May 23, 2015

RAIS WA SIMBA, EVANS AVEVA AKITOA HUTUBA, HUKU MAKAMU WAKE, GEOFREY NYANGE 'KABURU' AKIWAZA JAMBO FULANI...

Na Saleh Ally
KLABU ya Simba imeanza usajili kwa ajili ya msimu ujao, ikiwa imepania kufanya mabadiliko makubwa na lengo kubwa ni kukiweka kikosi chake katika hali itakayorejesha makali ya Simba.


Simba haijashiriki michuano ya kimataifa kwa misimu mitatu sasa na inaonekana kama watalala, basi itakula kwao kwa msimu mwingine.

Mambo yalivyo kwa uhakika, si mazuri. Juhudi za kuhakikisha kikosi kinakuwa bora zinahitaji mambo mengi sana lakini muda na fedha, vyote havikwepeki.
Bado kuna utulivu, ushirikiano na kuaminiana. Lengo la yote ni kutimiza mambo muhimu yanayotakiwa kwa ajili ya kuiimarisha Simba.
 
HANS POPPE AKIWA NA TALIB HILAL, MMOJA WA MAKOCHA WA ZAMANI WA SIMBA, PIA WALIOWAHI KUICHEZEA TIMU HIYO KWA MAFANIKIO.
Jana nilizungumza kuhusiana na Kamati ya Usajili ya Simba kupewa nafasi ya kufanya kazi yake na si kila mjumbe wa kamati ya utendaji kuwa fundi na kutaka kufanya usajili, ili mradi anajuana na wachezaji au makocha.

Wakati juhudi za kufanya mabadiliko zinaendelea, kuna kila haja ya uongozi wa Simba na kamati yake ya utendaji kwanza kukubali kwamba wana matatizo ambayo pia ni sehemu ya kuyumba kwao.
MJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI YA SIMBA, KASSIM DEWJI AKITETA JAMBO NA KOCHA PATRICK PHIRI ALIYETIMULIWA KWA KIWANGO KIBOVU CHA TIMU. LAKINI SUALA LA KIONGOZI KUTOA DAWA ZILIZOWAPUNGUZA NGUVU WACHEZAJI HALIKUWEKWA HADHARANI!
Kwamba ili wabadilike, ni lazima wayakubali na kuyafanyia kazi. La sivyo watafanya kila kitu halafu mwisho itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu, maana hawatafanikiwa na wataonekana kuwa wanaidanganya jamii ya Wanasimba.

Ndani ya uongozi wa Simba, ukianzia viongozi hadi wajumbe wa kamati ya utendaji, kuna ubinafsi. Wapo viongozi ambao wamekuwa wakitaka kuonekana au kujulikana zaidi ya wenzao.

Hawataki wengine wajulikane. Wapo wengine wanafanya kazi sana, hata kuonekana kwao kunalingana na wanachokifanya, lakini wapo wasiofanya lolote, wasingependa kuona wenzao hata kama wanafanya kazi sana wanaonekana!
 
MUSLEY, MMOJA WA WAJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI PIA KAMATI YA USAJILI YA SIMBA.
 Mfano ambao nafikiri unaweza kuwa chanzo cha mimi kuamua kuwaeleza Simba kuhusiana na kukubali kupitia makosa yao ni lile sakata la kupatikana kwa mtu aliyeaminika alikuwa akiwapa vitu wachezaji ambavyo vilionekana kuwaathiri.

Simba wamelificha sana hili, sijui kwa nini wameamua kulifanya siri wakati ilibainika kiongozi wa kuchaguliwa tena wa ngazi za juu, alibainika kuwapa wachezaji dawa ambazo ziliwapunguza nguvu, wakashindwa kucheza kwa kasi waliyonayo kwa muda wote.
TULLY, MJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI NA KAMATI YA USAJILI YA SIMBA AKIZUNGUMZA NA KOCHA WA ORANDO PIRATES WAKATI SIMBA ILIPOWEKA KAMBI NCHINI AFRIKA KUSINI.

Wao Simba wanajua hilo ndiyo tatizo la wao kutoka sare nyingi kwa kuwa kila timu ilipofunga, kipindi cha pili ilidorora na kuachia nafasi ya kusawazishiwa na baadaye kufungwa.


Uchunguzi wa viongozi wa Simba ulifanyika, wakabaini hilo, wakamuweka chini daktari naye akakiri kwamba alikuwa akipewa vitu na kiongozi fulani na kweli hata mpishi alikiri kuhusiana na hilo!



Sijui sababu za wao kuamua kukaa kimya na kulificha hilo? Lakini taarifa zinaeleza kuwa walimuweka kiongozi huyo kiti moto, naye akaomba radhi akitoa utetezi usiokuwa na mashiko.



Kwangu kiongozi wa namna hiyo ni hatari kabisa kwa Simba, kwangu bado siamini kama kweli anaipenda klabu hiyo na sitakuwa tayari kumsikiliza hata siku moja akisema ana mapenzi na klabu hiyo.

Huyo ana mapenzi na yeye mwenyewe na ndiyo mfano sahihi wa ubinafsi ninaouzungumzia ambao Simba wakati wanaanza usajili wa msimu huu lazima waukomeshe kwanza.

Nimekuwa nikijiuliza, hata kama kweli kiongozi huyo amesamehewa wakati alidiriki kuihujumu timu anayoipenda na kuiongoza, sasa anaendelea kuwa ndani ya kikosi, kweli ataacha tabia hiyo au ataendelea kupanga mipango mingine ya kuiangusha?

Uongozi wa juu kwa kushirikiana na kamati ya utendaji, wanapaswa kuwa makini kwa kuwa adui wa ndani ni hatari maradufu kuliko adui wa nje.
Mmekubali kumbakiza ndani, huenda kwa undugu, urafiki wenu au uungwana wenu tu, lakini mimi nasisitiza, lazima muwe makini maradufu, mkubali makosa yenu ili muweze kufanya vizuri zaidi.

Kwa wewe uliyekamatwa na shutuma hii mbaya kabisa, kama kweli ulifanya basi jirekebishe na ubadilike kweli, pia bahati yako sijakujua jina.



1 COMMENTS:

  1. Kaka unazungumzia kitu unachokijua au unazungumzia habari za kijiweni na majungu!!? Sasahivi si wakati wa kuanza kuchafuana!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic