March 6, 2015


Na Saleh Ally
SIMBA itakuwa na kazi ngumu kuhakikisha inalipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wao, Yanga.


Simba inakutana na Yanga katika mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2014-15 baada ya mechi ya kwanza ya msimu huu kumalizika kwa suluhu.

Kikosi cha Simba chenye wachezaji kadhaa wenye uwezo wa kubadili matokeo kupitia uwezo wao binafsi, kitakuwa na kazi ngumu ya kufanya mabadiliko ya kuhakikisha kinapata ushindi.

Tofauti na hali ambayo imekuwa ikionekana kama Simba imekuwa ikiionea Yanga, takwimu zinaonyesha Yanga ndiyo imefanya vizuri zaidi ya Simba katika mechi tano zilizopita.

Hapa tunazungumzia mechi za Ligi Kuu Bara na si zile za Kombe la Nani Mtani Jembe ambalo Simba ndiyo wababe zaidi ya watani wao Yanga.

Katika Nani Mtani Jembe, Yanga na Simba zimeshakutana mara mbili na mara zote Yanga wamekiona cha moto kwa kuchapwa mara mbili.


Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Desemba 21, 2013, Yanga walikutana na kipigo cha mabao 3-1 na Simba kubeba ubingwa. Mechi ya pili, Desemba 13, 2014, Simba wakaendeleza ubabe kwa kushinda mabao 2-0.

Ukiachana na mechi hizo za Nani Mtani Jembe, ukirejea kwenye Ligi Kuu Bara, Simba haijashinda hata mara moja katika michezo mitano iliyopita.

Mchezo wa sita kabla, ni ule ambao Simba ilitoa adhabu ya kipondo cha mabao 5-0 kwa watani wao hao ikiwa ni mechi ya kufunga msimu wa 2011-12 iliyopigwa Mei 6, 2012.

Kwa hesabu nzuri, unaweza kusema Simba haijaifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu hadi sasa.


Kwani kuanzia msimu wa 2012-13, katika mechi mbili za ligi hiyo, mechi ya kwanza timu hizo zilikutana Oktoba 3, 2012 na zikatoka sare ya bao 1-1, Simba ikianza kupata bao la mapema kupitia kwa Amri Kiemba katika dakika 4, lakini Said Bahanuzi akaisawazishia Yanga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 65.

Watani wakafunga msimu kwa Yanga kuifunga Simba katika mechi ya pili kwa mabao 2-0 mnamo Mei 18, 2013, wafungaji wakiwa ni Hamis Kiiza na Dider Kavumbagu.

Yanga wakaondoka msimu huo wakiwa wababe na msimu uliofuata ni 2013-14. Mechi ya kwanza Oktoba 20, 2013, ngoma ikalala 3-3. Kama unakumbuka Yanga waliongoza 3-0 hadi mapumziko, wengi wakajua Mnyama ‘anakula’ 5, Simba ‘wakachomoa’ zote!

Mechi ya pili ya kufunga msimu, ikapigwa Aprili 19, 2014 na Simba wakaanza kufunga katika dakika ya 75 kupitia kwa Haruna Chanongo, Yanga kupitia kwa Simon Msuva wakasawazisha katika dakika ya 86.

Msimu wa tatu ni huu wa 2014-15 ambao timu hizo zilikutana mapema zaidi, ilikuwa Oktoba 18, 2014 baada ya kila timu kuwa imecheza mechi tatu na zikamaliza kwa suluhu.


Mechi ya keshokutwa ni ya sita inayokamilisha misimu mitatu kamili kwa kuwa kila msimu, timu hizo zinakutana mara mbili.

Takwimu zinaonyesha hivi, katika mechi tano za misimu mitatu zilizokutana timu hizo, Yanga imeshinda mara moja na sare nne.

Simba ina kazi hiyo ya kulipa kisasi cha ubabe wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa Yanga angalau wanaongoza kwa kuwa na ushindi mmoja uliowapa pointi tatu.

Ndani ya misimu mitatu, Simba haijawahi kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara, huenda keshokutwa wanaweza kubadilisha mambo.

MECHI 5 ZILIZOPITA ZA MISIMU MITATU:
Yanga 1-1 Simba 
Simba 0-2 Yanga
Simba  3-3 Yanga
Yanga 1-1 Simba 
Yanga 0-0 Simba 

MABAO YA KUFUNGA:
Simba 5
Yanga 7

MECHI 5:
Yanga (Shinda 1, Sare 4, Poteza 0)
Simba (Shinda 0, Sare 4, Poteza 1)

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic