Na Saleh Ally
BADO nitakuwa naendelea kukumbushia
kuhusiana na namna ambavyo nimekuwa nikihadithiwa na wazee mbalimbali wa Yanga
na Simba ambao niliomba kukaa nao kwa lengo la kujifunza.
Nimekuwa nikitaka kujua mengi
kuhusiana na historia ya Yanga na Simba, sijali sana kama wakati mwingine
inachanganya, kitu kizuri ni kwamba, nimekuwa nikijifunza mengi.
Moja ya mambo ambayo yamekuwa
yakinivutia na kunifanya nitake kujua mengi zaidi ni namna walivyoishi kwa
kushirikiana na upinzani wao ukawa ni uwanjani iwe Simba dhidi ya timu nyingine
au siku wanapokutana wenyewe watani.
Kwamba kama kuna msiba, aliyefariki ni
mwanachama au shabiki wa Yanga, basi Simba walikwenda msibani na kuwataka
wafiwa kukaa kando na wenyewe wangefanya taratibu zote za mazishi hadi mwisho.
Huo ndiyo ulikuwa mfumo wa klabu hizo,
ndiyo maana kuna mzee mmoja shabiki na mwanachama wa Simba, siku zote amekuwa
akikaa kwenye jukwaa la Yanga huku akiendelea kutaniana na mashabiki na
wanachama wa Yanga.
Kawaida, wanachama wa Yanga wamekuwa
wakimuwekea kiti kuhakikisha hakosi nafasi, ili anapofika pale aendeleze utani
wao na ukikaa karibu yake ni burudani ya kutosha.
Huo ndiyo mpira, soka ni mchezo wa raha
tupu, kweli ni biashara lakini burudani yake ndiyo imefanya uwe unaingiza fedha
nyingi hadi kujipatia umaarufu.
Nchi kama Rwanda ambazo zilivurugwa na
vita vya wenyewe kwa wenyewe, mfano wa mauaji ya kimbari mwaka 1994, zinautumia
mchezo huo kurudisha umoja, lakini ajabu hapa nyumbani wako watu, tena ni
vijana wanakwenda tofauti, haijulikani ni wapi!
Siku chache zilizopita, mashabiki wa
Simba wamechoma jezi ya Yanga yenye namba 7 ikiwa na jina la Coutinho, yule
Mbrazil ambaye Yanga imemsajili kwa ajili ya msimu ujao.
Mashabiki bao walimvua jezi hiyo
shabiki mmoja wa Yanga aliyekuwa ameivaa na kujitokeza kwenye mazoezi Simba
yaliyokuwa yanafanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kisa ni kwa nini amejitokeza kwenye
mazoezi hayo? Waliamini haikuwa sahihi yeye kwenda pale na mwisho wakamvua jezi
na kuichoma. Si jambo zuri, si jambo la kimichezo na si sahihi kwa uongozi wa
Simba kukaa kimya bila ya kusema lolote.
Waliofanya hivyo ni watu wachache sana,
wanaweza wakawa wanachafua sifa ya Simba wengi ambao wana sifa ya ustaarabu na
urafiki. Simba ina sifa ya kuwa na mashabiki na wanachama wavumilivu na waelewa
zaidi kwenye soka, kwamba timu yao imecheza vipi na si walalamishi kupita
kiasi.
Hawa wengine wametokea wapi? Tena
wanafikia hatua ya kuchoma jezi ya timu pinzani, hali inayoashiria uhasama,
uadui ambao unawashawishi wengine pia kujibu mapigo na mwisho itakuwa ni
kuumizana. Nani amezungumza na kukemea hilo?
Jambo ambalo limefanywa na watu wasiojua
michezo na hasa wa soka maana yake nini, watu ambao hawajui historia au
chimbuko la Simba na Yanga na namna walivyoishi huko nyuma hadi wao wakazikuta
timu hizo sasa.
Wamechoma jezi, eti shabiki wa Yanga
ameenda mazoezi ya Simba kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Dar es Salaam. Hawaoni
matumizi ya viwanja vya chuo hicho, watu wangapi wanafanya pale? Kuna tenisi,
judo, kikapu, netiboli na mingine. Je, ni kiwanja cha Simba? Hata kingekuwa,
vipi iwe hivyo, hawa watu vipi?
Kawaida nafanya mazoezi kwenye viwanja
vya Chuo Kikuu Dar es Salaam tangu nikiwa ‘kula kulala’ hadi leo najitegemea.
Hakuna suala la rangi na si uwanja wa klabu, hivyo mashabiki waliofanya hivyo
watakuwa ni wageni katika jiji hili au eneo hilo. Ndiyo maana nataka wajifunze
ili siku nyingine wasichafue sifa nzuri ya Simba, undugu wa Yanga na Simba na
amani ya soka nchini.
Angalia sura na maumbo yao, hakuna
ubishi ni vijana na sura zao ni za kisasa. Lakini wana mawazo duni kuhusiana na
mchezo wa soka ambao umekuwa ukitumika kumaliza uadui na uhasama na mwisho
kurudisha umoja, lakini wao wanautumia kujenga uadui tena, watu wa aina gani
hawa wasio na haya wala kutaka kujifunza?
Inawezekana wengi wanalichukulia tukio
hilo kama utani, lakini ni baya na linaweza kuwa tatizo kubwa, pengine ingekuwa
vizuri kusikia hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likifumbua mdomo na
kusema jambo kuhusiana na suala hilo.
Kwangu nitakuwa nina maombi mawili,
naanza na upande wa vijana kwa kuwa bado nipo kwenye kundi hilo. Kuwa ni vizuri
kuachana na ushabiki wa fuata mkumbo au kutaka sifa. Wapo mashabiki wanaokuwa
wendawazimu wanapokuwa mbele ya wenzao na wanataka kuonyesha wanazijua au
kuzipenda sana timu na klabu zao.
Ukiwauliza, hawajalipa ada au si
wanachama kabisa. Ikiwezekana hawajawahi kuiunga mkono Simba au Yanga kwa
lolote lile. Badala yake vitendo vya kipuuzi au maneno mengi tu, lengo
kuonyesha wanajua sana, kumbe hakuna lolote!
Nawaomba vijana, wanaoshabikia soka na
hasa Yanga na Simba, kuachana na tabia za sifa zisizokuwa na mpaka, tabia za
kutaka kuonekana sana kwenye makundi ya watu, mwisho wake zina madhara na faida
zake ni chache sana.
Pili, kwa mashabiki na wanachama wa
Yanga, wanapaswa kulichukulia suala hilo la mashabiki wa Simba kuchoma jezi ni
la kipuuzi, lililofanywa na watu wasioelewa lolote.
Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
ni sehemu ya watu wote, hivyo waamini Simba wengi hawatakuwa wamefurahishwa na
hilo na wao Yanga hawana sababu ya kulichukulia kwa uzito na mwisho kulipa
kisasi.
Wajue wakilipa kisasi, watamuumiza
Simba ambaye hakushiriki kwenye tukio hilo. Wanaweza kulaani kilichotokea kwa
lengo la kuonyesha njia na mwisho kurekebisha, lakini si kulipa kisasi.
HAWA KAKA NI WATANI WAJADI WALA HAKUNA MBORA HAPA NI KWAHI TU NA UTANI HAUNA KISASA WALA KIZAMANI, LAKINI SHABIKI UNAUMIA,MWANACHAMA UTANI
ReplyDelete