January 30, 2015


Na Saleh Ally
KOCHA wa zamani wa Yanga, Ernie Brandts huenda ndiye aliyeongoza kwa kulalamika kwamba anashindwa kutoa kila alichokuwa nacho kiuwezo kwa kikosi chake kutokana na ubovu wa kupindukia wa miundombinu.


Brandts raia wa Uholanzi, haikuwa mara yake ya kwanza kufundisha soka Afrika. Alifanya kazi nchini Rwanda kwa zaidi ya misimu mitatu, tena kwa mafanikio makubwa.

Beki huyo wa zamani, alidai Yanga ilishindwa hata kumnunulia magoli madogo kwa ajili ya kupambana na zoezi la ubutu wa utumiaji nafasi, viongozi walimuahidi kila siku jua lilipochomoza, wakampotea jua lilipochwea.

Miaka saba iliyopita, Kocha Nielson Elias raia wa Brazil, aliamua kuondoka Simba baada ya kugundua timu haikuwa hata na uwanja wa mazoezi na kusema anaamini timu hiyo haitafika popote hadi itakapopata uwanja.

Karibu kila kocha kutoka nje ya Tanzania amelalama kuhusiana na uwanja kwa kuwa Yanga na Simba zenye tofauti ya mwaka mmoja tu kiumri, moja ikiwa na miaka 80 na nyingine 79, bado hazijui zinachokifanya.

Bara:
Wako wanaoshangaa Mtibwa Sugar, Azam FC kuonyesha soka bora kuliko Yanga au Simba. Wanasahau timu hizo ziko ‘busy’ na soka kwelikweli.

Azam FC au Mtibwa Sugar zinamiliki viwanja vyake zinavyovitumia kwenye ligi pia. Haziwezi kupangiwa mazoezi kama ilivyo kwa Yanga au Simba zinazotangatanga na wakati mwingine kufanyia mazoezi kwenye viwanja vibovu kama Tanganyika Packers, Bora Kijitonyama au Loyola Sekondari.

Timu hizo kongwe ziko busy na viwanja vya shule, vya timu za daraja la tatu au vinavyomilikiwa na timu za veterani. Jamani, hadi veterani wana uwanja wao wa mazoezi, Yanga na Simba hawana!

Timu nyingi za mikoani zina viwanja bora vya mazoezi. Hata kama utasema zitacheza ligi kwenye viwanja vingine visivyokuwa na ubora lakini ukweli zitakuwa zimefanya mazoezi bora kwa wakati wa kutosha na zinakuwa tayari kukabiliana na lolote kwa stamina na pumzi, ndiyo maana zinaweza kupambana mwanzo mpaka mwisho tofauti na Simba na Yanga.

Usilalamike Yanga au Simba kutokuwa na stamina. Mazoezi ya gym nayo ni ya kuibia kwa kuwa lazima zilipie kwenda, kweli kwa miaka yote zimeshindwa kuwa hata na chumba cha gym na vifaa vyake!

Hivi viongozi wa klabu hizo hawaoni au wanafumba macho kwa kuwa wanajua wanafanya siasa na si masuala ya mpira?

Wachezaji wa Yanga na Simba wana nafasi ya kuwa na majina makubwa lakini wasiwe na soka kubwa.

Azam FC imepambana ndani ya miaka minne imebeba ubingwa wa Tanzania tena kabla ya hapo ikiwa imeshika nafasi ya pili mara mbili mfululizo.

Inawezekana kuna wakati Azam FC wanakosea, lakini lazima tukubali hatua wanazopiga kwa vitendo, baadaye watakuwa imara kuliko timu nyingine halafu tutawasingizia mengine wakati ukweli tunaona sasa.

Afrika:
Simba na Yanga ni timu zenye ndoto ya kufanya vema katika michuano ya Afrika, hasa ile iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Jiulize, kwa timu yenye miaka 80 au 79, halafu haina hata uwanja wa Mazoezi inawezekana vipi? Nani anaamini Yanga na Simba zinaweza kucheza soka bora kushindana na timu kama Enyimba ya Nigeria, TP Mazembe au AS Vita ya DR Congo huku zikiwa hazina hata uwanja wa mazoezi!

Timu hizo mbili za Tanzania si timu zenye ndoto ya kufanya vema. Mtu anayetaka kutimiza ndoto zake ni yule anayepiga hatua baada ya hatua akienda anakotaka kufanikiwa.

Kushindwa leo, ukijipanga upya na kupambana tena hadi ukafanikiwa ndiyo sehemu ya ubora. Hauwezi kusema timu isiyo hata na uwanja wa mazoezi ina ndoto za kuwa bingwa wa Afrika, kitakuwa kichekesho cha karne.

Yanga na Simba ni roli aina ya Scania lenye injini ya Volkswagen Beatle maarufu kama mgongo wa chura.

Scania yenye injini ya mgongo wa chura, ikiwa na mzigo mkubwa halafu inataka kupanda mlima, jiulize mara mbili, nini kitafuatia?

Hadithi za Yanga na Simba hata kuwa na uwanja wa mazoezi tu, umezisikia tokea lini? Hata mimi hii si mara yangu ya kwanza kuandika, hawa watu ni wa aina gani hadi hawaelewi!

Hili suala la kusisitiza Yanga na Simba wanapaswa kuwa na uwanja, kweli wao hawajui! Huo ni wajibu wao na wanajua umuhimu wake.

Leo Yanga na Simba wanasema wanakuza vijana, eti wana timu B. Wakati mwingine ni kichekesho tu kulazimisha kukuza watoto wanaotumia viwanja vyenye mabonde, vikavu.

Kweli watakuaa, wachache wasiokata tamaa wataonekana lakini kuna mengi wanakosa kama suala la vifaa na hasa viwanja lingepewa kipaumbele na wao kukua kwenye misingi sahihi.

Usisahau kuwa afya za wachezaji kwa maana ya magoti, enka, nyama za paja na vinginevyo haziko salama.

Ukitaka kunielewa zaidi baada ya mazoezi, angalia viatu vya Haruna Niyonzima wa Yanga na Jonas Mkude wa Simba, fananisha na cha Didier Kavumbagu wa Azam FC au Ame Ali wa Mtibwa Sugar.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic