January 26, 2015


Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, ametoroka nchini na kukimbilia kusikojulikana huku viongozi wake wakijua kuwa amekwenda Tanga kwa ajili ya msiba wa mamamkwe wake.



Ngassa hajaonekana Yanga tangu Jumanne ya wiki iliyopita. Aliwaaga viongozi wa klabu hiyo kuwa anakwenda Tanga kuhudhuria msiba lakini taarifa zinadai ametoroka nchini.

Chanzo chetu cha habari kimesema winga huyo ameonekana akipanda ndege kuelekea Afrika Kusini.
 
SIKU NGASSA ALIPOKWENDA TFF KUPELEKA FEDHA SH MILIONI 30 ALIZOKUWA AKIDAIWA NA SIMBA.
Bado haijawekwa wazi kuwa amekwenda kufanya nini lakini inaaminika amekwenda katika Klabu ya Free State ya Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

Championi Jumatatu ilipomuuliza katibu wa klabu hiyo, Dk Jonas Tiboroha, alisema Ngassa aliwaaga kuwa anakwenda msibani Tanga ambapo alifiwa na mamamkwe na si vinginevyo.

“Sisi alituaga kuwa alipatwa na matatizo ya kifamilia, kwamba alifiwa na aliondokewa na mamamkwe wake, kama ni hizo habari nyingine binafsi sina,” alisema Dk Tiboroha.

Chanzo cha habari chetu kilikwenda mbali na kusema kuwa, uongozi hautaki kuliweka wazi suala hilo ingawa wameandaa adhabu ya kutosha kama fundisho kwa wachezaji wengine kwa ukosefu wa maadili ya kikazi.

“Kuna watu walimuona akipanda ndege ya Sauz, kwa hiyo viongozi wanasema bado wanalichunguza kwa umakini ili wajiridhishe kuhusu safari yake na iwapo itabainika kweli alikuwa Sauz, kitakachomkuta  ni siri yao, ila ni adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa wenzake wanaofanya mambo ya Kiswahili,” kilisema chanzo chetu.

Ngassa alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi ambayo amekuwa akiitumia Tanzania, hakuweza kupatikana kwa siku nzima ya jana, hali inayoonyesha kuwa hayupo nchini.

Kwa siku za hivi karibuni, Ngassa amekuwa katika mgogoro wa chinichini ya Yanga, hasa kutokana na uongozi wa klabu hiyo kukiuka makubaliano ya kumlipia kiasi cha Sh milioni 45 anachodaiwa na Simba kutokana na adhabu aliyopewa na TFF kwa kusaini klabu mbili mwaka 2013.


Yanga ilikuwa imekubaliana na kiungo huyo kwamba itamlipia nusu ya deni wakati alipokuwa akisaini kuichezea Yanga mwaka 2013 na kiasi kingine watakuwa wakimkata kidogokidogo kwenye mshahara lakini badala ya kumkata Sh 500,000 kama makubaliano yalivyo, wamekuwa wakimkata Sh 1,000,000 hali inayodaiwa kumuondolea morali na kumfanya acheze chini ya kiwango. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic