RASMI!
mambo yamekamilika na sasa timu ya magwiji au wakongwe wa klabu ya Real Madrid
ya Hispania itatua nchini Agosti 22, mwaka huu kwa ajili ya kucheza mechi ya
kirafiki dhidi ya kikosi maalum cha nyota wa Tanzania Agosti 23.
Magwiji
hao wanaotarajiwa kuongozwa na Zinedine Zidane, Luis Figo, Ivan Helguera na
wengine wengi watakuwa na ziara ya siku nne nchini ikiwa ni pamoja na
kutembelea mkoani Arusha kwa ajili ya kutazama vivutio vya utalii.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, meneja wa ziara hiyo, Denis
Ssebo, amesema kwamba mpaka sasa ziara hiyo ina idadi ya watu 50, wakiwemo wachezaji
wenyewe na viongozi wao 27 pamoja na mashabiki 23 waliojitokeza kutaka kuongozana na mastaa hao
lakini alisisitiza kuwa idadi inaweza kuongezeka kulingana na maombi ya mashabiki
hao.
Aidha,
aliongeza kuwa timu ya Tanzania itakayocheza na mastaa hao kwenye Uwanja wa
Taifa itaundwa na wachezaji kutoka Taifa Stars, huku kocha wa kikosi hicho
akiwa ni Kocha Mkuu wa Stars,
Mholanzi Mart Nooij.
“Kikosi
cha magwiji au wakongwe wa Real Madrid kitatua rasmi Agosti 22, na kitakuwa na
ziara ya siku nne ambapo Agosti 23, kitacheza mechi ya kirafiki dhidi ya kikosi
maalum cha Tanzania kitakachokuwa chini ya kocha mkuu wa Stars.
“Baada
ya hapo Agosti 24, wataelekea Arusha kwa ajili ya kujumuika pamoja na wakazi na
mashabiki wa kuangalia vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani humo.
“Baada
ya hapo Agosti 26 watakwea pipa kurejea kwao, viingilio vya mechi hiyo bado
havijatangazwa lakini itakuwa ni vya chini kwa ajili ya kumuwezesha kila Mtanzania
kuushuhudia huo mtanange,” alisema Sssebo.
0 COMMENTS:
Post a Comment