May 27, 2015



Na Saleh Ally
SIMBA imeanza usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake, kabla ya kuanza kusajili wachezaji wapya, imeanza na wachezaji wake kwanza.

Uongozi wa Simba umelazimika kuanza kuwaongezea mikataba wachezaji wake kwanza ambao imekuwa nao kabla ya kuanza kusajili wapya.

Hali inavyokwenda imeonekana wachezaji ambao wamekulia Simba ndiyo wamekuwa ghali zaidi hata kuliko wale wageni!

Kitendo cha wachezaji wa zamani waliochezea Simba kuwa ghali zaidi kimenifanya nitafakari mambo mengi sana, lakini matatu huenda yakawa ya msingi sana.


Muda:
Vijana waliotakiwa kuongezewa mikataba Simba, wengi walibadilika na kutaka fedha nyingi sana ambazo huenda Simba ingetoa chini ya hapo na kupata wachezaji wengine.

Vizuri kwa kuwa wakati unawaruhusu na vijana nao wanataka maendeleo hivyo ni lazima wapambane kuhakikisha wanapata nafasi ya maisha mazuri.

Ndiyo maana ulisikia Jonas Mkude akifikia hadi Sh milioni 60, Said Ndemla na Hassan Isihaka, kila mmoja Sh milioni 30 na wengine pia walionekana kutaka fedha nyingi zaidi.

NDEMLAKwangu naona sawa kwa vijana kupata maslahi mazuri, lakini bado nabaki kutaka kujua kila aliyepata anastahili?

Msaada:
Timu nyingi za Ulaya si rahisi kusikia zimetoa fedha nyingi au kubwa sana kumsajili mchezaji ziliyenaye, badala yake huongezewa maslahi makubwa hasa katika mshahara na kipato kama posho na mengineyo.

Kwa Simba, wachezaji wengi walitaka fedha kubwa za usajili ambazo hata kama Simba ingetaka mchezaji kutoka nje, basi ingempata kwa fedha hiyo au chini yake.

Mfano, Simba imefanya usajili wa mchezaji kutoka Mbeya City, imemlipa chini ya fedha ilizowalipa wachezaji iliyonao na hii inaonekana ni presha kutoka nje. Kwamba Simba wakimuacha fulani, Azam FC au Yanga watamchukua na wenyewe wataonekana hawana lolote kwa wanachama wao!
 Lakini jiulize, Simba iliyoacha kusajili wachezaji wazoefu igombee ubingwa, ikaamua kubaki na wachezaji makinda kwa misimu mitatu mfululizo, Simba haijawa na mafanikio yoyote!
ISIHAKA.

Imekosa mafanikio kwa kuwa ilisema inawakuza wachezaji. Sasa ilikuwa inawakuza ili iweje kwa kuwa kama ni kutoa fedha, mwisho imesajili kwa gharama sawa au zaidi na ingetaka wachezaji wapya kutoka nje ya timu. Kwa kipengele hiki naona Simba imepata hasara.

Naweza kushauri kwamba kunalazimika kuwa na hesabu za kitaalamu zaidi kuliko kuangalia wanachama watasemaje. Simba lazima iwe inajali suala la faida hata kama ni vizuri vijana kupata maslahi mazuri.

Kama imemsajili Mkude kwa Sh milioni 60, Simba ina uhakika wa kumuuza Sh milioni 150? Kwa kuwa kama haina uhakika, itakuwa imepata hasara mara mbili. Imemkuza halafu ikamnunua yenyewe na mwisho ishindwe kumuuza!

 
MKUDE AKISAINI SIMBA... 
Hasara:
Yanga imepata hasara kwa Mrisho Ngassa ingawa wengi wamelichukulia hilo kama jambo la kawaida tu. Kamwe hauwezi kumuacha mchezaji kama huyo aende akiwa free, wewe usipate hata senti, si sahihi.

Simba inaweza kuingia katika kundi hilo la kupata hasara mfululizo kwa kuwa pia iliwahi kumuongezea Emmanuel Okwi mkataba kwa dola 40,000 (Sh milioni 81), ikatangaza kumuuza ‘bure’ kwa dola 300,000 (Sh milioni 608) kwa Etoile du Sahel lakini hadi leo haijapata kitu!

Si ajabu siku fulani ukasikia Mkude au Ndemla akiondoka Simba kama mchezaji huru, itakuwa kichekesho.

Kukuza, faida yake kubwa ni kuuza. Mfano mzuri ni Barcelona na Cesc Fabregas, ilimuuza akiwa kinda, akakuzwa Arsenal nao wakamuuza tena Barcelona, ikamtumia halafu ikamuuza tena Chelsea. Utaona mchezaji huyu mmoja alitengeneza mamilioni ya fedha.

Kama Simba haitawauza wachezaji hao, itakuwa imepata hasara kwa kuwa tayari imewasajili kwa fedha nyingi zaidi kuliko hata kama ingewanunua kutoka nje ya timu. Unaweza kuifananisha na hadithi ya samaki anayekaanga mafuta!
 Klabu ni taasisi inayopaswa kuingiza faida, si kujifurahisha tu. Kama wachezaji hao wanaigharimu Simba fedha nyingi kuliko ingeleta wengine kutoka nje, hiyo ni hasara kimahesabu kwa kuwa miaka mitatu yote imeingia hasara ya kushindwa kucheza michezo ya kimataifa kwa kuwa ilikuwa ikiwakuza vijana ambao haistahili kugharimika tena kwa kiasi kikubwa labda tu kama ina uhakika wa kuwauza.
Je, hao iliowanunua kwa fedha nyingi baada ya kuwakuza kisoka, ina uhakika itawauza na kurudisha fungu lake?

Bado natetea maslahi ya vijana wa Kitanzania, kwamba akina Mkude, Ndemla na wenzake kupata maslahi mazuri ni jambo jema, lakini wao pia wanapaswa kukumbuka kuwa wana deni na klabu hiyo.

Maana imewakuza, halafu ikawapa nafasi ya kucheza na kuonekana, ndiyo maana leo wanajiona ni watu wakubwa.

Kupewa tu nafasi ni jambo kubwa sana. Sasa wamenunuliwa tena utafikiria wanatokea nje ya Simba! Swali langu wanatambua Simba imegharimika kwa ajili yao na wana deni kubwa?

Wachezaji wengi sana hujisahau kutokana na gharama yao baada ya kuuzwa au kununuliwa! Hawa wa Simba wanajua deni lao, kwamba Simba haikushiriki michuano ya kimataifa kwa kujaza vijana. Sasa wao wanalipwa kama mastaa, wataisaidia ibadilike na kushiriki michuano ya kimataifa?



5 COMMENTS:

  1. Ungetafakari ya Man Utd na Pogba pengine ungebadili mawazo yako na kukubali kuwa Simba haifanyi makosa ila inalinda ilichonacho....

    ReplyDelete
  2. Tatizo ni uelewa wa viongozi wetu wa soka na mikataba wanayoingia!! Agharabu club kumnunua mchezaji wake mwenyewe!! Leo eti arsenal wamlipe walcot pesa ya usajili!!?

    ReplyDelete
  3. Saleh unaamini maneno ya Zakharia HansPope kwamba Singano hana thamani ya tsh.10,000,000/-?

    ReplyDelete
  4. Nyie waandishi mnachekesha. wachezaji wetu wakinunuliwa bei ndogo mnapiga kelele, bei kubwa makelele, sasa mnataka nini? alafu Jonas Mkude amesajiliwa lini? usituchanganye. unapenda kufurahisha watu?

    ReplyDelete
  5. Wote mnaoona simba wanakosea, usipowaongezea hao wachezaji mikataba kwa kuwapa hela unafikiri Azam Yanga na wengine watawaacha tu kwa sababu walikuzwa na simba? Msifananishe mazingira ya bongo na ulaya wakati setup ya mpira wetu na huko ni tofauti kabisa. Hebu toeni alternative kuwa simba wangefanyaje kuwabakiza hao wachezaji bila kuwapa hela. Ulaya wachezaji wengi hawapati signing on fee kwa sababu mishahara yao ni mikubwa sana

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic