazalendo ambao Tanzania inaweza kuwategemea katika vikosi vya timu ya taifa au
kuwa changamoto katika kuendelea kwa soka nchini.
Hivyo,
wakati wenyewe wanatakiwa kujiamini na kujituma, basi hata upande wa benchi la
ufundi linaloongozwa na Marcio Maximo linapaswa kuwaamini na kuwapa nafasi.
Sitaki
kuingilia anachokifanya Maximo, safari hii yuko kwenye klabu na si timu ya
taifa lakini bado suala la wazalendo kupata nafasi ya kucheza litakuwa ni jambo
zuri kwa kuwa ujio wa Jaja na Coutinho au wageni wengine ni kuongeza changamoto
na kukua kwa soka ya hapa nyumbani.
Hivyo
haiwezi kuwa sahihi kama watakua wageni tu na wenyeji wakabaki palepale, maana
yake soka ya nyumbani haitakuwa imepiga hatua maana baadaye wageni wataondoka
na soka ya nyumbani itaendelea kubaki hapo ilipo, haitakuwa sahihi.
Kuendelea
kuwakuza au kuwafanya kina Tegete na wenzao kuwa imara zaidi ni kuwapa nafasi
kulingana na nafasi iliyopo. Lakini bado nasisitiza suala hili linategemeana
katika pande zote mbili.
Kwamba
mwalimu atoe nafasi na atafanya hivyo akiona juhudi za upande wa pili, yaani
kwa wachezaji. Moja mazoezini, lakini pili kwenye mechi, kama watapata nafasi
basi wamuonyeshe kocha hakukosea, maana yake hivi; wafunge au kuisaidia timu
kama alivyotaka kocha au zaidi.
Pia kwa
kocha, awe ‘flexible’. Kama wageni hawafanyi vizuri, basi wasiendelee kupata
nafasi kwa lazima, badala yake nao wakutane na changamoto kwamba anayefanya
vizuri ndiye atakayepewa nafasi ya kwanza, hii itawasaidia kujituma zaidi na
kuwa msaada kwa kikosi chake.
Nyongeza ni
kuhusiana na ushirikiano, linaweza kuwa jambo zuri zaidi, kwamba kama kutakuwa
na kutopendana basi hakuna maana ya timu, hakuna sababu ya wachezaji wa kigeni
na wenyeji watafeli na mwisho kutakuwa ni kufeli kwa Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment