December 20, 2014



Na Saleh Ally
WAKATI fulani kulizuka mzozo mkubwa sana kati ya mmoja wa viongozi wa wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali na mchambuzi wa michezo wa Clouds FC, Shaffi Dauda na ishu kubwa ilikuwa Kocha Marcio Maximo.


Taarifa zilizagaa kwamba Dauda alimzuia Maximo kuja kuifundisha Yanga wakati klabu hiyo ikifanya juhudi za kumnasa kutoka kwao Brazil. Ilielezwa Dauda alimueleza akija Tanzania kuifundisha Yanga ataaibika bure.

Baadaye ilionekana Akilimali alikosa ukweli, mwisho akamuomba Dauda aliyekuwa ametishia kwenda mahakamani yaishe. Naye akamsikiliza mzee wake na kufunika kombe.

Baadaye Yanga ilimpata Ernie Brandts akaja kufanya kazi yake. Alitimuliwa katika mechi iliyopita ya Nani Mtani Jembe, nafasi yake ikachukuliwa na Hans van der Pluijm, akaondoka halafu akaja Maximo, naye ametimuliwa kwenye Nani Mtani Jembe 2, mwaka huu.

Hesabu zinaonyesha tangu tafrani la Dauda na mzee Akilimali, hadi Maximo anaajiriwa na kutimuliwa, haujavuka hata msimu mmoja! Kweli amevunjiwa heshima yake.


Tuanze kwa kuangalia hesabu sahihi za mechi na michezo kama kweli kocha huyo Mbrazili aliyewahi kuinoa Taifa Stars alistahili kufutwa kazi na uongozi wa Yanga au ulifanya mambo yake kwa jazba tu!


Msimamo:
Wakati Maximo anatupiwa virago, tayari Ligi Kuu Bara ilikuwa imechezwa kwa mechi saba kwa kila timu. Yanga ilikuwa katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 13, ambazo ni mbili pungufu dhidi ya vinara Mtibwa Sugar.

Ukirudi kwenye mabao ya kufunga, Yanga ina 9, inashika nafasi ya pili baada ya vinara Mtibwa Sugar wenye 10.

Kwenye kufungwa, pia haikuwa na safu imara sana lakini si mbovu kwa kuwa imefungwa mabao matano wakati vinara Mtibwa wamefungwa matatu tu na ndiyo timu iliyofungwa mabao machache zaidi.
 
Maximo Vs Phiri, Omog:
Hadi anaondolewa, Maximo ndiye kocha wa kigeni aliyekuwa juu zaidi kwenye msimamo kuliko makocha wengine wote.

Joseph Omog wa Azam FC, aliongoza kikosi chake katika mechi saba akafanikiwa kufikisha pointi 13 kama za Maximo lakini akabaki katika nafasi ya tatu kutokana na mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam FC ilifunga mabao nane ikaruhusu manne, maana yake safu zote mbili za ushambulizi na ulinzi zilikuwa dhaifu ukilinganisha na zile ya Yanga.

Yusuf Chippo raia wa Kenya, yeye aliiongoza Coastal Union kushika nafasi ya nne, ikiwa na pointi 11. Ilifunga mabao 9 kama ya Maximo na kufungwa saba.

Mganda, Jackson Mayanja wa Kagera Sugar alishika nafasi tano akiwa na pointi 10, alifunga sita na kufungwa nne.

Patrick Phiri kutoka Zambia, aliiongoza Simba kuangukia nafasi ya saba katika mechi saba ikiwa imefunga mabao saba na kufungwa sita.

Kocha mgeni ambaye kikosi chake kimefeli kabisa ni Tom Olaba raia wa Kenya ambaye baada ya mechi saba, Ruvu Shooting ilishika nafasi ya 12, ikiwa na pointi 6 tu, imefunga mabao 6 na kuchapwa 7.


Kwa maana ya hesabu au takwimu za michezo, hakika Maximo alitakiwa kuwa kocha mgeni wa mwisho kutimuliwa nchini kama ungechukua wageni wote wanaofanya kazi ya ukocha katika Ligi Kuu Bara.

Unaweza kusema angekuwa na nafasi ya kujirekebisha baada ya hapo na hasa baada ya Yanga kufanya usajili kujiimarisha lakini safari imemkuta.

Rekodi:
Kwa upande wa rekodi nzuri na mbaya, huenda zimechangia kwa Maximo kuondolewa nchini.

Maximo hashauriki, Maximo mbishi na anajua kuliko yeyote, huenda akawa na ‘haki’ ya kumdharau kocha yeyote nchini kwa kuwa anatokea Brazil.

Imekuwa ni siri, lakini wasaidizi wake na wengi walio kwenye benchi la ufundi hawakufurahia uongozi wake wa kibabe, hakupenda kushauriwa na kwa kuwa ni kocha mkuu, basi alikuwa ni mwenye kauli ya mwisho.

Aliwahi kuonyesha tabia kama hizo vikiwemo visasi wakati akiwa Taifa Stars. Watu wakamtetea lakini huenda wakati huu ulikuwa mzuri kuonyesha vizuri upande wa pili wa shilingi ya Mbrazili huyo.

Hakuna anayefanikiwa bila ya kushirikiana na wenzake, hakuna anayeweza kukibadilisha kitu kwa kuonyesha anajua peke yake. Ushirikiano ndiyo namba moja.

Hakuna ubishi kwamba wako watu wenye vipaji katika soka, uandishi na kazi nyingine lakini wanaweza kushindwa kufika mbali kutokana na tabia zao za kibinadamu na hasa ujeuri au viburi.

Kwa tathmini hii, kwa hesabu zinaonyesha bado Maximo alipaswa kubaki Yanga. Kitabia kuanzia kwenye enzi za Taifa Stars, acha tu Maximo aende kwao.


3 COMMENTS:

  1. Tatizo lako Saleh usimba umekujaa sana hata kuona vilivyohai huwezi,wewe ongelea mambo ya Ndumbaro anayekuweka mjini ya Yanga waachie akina bin Zubeir!

    ReplyDelete
  2. Saleh yuko sahii sana tu

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hata mimi ni shabiki wa Yanga, ila Salehe kiukweli ni mwandishi mzur. Nakuunga mkono Salehe ameongea ukweli kabisa.

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic