February 28, 2015

HII ILIKUWA NI GAME YA MWISHO ANFIELD, MSIMU ULIOPITA, LIVERPOOL IKIWA NA SUAREZ. MECHI YA KESHO CITY WANAKWENDA TENA ANFIELD WAKIWA WANAUTAKA UBINGWA TENA.

Manchester City wanashuka dimbani kesho kuwavaa Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu ya England wakijua ndiyo kombe pekee wanaloliwania pia wanalopaswa kulitetea.


Hawamo Capital One, FA na Ligi ya Mabingwa mwendo wao hauna uhakika. Sasa wataifunga Liverpool kesho ambayo katika mechi tano walizokutana nayo wameifunga mara 2, imewafunga mara moja na sare 2?

Liverpool ina majeraha ya kung'olewa kwenye Kombe la Europa, itakubali kilahisi tena ikiwa nyumbani?

City walifungwa mabao 2-1 na Barcelona kwenye hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki hii, wameshatolewa kwenye Kombe la FA pamoja na Capital One hali ambayo itawafanya wafanye kazi ya ziada ili waweze kumaliza msimu na kombe.


Watatakiwa kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili waweze kupunguza gepu kati yao na vinara Chelsea na kubakiza pointi mbili, kwani sasa wanadaiwa pointi tano wakiwa nafasi ya pili.

Pamoja na kwamba wana kikosi cha bei ghali, City walimaliza michezo minne bila kupata ushindi hivi karibuni ambapo kiungo wao mahiri, Yaya Toure, alikuwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Lakini kitendo chao cha kuanza kupata ushindi dhidi ya Stoke City na Newcastle United, kimewafanya kuanza kurejea kwenye kasi yao.

Hali hii inawafanya waaminike kuwa, wanaweza kufanya maajabu kesho na kuifanya Chelsea ya Mourinho kuanza kuweweseka.

Lakini kazi haitakuwa ndogo wakati unapocheza na timu ngumu kama Liverpool ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kati ya 10 ya hivi karibuni kwenye Ligi Kuu ya England.

Mchezo wa kesho unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki kwenye Uwanja wa Anfield kutokana na kiwango cha timu yao cha hivi karibuni.

Kwa mara ya kwanza, Liverpool walipoteza dhidi ya Manchester United, Desemba 14, mwaka jana ilipokula kichapo cha mabao 3-0 na kusogea hadi katikati ya msimamo wa ligi hiyo.

Mashabiki wanaamini kuwa ushindi wa hapa utawafanya Liverpool kuwa na matumaini makubwa ya kumaliza msimu huu wakiwa katika nafasi nne za juu.

Liverpool ambao kwa sasa wapo nafasi ya sita, wamefanikiwa kushinda michezo miwili migumu ya hivi karibuni dhidi ya Southampton walipopata ushindi wa mabao 2-0, lakini pia wakiwa wamewachapa Spurs mabao 3-2 na sasa wapo pointi tatu tu nyuma ya Arsenal waliopo nafasi ya tatu.

Mastaa wa Liverpool, Philippe Coutinho, Raheem Sterling na Daniel Sturridge, wamekuwa kwenye kiwango cha hali ya juu sana kwa kipindi cha hivi karibuni, jambo ambalo ni hatari sana kwa City.

Lakini bado kila mmoja anafahamu kuwa City ni timu hatari ikiwa na wanaume kama Yaya, Sergio Aguero na David Silva ambao wamekuwa wakifanya maajabu sana msimu huu.

Mwamuzi:
Mwamuzi wa mchezo huu ni Mark Clattenburg, mwamuzi huyu amekuwa na majanga ya hapa na pale, lakini akiwa bora sana wa kutoa kadi nyekundu uwanjani.

Ni mmoja kati ya waamuzi bora kwenye Ligi Kuu England lakini karibu kila msimu amekuwa akikumbana na majanga, mwanzoni mwa msimu huu alisimamishwa baada ya kupanda gari binafsi wakati akitoka kwenye mchezo kati ya West Brom dhidi ya Crystal Palace ili kuwahi kwenye pati jijini Newcastle.

Uso kwa uso:
Man City             3 - 1        Liverpool         
Liverpool            3 - 2         Man City         
Man City              2 - 1        Liverpool          
Man City              2 - 2        Liverpool         
Liverpool             2 - 2        Man City


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic