November 24, 2014


Na Saleh Ally
KUWA mkweli ni tabu, lakini nianze na kusimamia kuhusiana na mshambuliaji Geilson Santana ‘Jaja’ aliyekuwa akikipiga Yanga.
Santana, raia wa Brazil, ameamua kubaki kwao Brazil, kuna mengi yanasemwa kuhusiana naye kwamba yeye ameamua, wengine uongozi umeona aende, familia yake imeona asirudi Tanzania lakini ukweli, hataichezea Yanga.


Mipango ya kuziba pengo lake imeanza, kiungo Mbrazil, Emerson De Oliveira Neves Rouqe, anatua nchini kesho kuanza majaribio, akifuzu atapewa nafasi ya kuziba pengo la Jaja, akionekana hawezi, basi safari imemkuta na Yanga itasaka straika DC Congo au Zambia.


Nilimsikia mmoja wa wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, akisema kuwa wamefurahishwa na kuondoka kwa Jaja kwa kuwa katika mechi saba za ligi alifunga bao moja. Tena alikuwa mshambuliaji asiyegombea mpira.

Kauli hiyo ya Akilimali imekuwa ikizungumzwa na mashabiki wengi wa soka ambao huenda wamekuwa wakikubali kusikiliza tu wanachoelezwa bila ya kufanya tathmini.

Usimlaumu mzee Akilimali, wala usiwashangae wanaosema Jaja alikuwa anaweza. Ishu ya msingi tujifunze kuwa, baada ya kuondoka tuliona nini kwake.

Hakuweza kupambana kugombea mpira, hilo alifeli. Lakini alikuwa bora kwenye kufunga na mabao yake matatu yanajibu maswali zaidi ya mia aliyotuachia. Nani amejifunza ambaye anaweza kufaidika na walichopatia na kukosea Yanga kwa kumleta Jaja?

Je, Jaja angepewa ushindani zaidi, mfano Kocha Marcio Maximo akawa anawapanga akina Jerry Tegete au Hussein Javu, halafu yeye akaingia baadaye ingekuwaje?

Wanaosema alikuwa ni mbovu, takwimu zinaonyesha vipi? Kwamba kweli alifeli kupita wote na hakuwa ni mwenye viwango?

Huenda ni hisia, lakini ukisema mechi zinazotambulika, achana na zile za kirafiki, Jaja aliichezea Yanga mechi nane. Moja ya Ngao ya Jamii na saba za ligi.

Amefunga mabao matatu katika mechi saba. Akianza na kufunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Azam FC, Yanga ikabeba ngao.

Katika ligi, mambo yalikuwa magumu hadi alipofunga dhidi ya Stand United mjini Shinyanga wakati Yanga ikishinda kwa mabao 3-0, mawili yakiwa yamefungwa na Jerry Tegete.


Kukimbia:
Huenda mashabiki wengi hawakufurahishwa na Jaja kutokuwa na mbio, kutopambana au kuonekana mshambuliaji mwenye mikiki na vurugu.

Huenda naweza kuungana na mashabiki au watoa tathmini, kuwa Jaja hakuwa akipambana, jambo ambalo niliamini angeweza kubadilika kama angetaka na kucheza soka bora baadaye.

Lengo si kuwalaumu Yanga au mtu mwingine, ila kupitia mshambuliaji huyo, licha ya kuondoka, bado tunaweza kumtumia kama somo.

Mabao:
Alifunga mabao matatu katika mechi zinazotambulika na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Angalia mabao yake matatu, mawili katika mechi dhidi ya Azam. La kwanza akifunga katikati ya mabeki wawili na kipa, akajirusha na kuuguza mpira kiufundi.

Bao la pili, hii itabaki zawadi ya muda mrefu kwa mashabiki wa soka. Baada ya kupewa pasi, alitulia na kumuangalia kipa, kwa ujasiri mkubwa akauchota mpira, ukajaa wavuni.

Bao la tatu, mechi dhidi ya Stand kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Jaja huku akiwa anaangalia upande wa lango lake, akageuka kama mshale na kuachia shuti lililojaa wavuni.

Hakuna anayeweza kubisha kwamba Jaja alifunga mabao matatu, yote yakiwa kwenye kiwango cha “yanayoweza kufungwa na straika anayejua tu.”


Viwanja:
Kingine ni kwa viongozi, kwamba wanaweza kujadili na kuangalia kwamba kwa wachezaji kutoka mabara ya Ulaya, Asia na Amerika Kusini wanaweza kupata kazi kutamba hapa nyumbani.

Ukiachana na viwanja vya Taifa na Azam Complex, Chamazi vyote vya jijini Dar es Salaam, uwanja pekee wenye ubora mzuri ni Kambarage, Shinyanga.

Jaja amefunga mabao kwenye viwanja vyote vyenye kiwango kizuri. Ingawa Taifa alifunga mabao mawili tu, lakini hakuna ubishi alifunga. Hivyo kuna tabu na viwanja vyetu na Jaja ameondoka akituachia somo kwamba lazima TFF na Bodi ya Ligi wasimamie ubora wa viwanja ili timu zisajili wachezaji kutoka kwingine ikiwezekana Ulaya, la sivyo, watakuja hapa kuchekesha tu.

Suala la kusimamia viwanja vikawa bora linawezekana, tumeona Shinyanga hawakuwa kwenye ligi. Wamerejea na uwanja wao tayari uko bora kuchezewa. Vipi kwingineko washindwe?

Wanaomzidi Yanga:
Simon Msuva mwenye mabao matatu na Jerry Tegete mwenye mabao mawili. Wachache wana bao moja kama Jaja (kwenye ligi), hivyo hakuwa mbali na kujirekebisha na huenda kama angepewa changamoto, angeweza kufunga zaidi.

Wageni wenzake:
Ukizungumzia wachezaji wa kigeni, anza na mfungaji bora wa msimu uliopita, Amissi Tambwe kutoka Burundi, hadi ligi imesimama alikuwa na bao moja kama ilivyo kwa Jaja.

Wageni wengine ambao walikuwa wana bao moja hadi mechi saba zimepigwa kwa kila timu ni Kipre Tchetche (Azam FC-Ivory Coast), Haruna Niyonzima (Yanga-Rwanda), Andrey Coutinho (Yanga-Brazil), Yayo Lutimba (Uganda) na Itubu Imbemu (Coastal-DR Congo).

Kwa kuwa hata wageni hawa wana bao moja, huenda wanaweza kujirekebisha na kufunga mabao zaidi katika mechi sita zilizobaki za mzunguko wa kwanza na 13 za mzunguko wa pili.

Wanaoongoza:
Wanaoongoza ni wale wenye mabao manne kila mmoja ambao ni Danny Mrwanda (Polisi Moro), Didier Kavumbagu (Azam FC), Rashid Mandawa (Kagera), Rama Salim (Coastal) na Ame Ali (Mtibwa Sugar).

Bado hakuna tofauti kubwa kutoka bao moja hadi manne. Utaona katika wafungaji watano wa mabao manne kila mmoja, kuna wageni wawili na wenyeji watatu.

Kavumbagu kutoka Burundi, huu ni msimu wake wa tatu Ligi Kuu Bara, Salim anayetokea Kenya, amefanikiwa kwa msimu wa kwanza kuanza vizuri lakini utaona hakuna tofauti kubwa Kenya na Tanzania kiuchezaji.

Mwache aende:
Mwisho mwache Jaja aende, lakini bado alihitaji muda kuzoea mazingira ya soka ya Bongo. Maana hata Coutinho pamoja na kasi, chenga, bado amefunga bao moja tu la mkwaju wa faulo, hii inathibitisha muda ulitakiwa.

Wakati anakwenda Jaja, vizuri kujifunza kama nilivyoeleza awali. Lakini Mbrazil huyo kama tukikubali kujifunza kupitia kwake bila ya kujali Uyanga, Usimba basi kuna faida hapo baadaye. Tukipuuza, basi tutaendelea kubaki kama jana.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic