January 28, 2015


KATIKA miaka ya 1990, mwamuzi mmoja alipokea rushwa wakati Pan African ikiwa na mechi dhidi ya Simba. Baada ya hapo alichukua fedha hizo na kuzipeleka kwa wachezaji.


Mwamuzi alizikabidhi fedha hizo kwa nahodha wa Pan African na kumwambia amehongwa na viongozi wa klabu yao, lakini wao ndiyo wanaocheza hivyo wazigawane.
Lakini hadi sasa kuna mwamuzi mmoja tu anajulikana hata na viongozi wa soka, huyu anaitwa Crina Kabala, uhakika hachukui rushwa.

Kabala ni mlokole, amekuwa akikataa kuchukua fedha hizo na taarifa zinaeleza timu nyingi hazitaki kuchezeshwa na mwamuzi huyo kwa madai anakosea sana na hajui sheria 17 za soka!

Nani anaweza kukataa kuhusiana rushwa kutembea katika mechi za Ligi Kuu Bara na zile za Daraja la Kwanza Bara. Timu zinamwaga fedha na waamuzi wanapokea.

Uchunguzi wa wiki tatu wa gazeti hili umegundua waamuzi wamebandikwa jina la kunguru, wakifananishwa na ndege aina ya kunguru kutokana na rangi za nguo zao kuwa nyeusi na wenyewe mara nyingi kuvaa mavazi ya aina hiyo.

Viongozi wa timu kadhaa za soka wakati wakifanya majadiliano yao kutaka kupata uhakika wa ushindi kwa kuwahonga waamuzi, wanawaita kwa jina hilo la kunguru.
“Kunguru amesema anahitaji kiasi gani,” anauliza kiongozi wa kwanza.

“Usisahau ni kunguru wanne, isiwe chini ya milioni tano maana itapitia kwa mmoja wa viongozi wao, lazima naye alambe kidogo,” anajibu kiongozi mwingine.

Kwa viongozi wa timu za Ligi Kuu Bara ni lahisi sana kukataa kwa kuwa wanajua ni siri kubwa kwa kuwa kutoa na kupokea rushwa ni kosa kubwa kisheria.

Uchunguzi huu umepita kwa baadhi ya viongozi wa klabu, waamuzi na viongozi wa waamuzi na wako ambao wamekiri kuwa rushwa katika soka ipo na imekuwa ikizidi kupanda kwa kasi.

“Kweli rushwa inatolewa, timu yetu imekuwa ikitoa rushwa, tunaweka bajeti kabisa na wakati mwingine hadi shilingi milioni tano kwa mechi moja tu. Unajua unalazimika kutoa kwa waamuzi wote,” alisema kiongozi mmoja wa timu maarufu.

Lazima:
Nani anaweza kubisha tena kwamba hakuna rushwa, timu ipi inaweza kupinga kuwa haijawahi kutoa rushwa? Jibu hakuna, tatizo kila mmoja anajificha kwenye mwamvuli wa “umetuona wapi” au ule “thibitisha sasa”.

“Hauwezi kuacha kutoa, wengine pia wanatoa rushwa. Ukiacha wewe ujue imekula kwako, sasa sisi tufanyeje?” anaongeza kiongozi wa klabu moja kubwa.

“Angalia unacheza na timu kama (anaitaja), una uhakika unaweza kuifunga. Lakini kwa kuwa mwamuzi hamjampa hata senti, basi anachezesha kwa kuwaharibia makusudi, hivyo lazima kila mechi mumpoze mwamuzi hata kama mnajua mna uwezo wa kushinda,” anasisitiza kiongozi huyo.

Madalali:
Championi limegundua mfumo wa rushwa unaundwa na madalali. Yaani watu wa kati ambao wamekuwa na kazi ya kufikisha fedha hizo za rushwa.
Kuna aina mbili za madalali, kwanza ni wale kutoka katika klabu na pili wale wanaokuwa upande wa waamuzi.

“Kweli, mara nyingi tumekuwa wakija wale makomandoo wa timu zao au baadhi ya watu maalum na wanajulikana. Hao watu pia ukikataa kuchukua fedha wamekuwa wakisingizia umechukua na wakati mwingine hawafikishi zote,” anasema mmoja wa waamuzi aliyechezesha Ligi Kuu Bara kwa miaka mitatu mfululizo kabla ya kustaafu.

Lakini taarifa za baadhi ya viongozi wa waamuzi kuwa madalali pia inatia hofu kubwa ya kuwa rushwa haitaisha kwenye soka.

Juhudi zikafanyika kumpata Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Tanzania (Frat), Nassor Mwalimu ambaye anasema tena kwa msisitizo kweli rushwa ipo, waamuzi huchukua na viongozi wa soka hutoa. Kwa nini?

“Hilo suala tunalijua, ndiyo maana tunapambana na kuweka mikakati. Mfano hivi karibuni tulikuwa na semina ya waamuzi ambayo iliendeshwa na watu wa Takukuru, hii ni sehemu ya kuonyesha tunalitambua hili jambo na tunalifanyia kazi.

“Angalia hawa waamuzi wanaolipwa hadi shilingi laki nne kwa mechi, tena inaanzia laki na hamsini. Mechi inaingiza mamilioni na timu zinagawana lundo la fedha.
“Siungi mkono waamuzi kuchukua rushwa, nataka maslahi yao yaboreshwe ili itusaidia na sisi kupambana na jambo hili. Kila siku tunawawinda waamuzi wanaochukua rushwa, lakini kazi kuwapata.

“Kuna mtandao unaofanya kazi hii na unajua jinsi ya kucheza mchezo wao. Utaona kila mara tunasimamisha waamuzi au kuwaondoa kabisa. Bado nasema kutoa na kupokea rushwa ni kosa, tunajua. Lakini sisi tunawaadhibu wapokeaji na hakuna anayeshughulika na watoaji. Vipi hao viongozi wa klabu?” anahoji Mwalimu ambaye ni mwalimu kitaaluma.

“Kuhusu viongozi wa waamuzi kupokea rushwa kwa ajili ya waamuzi silijui, lakini inawezekana maana sisi ni binadamu. Lakini niliwahi kupata mkasa wa huyo mtu wa kati ambaye alipewa fedha na klabu yake, akasema amempa mwamuzi, kumbe hakufikisha.

“Timu ilipofungwa, viongozi wakamvaa mwamuzi, akasema yeye hajawahi kupewa na huwa hachukui rushwa. Wakambeba yule middle man wakaenda kwa mwamuzi, akashindwa kuthibitisha wakaondoka naye na kusema watamalizana naye.

“Wako waamuzi wamewahi kukataa rushwa, hili nina ushahidi. Lakini walipochezesha halafu ile timu iliyotaka kuwahonga ikafungwa, viongozi na wachezaji wakataka kuwapiga. Eti ile timu nyingine itakuwa iliwapa fedha nyingi!
“Kazi ya waamuzi ni ngumu, lazima ipewe hadhi yake na maslahi mazuri yatapunguza wao kutetereka na kuingiwa kwenye ushawishi.
“Ila nasisitiza, timu zikiona zimeshindwa, zisiwageuze waamuzi mbuzi wa kafara na kuwapiga tu kwa kisingizio wamehongwa. Wakati mwingine hata mashabiki wanajua sheria kuliko waamuzi, ukiwaambia wataje hata moja, hawaijui, ajabu kabisa!” anahitimisha Mwalimu.

Kwa maelezo ya Mwalimu, viongozi na waamuzi waliohojiwa, mchezo mchafu wa rushwa unaendelea kupitia kunguru wachafu.


Juhudi za kupambana na rushwa katika soka lazima zitiliwe mkazo ingawa ni jambo litakalowaudhi wengi wanaofaidika lakini uchunguzi huu mdogo umegundua mtandao mkubwa ndani ya waamuzi, viongozi na klabu zote za Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic