January 23, 2015

MICHAEL AKIMKABA TAMBWE KATIKA MECHI YA LIGI KUU BARA...
PICHA ya ukurasa wa mbele wa gazeti namba moja la michezo nchini, Championi ilionyesha beki George Michael wa Ruvu Shooting akimkaba mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga.


Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ilimalizika kwa sare ya bila mabao huku Yanga ikishindwa kuendeleza ubabe dhidi ya timu hiyo ya jeshi ambayo msimu uliopita ilikubali kipigo cha mabao saba.

Ingawa mashabiki wa Yanga walionyesha wazi kukerwa na sare hiyo, lakini kabali ya Michael ‘iliyogunduliwa’ na Championi ndiyo ilikuwa gumzo zaidi na kufanya hali ya hewa ibadilike kabisa.

Wapenda mpira waungwana, waliungana bila ya kujadili ushabiki wa Yanga na Simba au timu nyingine na kukemea kitendo kile cha kikatili ambacho muungwana yeyote, kamwe hawezi kuungana nacho.

Viko vyombo vya habari navyo vilisimama kidete kukikemea kitendo hicho, vingine vikashindwa kusimama na kuonyesha hakikuwa sahihi kwa hofu ya kushindwa au kuonekana havikuwa vya kwanza kukiibua kitendo hicho na kukizungumzia zaidi, huenda Championi litapata sifa nyingi sana!

Ukweli unabaki palepale, picha hiyo ilichapishwa kwenye Gazeti la Championi na ndiyo iliyozua gumzo. Haitabadilika na jambo la msingi si kuangalia nani atapata sifa kubwa sana, badala yake tusaidie vipi matendo ya kikatili kama hayo kutofanyika.

Ninachoshangazwa, wako wanaotetea na hasa baadhi ya viongozi wa Ruvu Shooting. Wanaingiza mzaha au utani katika jambo linalotaka kudhibitisha kuwa mchezo wa soka si wa kiungwana.

Wako wanaotaka kulikwepesha jambo hilo lionekane kama linakuzwa au ni la kawaida sana. Huenda wanasahau kuwa kwa kiwango cha Ligi Kuu Bara, basi huenda lililotokea ni kiwango cha soka la mchangani.

Wako wanaotaka Michael achukuliwe hatua kali. Mimi naungana nao, lakini napendekeza achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na kusiwe na jazba katika utekelezaji wake.

Ninashauri kwa kuwa nimeelezwa Michael ni askari, kuna kila sababu ya afande huyo kujitokeza na kulizungumzia suala hilo hadharani kama ambavyo Tambwe alizungumza na waandishi wa habari, juzi.

Afande Michael ajitokeze, azungumze kwa kuwa sisi wote ni binadamu na tunakosea. Kila anayekosea pia ana nafasi ya kurekebisha makosa yake hasa kama atakuwa ameanza kwa kuyakubali makosa aliyotenda. Kama haukubali ulipojikwaa, basi kujikwaa yatakuwa ndiyo maisha yako milele.

Michael ajitokeze na kueleza ilivyokuwa. Kama anaamini amekosea basi aombe radhi na kama inawezekana hata kama atapewa adhabu basi wako wanaopaswa kumsamehe.

Sidhani kama kila mmoja atamuadhibu kwa kuwa waliokasirishwa ni wengi. Kama ataonyesha uungwana wa kujutia kosa, wadau wengi watamsamehe wakiamini naye ni binadamu kama wao ndiyo maana amekubali kuhusiana na kosa.

Pamoja hivyo, bado ninaweza kuweka msisitizo kuhusiana na suala la kuangaliwa kuhusiana na uchezeshaji wa waamuzi na ukuzaji wa viwango vyao.

Bado tunahitaji waamuzi imara ambao wanaweza kufanya kazi yao kwa ufasaha kuliko kuwa ni wenye hofu ya lawama.

Anayeogopa lawama, kamwe hawezi kuifanya kazi yake kwa ufasaha na kiwango cha juu. Naamini mwamuzi Mohamed Teofili wa Morogoro au wasaidizi wake walikuwa wamejawa hofu muda mwingi na huenda kuna matukio waliyashuhudia lakini wakashindwa kuchukua hatua kutokana na uoga.

Niikumbushe TFF kuwa, waamuzi ambao wamepigwa kwenye michuano ya Ligi Daraja la Kwanza, wangependa kuona shirikisho hilo linawachukulia hatua wahusika, tena mara moja.

Wakifanya hivyo, watasaidia kuwaondolea waamuzi hao woga na pia kuwapa woga wale wenye tabia ya kupiga waamuzi kwamba wakifanya upuuzi huo, haraka sheria itachukua mkono wake. Picha za mchezaji anamkimbiza mwamuzi na wengine wakimpiga zipo na zinaweza kufanyiwa kazi ili kulisafisha soka hapa nyumbani, ukweli sasa limechafuka!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic