October 20, 2014

WILLIAM LUCIAN 'GALLAS'..

Na Saleh Ally
KATIKA mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa juzi Jumamosi jijini Dar es Salaam, ungeweza kuangalia mambo mengi sana ambayo yanaweza kuwa burudani au mafunzo.


Kwanza kabisa ni idadi kubwa ya mashabiki waliojitokeza na kuonyesha kuwa kweli klabu hizo mbili ni kubwa, zimebeba furaha na majonzi ya watu na hakuna ubishi kuna kila sababu ya kuhakikisha zinabadilika ili kuwaridhisha mashabiki na wanachama wao.
 
SAID NDEMLA...
Wamejitokeza kwa wingi sana, wameonyesha wanaziamini na kuzipenda, hilo ni deni kubwa na zinapaswa kuwalipa kwa kuonyesha soka la uhakika na ushindi ili kuzifurahisha nyoyo zao. Anayekupenda, mpende pia.

Lakini kuna somo tunalolisubiri, maana kila mara kumekuwa na malalamiko ya uchakachuaji wa mapato, hatujui ni klabu zenyewe, wadau wake au mashirikisho na vyama vinavyosimamia, limekuwa ni jambo la siri.

Kwa kuwa juzi mashabiki wamejitokeza kwa wingi sana huku tiketi za kielektroniki zikitumika na ndizo zinazoaminika kwamba ni salama katika suala la mapato, sasa acha tusubiri.
 
MKUDE (KULIA) AKIPAMBANA NA JAJA.
Kweli mengi yalikuwa ya kuangalia kama hayo ya mwanzo, lakini kubwa ni rekodi waliyoiweka Simba kuwachezesha vijana saba katika mechi ngumu, wakitokea katika presha kubwa ya sare tatu mfululizo, lakini wakathubutu kwa ajili pia ya soka ya Tanzania hapo baadaye.

Simba ilianza mechi hiyo ikiwa na wachezaji sita makinda, kati ya hao ni watano ambao wamelelewa katika timu B hadi kufikia kiwango kizuri. Mchezaji wa sita, alikuwa ni kipa Peter Manyika.

Waliokuwa Simba B na walianza katika kikosi cha kwanza ni William Lucian ‘Gallas’, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Haruna Chanongo na Saidi Ndemla.

Usisahau baadaye, Simba ilimuingiza Ramadhani Singano ‘Messi’, hivyo kutimiza nafasi ya wachezaji makinda saba katika dakika 90 dhidi ya Yanga ambayo haikuwa na mchezaji kinda hata mmoja katika kikosi chake.

Listi ya Yanga iliyoanza ilikuwa hivi; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Geilson Santana ‘Jaja’, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho.

Wachezaji wote walioanza katika kikosi cha Yanga ni wale waliojiunga na timu hiyo tayari wakiwa na uzoefu wa ligi kubwa. Hakuna aliyekuzwa Yanga kisoka kama ambavyo ilikuwa kwa Simba kwa makinda hao sita.

Lengo si kuonyesha Yanga walikosea, lakini kuwafumbua macho hata wao kwamba falsafa ya kukuza vijana ina faida yake. Hata kama si Simba iliyowaanzisha makuzi ya kisoka, lakini vijana hao kuchipukia, wamepata nafasi wakiwa na Simba.

Kama Yanga itakuza vipaji, Simba ikaendelea kufanya hivyo, kuna nafasi kubwa ya kutengeneza vijana wengi waliokuzwa kiushindani, mwisho kutakuwa na wachezaji wengi wanaochuana kusajiliwa na mwisho kuisaidia timu ya taifa kuwa na nafasi ya uchaguzi zaidi.

Tanzania haina wachezaji wengi wanaocheza nje, hivyo timu ya taifa inategemea wengi wa nyumbani. Ili ifanye vizuri pia inatakiwa kuwa na wachezaji bora wa hapa nyumbani na hakuna ujanja, kuwakuza wachezaji sahihi ni lazima kujali vijana.

Mfano wa timu nyingi zinazofanikiwa kupitia vijana upo, angalia Arsenal na Barcelona. Huenda Yanga inakwenda kwa falsafa ya Chelsea ambayo kupitia makocha kama Jose Mourinho, inataka watu wa ushindi na kuleta makombe.

Yote yanawezekana, lakini bado kunatakiwa kubadilishwa kwa mfumo na wachezaji makinda wapewe nafasi kama ilivyofanya Simba. Hakuna anayeweza kubisha kwamba walicheza vema na kuonyesha uwezo wa juu.

Kutoa nafasi ni jambo zuri kwa kuwa linatoa nafasi ya kugundua, kwamba waliopewa nafasi wanaweza kweli au hawawezi kabisa ili utaratibu mwingine ufanyike. Wakiweza inakuwa faida na makinda wa Simba wameonyesha.

Usisahau wakati Simba inacheza, kwenye benchi kulikuwa na nyota wawili wa kimataifa. Amissi Tambwe na Pierre Kwizera ambao sasa wanalazimika kupambana kupata namba.

Kama wameweza kucheza vizuri kwenye mechi hiyo ya presha, maana yake wamekua kutokana na kujifunza kitu na itawajenga kujiamini na kuweza kuwa huru kufanya mambo waliyonayo. Hiyo ndiyo faida kwao, kwa klabu na taifa letu. Vijana wanaweza, wapeni nafasi. Msisahau, bila ya nafasi, kipaji hakiwezi kuonekana.



1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic