Na Saleh Ally
SIKU zinavyosonga mbele na
mambo yamekuwa yakibadilika kwa kila namna, hivyo kila jambo linafanyika katika
mfumo unaolenga ushindani zaidi.
Ushindani umekuwa mkubwa
karibu kwenye kila jambo kwa kuwa kinacholengwa ni mafanikio na mambo mengi
zaidi yanakwenda kibiashara.
Hata kabla ya mechi hiyo
nilieleza namna ambavyo tunaweza kujifunza badala ya kwenda kuangalia tu
muonekano wa sura za akina Luis Figo, Cristian Karembeu na wenzao.
Wakati nakwenda uwanjani
nilitamani kujifunza mengi na nikiwa pale kweli hilo lilitokea ingawa kuna
jambo niliona lilikuwa ni sahihi kulijadili kwa pamoja na wadau wa soka kwa
ajili ya maendeleo ya mpira wetu.
Mashabiki walijitokeza kwa
wingi sana siku hiyo, inawezekana iliwashangaza wengi sana kuona mechi tu ya
wakongwe inahudhuriwa na watu wengi namna ile.
Karibu kila aliyefika
uwanjani pale alionyesha kushangazwa na idadi ile kubwa ya mashabiki ingawa
wako waliokuwa wakiwazia mengine, eti “waandaaji wamepiga mkwanja aisee”.
Kwa kuwa waandaaji
walipambana hadi kufikia kuwaleta Madrid kitu ambacho kilionekana hakiwezekani,
basi wana haki ya “kupiga” hizo fedha kama kweli itakuwa hivyo.
Hilo si la msingi sana
ingawa tunaweza kujifunza pia. Ila suala la mashabiki kujitokeza kwa wingi na
wengi wakiwa ni wageni wa Uwanja wa Taifa, hilo ndilo linaweza kuwa moja ya
mafunzo makubwa.
Nimekuwa kati ya wadau
wanaojitokeza Uwanja wa Taifa mara kwa mara kwenda kuangalia mechi mbalimbali.
Siku hiyo niliona sura nyingi mpya ambazo ninaweza kushindwa kufafanua vizuri
lakini nitajitahidi.
Idadi kubwa ya mashabiki
hao iliyojitokeza ilikuwa ni ya raia wa kigeni kutoka katika nchi za Ulaya
ambao mara chache wamekuwa wakijitokeza kuangalia mechi za ligi za hapa
nyumbani hasa Ligi Kuu Bara.
Wengine walikuwa ni
Watanzania wenye asili ya Bara la Asia ambao pia walijitokeza kwa wingi sana
pale uwanjani na kufanya muonekano wa baadhi ya majukwaa uwe tofauti na siku
nyingine zilizopita.
Pamoja na hivyo, wengi
waliofika uwanjani hapo, walifika wakiwa na familia zao kama wake na watoto zao
na wakaishuhudia mechi hiyo kwa furaha kubwa mwanzo hadi mwisho.
Hapa ndiyo tunaweza
kujifunza haraka na huenda Yanga, Simba, Azam FC na wengine wanaweza kuwa na
kazi ya kuanza kufanya ubunifu kuhakikisha wanawapata watu hao katika mechi za
ligi na zile za kimataifa.
Usiseme haiwezekani kwa
kuwa wale walikwenda kumuona Figo, bado Simba, Yanga na Azam FC zinapaswa
kufikiria mambo kibiashara zaidi na sasa ziamini kuwa kuna mashabiki hupenda
kwenda uwanjani lakini wanashindwa na vikwazo ni vipi?
Hakuna ubishi klabu za
Tanzania zinahitaji mapato zaidi kujiendeleza, lakini zimekuwa hazifanikiwi
kupata watu hadi zinapocheza Yanga na Simba tu na zenyewe si kila mechi. Mapato
ni sehemu ya mhimili wa kujiendeleza kwa maana ya malipo mazuri kwa wachezaji,
makocha na pia maendeleo kwa ujumla.
Hivyo ni lazima kubuni
kupata mashabiki wengi na mambo muhimu ni soka bora na la kuvutia kupitia
vikosi vyao na lazima liwe na nidhamu ya juu.
Pili kuangalia suala la
bei, kwamba Watanzania watakuwa wanaweza kujitokeza lakini kuwe na utaratibu wa
kuamini hiyo ni biashara, basi zijitangaze na kuelezea ujio wa mechi fulani au
jambo linalokuja.
Lakini kwa mashabiki wa
Yanga au Simba, au wengine ambao wamekuwa wakija uwanjani kwa wingi wanapaswa
kujua kuwa wao pia ni tatizo kwa kuwa wako wanaoamini kutukana matusi ndiyo
ujanja.
Si lazima kila mmoja kutoa
lugha chafu ili kujionyesha ni ‘mwenyeji’ wa Uwanja wa Taifa au unazijua sana
Yanga na Simba. Hali hii imekuwa ikiwakwanza wengi na kushindwa kupeleka watoto
wao uwanjani.
Taifa kumekuwa na vurugu
hata zisizokuwa na sababu za msingi, ili mradi kuna watu wengi wapenda sifa
hupenda kuonekana hasa wanapoona kundi kubwa la watu. Kupigana au kuvuana nguo,
jambo ambalo si rahisi kusikia linatokea kwingine kwa kuwa ni la kijinga!
Hivyo ni lazima kuwe na
mabadiliko, watu wanakwenda kuangalia soka na si kusikiliza matusi ya wapenda
sifa. Wako watu wengi wanapenda kwenda uwanjani na viingilio vyao vingekuwa
faida kwa klabu zetu lakini mambo niliyoyataja ni sehemu ya vikwazo.
0 COMMENTS:
Post a Comment