Majambazi Yameiba
gari la kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, aina ya Toyota Carina SI lenye
namba za usajili T 224 CXR.
Akizungumza
na Championi Jumatano, Barthez alisema kuwa gari hilo liliibiwa usiku wa
kuamkia Ijumaa iliyopita wakati yeye akiwa safarini akielekea Tunisia kwa ajili
ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel
uliomalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.
Barthez
alisema kuwa, gari hilo liliibiwa kwenye maegesho ya magari eneo la Majumba
Sita, Ukonga jijini Dar es Salaam.
Akisimulia mkasa huo kwa masikitiko
makubwa, Barthez alisema aliliacha gari hilo mikononi mwa mdogo wake hadi
linakumbana na mkasa huo.
“Ninaishi
Kitunda nilipojenga nyumba ninayoishi na familia yangu, mara nyingi
ninaposafiri ninamuachia mdogo wangu Aziz Mustapha anayeishi Majumba Sita kwa
ajili ya kulilinda.
“Kwa sababu
kule kwangu ninapoishi vibaka wapo wengi na mara nyingi wamekuwa wakiruka ukuta
na kuiba baadhi ya vitu vilivyopo kwenye gari. Wakati narejea nchini nikiwa
kwenye Uwanja wa Ndege, ndiyo nikampigia simu mdogo wangu na kunipa taarifa za
kuibiwa gari hilo. “Hivyo nikatumia usafiri mwingine kwenda Majumba Sita walipo
wazazi wangu ndiyo wakanipa taarifa hizo kuwa gari liliibiwa usiku wa kuamkia
Ijumaa iliyopita.
“Nilipohoji
vipi mlinzi alikuwa wapi, mdogo wangu akanijibu kuwa alipokwenda asubuhi
alikuta gari na mlinzi wote hawapo na ndiyo akaenda kuripoti kituo cha polisi,
wakati anafika hapo akakutana na watu wengine watatu waliofika kuripoti kuibiwa
gari kwenye maegesho hayo ya gari.
“Polisi
wanaendelea na upelelezi kwa ajili ya kuchunguza wizi huo wa magari manne
yaliyoibiwa,” alisema Barthez.
Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva anayemiliki
gari aina ya Altezza, naye alitoa masikitiko yake. “Kwa kweli nimesikitika
sana, nimempa pole Barthez kutokana na tukio hilo baya. Mimi mwenyewe kila
nikisafiri nimekuwa namuachia mzee gari anakuwa nalo maana pale nyumbani kuna
watu wengi na ulinzi upo.
“Nachofanya
ni kujaza mafuta ya kutosha na mzee anaendelea na misele yake. Siku nikirudi
nalichukua,” alisema Msuva.
Kwa upande wa
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema: “Kweli inauma sana, kwa
kweli wamefanya kitu kibaya sana.
“Mimi
nimekuwa makini sana, mara nyingi nikisafiri naliacha nyumbani Kigamboni ambako
kuna ndugu zangu na familia yangu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment