Na Saleh Ally
RAIS wa Baraza la Vyama vya
Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Leodegar Tenga na Rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, wameweka msimamo wao wazi
kuhusiana na uchaguzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Kwa pamoja, Tenga na
Malinzi wamesema Tanzania yenyewe iko wazi mapema na hakuna sababu ya kupoteza
muda kwamba katika uchaguzi ufuatao, itampigia kura Josep Blatter.
Blatter ndiye rais wa Fifa
sasa, amekaa madarakani tangu mwaka 1998, maana yake ana miaka 17 akiliongoza
shirikisho hilo kubwa, maarufu na tajiri kwelikweli.
Uamuzi wa Tenga na Malinzi
kutangaza hadharani umekuja huku viongozi hao wakisisitiza ni kutokana na namna
ambavyo Blatter amekuwa akisimamia maslahi ya Bara la Afrika katika mchezo wa
soka.
Alichokisema Malinzi,
hakina tofauti kabisa na Tenga. Maana yake wawili hawa wanaungana pamoja katika
njia moja, kuzungumza vitu vinavyofanana na wanavyoviamini.
Sina tatizo na uamuzi wa
Tenga na Malinzi kuhusiana na Blatter. Lakini nashangazwa kwa kuwa naona kama
uamuzi huo umekuwa ni wa haraka sana na unaonekana kama una ushabiki au maslahi
binafsi.
Tenga ni kati ya walio
katika kamati za Fifa. Inawezekana mapenzi yake au ameamua kumtetea bosi wake
na yeye ameamua kushuka hadi kwa Malinzi na kumshawishi kuhusiana na Blatter,
naye amekubali.
Au inawezekana Malinzi naye
ameamua kufanya hivyo kutokana na misaada ya chinichini, waziwazi au vinginevyo
ambayo anaipata kwa Blatter akiwa na shirikisho?
Napata maswali mengi sana
kwa kuwa Malinzi na Tenga hawakuweka wazi kipi hasa ambacho Blatter ameisaidia
Tanzania na si Afrika.
Sidhani kama Watanzania
wanataka kusikia zaidi kuhusu Afrika badala ya Tanzania ambayo ni nchi yao na
wanajua Fifa ina uwezo mkubwa sana wa kifedha.
Malinzi na Tenga wanaamini
kiasi cha fedha kinacholetwa na Fifa kama msaada kinatosha kweli? Hawaoni kama
Fifa inastahili kuisaidia Tanzania zaidi?
Lakini wakati wanakubali
kumpigia kura Blatter, wamewahi kumsikiliza Luis Figo ambaye ni mgombea mwenza
wa Blatter kwamba yeye ataisaidiaje Tanzania au Afrika?
Sasa vipi wamewahi kukubali
kumtetea au kumpigia kura Blatter wakati hawajajua lolote kuhusu Figo. Kama
walijua mbona hawajawaambia Watanzania kwamba Figo hatakuwa na msaada mkubwa?
Kweli Tenga na Malinzi wote
wanaweza kuwa na haki ya kuchagua wampigie nani. Lakini kwa Malinzi anapaswa
kujua yeye ni mwakilishi wa Watanzania ambao wamemchagua.
Nafasi aliyonayo ni
uwakilishi wake kwa Watanzania kwenda Fifa. Hivyo kabla ya kuchukua uamuzi
fulani au jambo fulani, basi wana kila sababu ya kuwafafanulia kwa undani
Watanzania wajue.
Bado sijawa na uhakika
uamuzi waliouchukua ni sahihi au la kwa kuwa sijasikia sababu zao ni msingi au
la. Hii inatokana na kutokuwa na maelezo ya kutosha kutokana na umuhimu
ninaouzungumzia.
Lazima Malinzi akubali, TFF
ni ya umma. Hivyo kuwafafanulia Watanzania kuhusiana na uamuzi unaowahusu ni
jambo jema ili kuondoa hisia za huenda kuna wachache wanaofaidika kwa kuwa
inajulikana, licha wa ukubwa wa Fifa, wakati mwingine imekuwa ikichafuka sana
hasa katika kipindi cha masuala ya uchaguzi.
Kila mtu anajua kuwa Blatter ni mtu wa rushwa!! Amekuwa raisi wa FIFA kiipindi chote cha Tenga na kuna pesa nyingi za miradi zilikuwa zinakuja zinaliwa na wajanja na mwisho wa siku wanakuja watu toka fifa kuwasafisha. Hata kipindi cha Malinzi anajua pesa nyingi za miradi na mapato wanazitumia sivyo ndivyo na hakuna mtu wa kuhoji zaidi ya Fifa. Zimwi likujualo...., wanjua wanamhitaji Blatter ili waendelee kula good time, na haya ni maelekezo ya Issa Hayatou!! Hawana maelezo ya kukupa zaidi ya kwamba ni maelekezo na wanachotakiwa ni kutimiza. Vicha vya panzi, hakuna siku vitakuja kuvaa kilemba
ReplyDelete