SALEH (KULIA) AKIWA NA NGASSA WAKATI YANGA IKIJIFUA UFUKWENI CHINI YA KOCHA MARCIO MAXIMO. |
Beki wa pembeni aliyetemwa Yanga hivi
karibuni, Saleh Abdallah, ameibuka na kusema kuwa anaidai Yanga mamilioni ya
shilingi ili kukamilisha taratibu za uvunjwaji wa mkataba wake klabuni hapo.
Saleh ambaye alisajiliwa na Yanga mara
baada ya kumalizika kwa ligi kuu msimu uliopita akitokea Azam B, alifungashiwa
virago wiki iliyopita na klabu hiyo, sababu kubwa ikielezwa kuwa ni kiwango
duni.
Saleh ameiambia SALEHJEMBE hajaridhishwa na uvunjwaji wa mkataba wake na Yanga, hivyo
bado ana haki zake za msingi kwa ajili ya kukamilika kwa zoezi hilo ikiwemo
kulipwa ada yake ya usajili pamoja na mshahara wa miaka mitatu, ambapo alisema
kuwa jumla yake ni zaidi ya Sh milioni 21.
“Unajua pale Yanga nilisajiliwa kwa
mkataba wa miaka mitatu, sasa uongozi umeniambia tu kwamba nimevunjiwa mkataba
wangu kwa kuwa kocha (Marcio Maximo) hajaridhika na uwezo wangu, sawa ila
inabidi nipewe haki yangu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuvunja mkataba.
“Bado nafuatilia haki yangu, mkataba
unajieleza kila kitu kwamba nini kifanyike kama ikitokea umevunjwa, nahitajika
kwanza kumaliziwa ada yangu ya usajili na kulipwa mshahara wa misimu miwili
iliyobaki ambayo kwa mahesabu ya haraka haraka ni zaidi ya milioni 21,” alisema
Saleh aliyeng’ara na kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka
23, Ngorongoro Heroes, iliyotolewa na Nigeria katika kufuzu Fainali za Vijana
Afrika.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza
kuwa, tayari mchezaji huyo alishapewa kiasi cha shilingi milioni tano kama
utangulizi wa ada ya usajili wake.
0 COMMENTS:
Post a Comment