July 30, 2014

MANJI


Na Saleh Ally
INAWEZEKANA hata wewe umewahi kujiuliza siku moja, kwamba Yanga na Simba ambao ndiyo wakongwe wa soka wataendelea kuishi katika mazingira duni kwa kipindi kirefu kiasi gani?
Yanga na Simba, hadi sasa zimekuwa zikifanya mazoezi kwenye viwanja vya kukodi katika shule au vyuo, ndiyo zinajiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara iliyopangwa kuanza Septemba 20, mwaka huu.
Jiulize, vipi Yanga na Simba zinakosa viwanja angalau vya kufanyia mazoezi. Sahau suala la klabu kubwa, lakini vipi mtu anataka kufanya biashara ya nguo au matunda na hasa sehemu ya kufanyia biashara hiyo.

Ninawaza utaniambia jibu, hivi; atafanya kwa kutembeza, maarufu kama biashara ya kutembeza, ile inayofanywa na kina ‘Chinga’, kama hivyo itakuwa ni kweli, basi, tukubaliane Yanga na Simba zinaendesha mpira wa ‘kutembeza’?

Sidhani kama ni sahihi kwa klabu hizo kongwe kuwa na timu zinazocheza au kushiriki mpira wa kutembeza. Nasema hivyo kwa kuwa hadi sasa zinategemea kuingiza mamilioni kuendesha timu, klabu na faida juu kupitia mpira.

Lakini hazina uhakika vikosi vyao vitajiandaa wapi zaidi ya kudandia viwanja vya vyuo, shule au maeneo mengine. Hiki si kitu sahihi kuendelea kufanya hivyo.
AVEVA

Yanga wanalipa Sh 100,000 kwa siku kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, Mabibo jijini Dar. Kama wataendelea kufanya mazoezi kwenye uwanja huo wa shule kwa miaka minne baadaye, bora wangekuwa wametengeza uwanja wao wa mazoezi.
Tayari Yanga wana eneo pale Kaunda, wakati wakiendelea kushughulikia suala lao la kuongezewa eneo ili wapate nafasi ya ujenzi wa uwanja mpya, bado wanaweza wakatengeneza sehemu tu ya kuchezea ‘pitch’ na kuepuka gharama za Sh 100,000 kwa siku ambazo ni nyingi sana kwa watu wawili ambao watakuwa wakisimamia uwanja.

Hali kadhalika, Simba wana eneo lao Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Niliona wameanza ujenzi wa uwanja huo, yaani sehemu ya kuchezea. Kama hilo ni kweli, vyema kuliharakisha na kulipa kipaumbele.

Haraka unaweza kuangalia kwamba kwa nini Yanga na Simba wanaweza kujenga viwanja vyao vya mazoezi au huenda suala hilo lingekuwa limefanyiwa kazi kitambo kama wote wangelitilia mkazo.
Usajili wa wachezaji wapya hasa wale wa nje umekuwa ukianzia zaidi ya dola 15,000 (zaidi ya Sh milioni 24.7), kwa wachezaji watano kama watasajiliwa ndani ya misimu miwili ni zaidi ya Sh milioni 120.

Lakini jiulize namna Yanga na Simba wanavyokwenda na mfumo wa ununuzi wa magari mapya kwa gharama kubwa, halafu linapofikia suala la matairi wananunua mitumba ambayo hayana uhakika katika usalama wa gari ambalo ni ghali.

Kwamba wanawasajili wachezaji kwa bei kubwa sana kutaka wazichezee timu zao. Hakuna ubishi kuwa klabu inapomsajili mchezaji kuichezea timu yake inachokuwa inataka ni matunda au sema mafanikio, si maneno.
Sasa kama mchezaji anasajiliwa mwisho anaishia kukaa nje ya uwanja kutokana na kuwa majeruhi, hiyo ni sehemu ya matumizi mabaya ya rasilimali za taasisi. Simaanishi ukiwa uwanja mzuri mchezaji hawezi kuumia, lakini uwanja mbovu, una asilimia nyingi za kuchangia wachezaji kuumia.
Vipi klabu hizo zitumie gharama kubwa za wachezaji mfano hao kutoka Burundi, Brazil, Kenya, Rwanda na kwingineko, pia ziendelee kuwalipa mishahara mikubwa, halafu wajiandae kwenye viwanja vya kubahatisha!

Makocha wote waliowahi kufundisha Yanga na Simba kwa kipindi karibu cha miaka 10 wamekuwa wakilalamika viwanja. Ernie Brandts wa Yanga ndiye ninamkumbuka zaidi kwa kuwa alionyesha kuumizwa tokea mwanzo na ubora wa viwanja.

Wakati wake, Yanga ilikuwa ‘inadandia’ Uwanja wa Bora Kijitonyama ambao unatumiwa na timu ya mtaani ya Kijitonyama. Hapa pia unaweza kujifunza thamani au maana ya klabu kongwe isivyoeleweka vizuri.

Nakumbuka nilisafiri na Simba ambao waliweka kambi nchini Oman, nikiwa huko nilielezea namna hadi timu za daraja la nne zilivyo na viwanja bora kabisa vya kufanyia mazoezi. Mwisho nikasisitiza namna klabu za Tanzania zinavyoweza kuwa na viwanja kwa kutumia gharama ndogo tu ili timu zao ziwe na uhakika wa mazoezi.

Huenda viongozi waliokuwepo awali kutokana na umri mkubwa au kutolitilia mkazo sana suala hilo waliona kawaida tu. Lakini sasa Yanga ina Yusuf Mehbub Manji, Simba ina Evans Elieza Aveva.
Sina maana ni majina tu, lakini ni watu ambao wamefanya mengi kwa maana ya mipango kisoka. Manji alifanya ukarabati wa makao makuu ya klabu yake, kukawa na mabadiliko makubwa ambayo hayakufanywa kwa zaidi ya miaka 20.
Pia amekuwa na mengi aliyofanya kama usajili wa juu kabisa, kuajiri makocha na wengine ni ghali na kadhalika. Aveva hali kadhalika, ndiye alianzisha Kundi la Friends of Simba (FOS). Hakuna ubishi kwa muda mfupi limefanya mambo mengi sana.
Achana na wale ambao wamekuwa hawapewi shukrani hata kidogo kwa FOS, lakini walichofanya na kwa kushirikiana nao pamoja na Wanasimba wengine, Aveva anaweza kuchangia kuleta mabadiliko na yakaanzia kwenye uwanja wa mazoezi.

Uwanja huo hauwezi kuwa unatumiwa na vikosi vikubwa tu vya Yanga au Simba. Klabu zote zinazungumzia programu za kukuza vijana. Haziwezi kuwa na mafanikio wakati hazina hata viwanja vya kuwakuza watoto hao.

Wakati mwingine naona Yanga na Simba, kila upande una mpango wa kupata mtoto wakati zinaishi kwa kutegemea msaada wa majirani. Wachezaji makinda wanahitaji viwanja vizuri na bora.
Manji amefanya mengi sana kwa Yanga, hata kama atakuwa shukrani hapati. Hali kadhalika Aveva na rafiki zake wa FOS. Ninaamini wanachama na mashabiki wa Yanga na Simba watakuwa tayari kuwasaidia kufanikisha hilo.

Lakini hata kama michango na kupatikana kwa fedha za klabu kutashindikana, basi niwaume sikio, mnaweza kwenda kwenye makampuni makubwa kama Coca Cola, mabeki na mengine mengi na kuwaambia wawatengenezee pitch halafu muweke mabango yao kwa miaka kadhaa na watafaidika na matangazo, tafadhali Manji na Aveva, ondoeni aibu hii.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic