October 31, 2014


Mshambuliaji nyota wa Simba, hiyo, Amissi Tambwe, ameamua kufunguka na kuweka wazi sababu zitakazomuondoa klabuni hapo.


Tambwe amesema yupo tayari kuondoka Simba licha ya kuwa bado anaipenda klabu hiyo lakini sababu kubwa ni maneno anayosingiziwa na manyanyaso anayopata klabuni hapo.

“Kabla ligi haijaanza, nilipatwa na hofu baada ya kuambiwa kuwa uongozi unataka kuachana na mimi ili nafasi yangu ichukuliwe na (Emmanuel) Okwi, hali hiyo ilinifanya nipoteze mudi ya mazoezi kutokana na kutumia muda mwingi kufikiria hali hiyo.

“Baada ya siku chache, viongozi hao waliibua jambo jingine tena, hilo lilikuwa ni lile la kuniondoa katika orodha ya wachezaji watakaosafiri kwa ndege kwenda Mtwara katika mechi dhidi ya Ndanda FC, si unakumbuka?

“Nilisafiri kwa basi kwenda na kurudi huku wenzangu wakipanda ndege, hakika niliumia sana.

“Lakini kitendo cha hivi karibuni cha kunisingizia kuwa ninaihujumu timu pia kinanifanya niwe na wakati mgumu na kujikuta nikitumia muda mwingi kufikiria mambo hayo, ndiyo maana kiwango changu kimeshuka ukilinganisha na msimu uliopita ambao nilikuwa na amani,” alisema Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Kuhusiana na mpango wa kujiunga na Yanga, Tambwe alisema: “Habari hizo za kujiunga na Yanga hazina ukweli wowote na zinalenga kutaka kunichonganisha na viongozi wangu, mimi ni mali ya Simba.

“Ndiyo, Yanga waliwahi kunihitaji lakini hiyo ni zamani, siyo sasa, walinifuata msimu uliopita nikawaambia wafuate taratibu zinazotakiwa kwa kuwa nilikuwa bado nina mkataba mrefu na Simba. Kama bado wana nia na mimi wafuate tu mchakato unaotakiwa.”

Akizungumzia juu ya Tambwe kuondoka klabuni hapo, Ofisa Habari wa Simba, Humphrey Nyasio, mapema wiki hii alinukuliwa akisema:

“Tambwe bado ni mchezaji wetu na ataendelea kuwa klabuni hapa kwa kipindi chote cha mkataba wake na bado tunamhitaji.”




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic