May 30, 2015


Na Saleh Ally
TAARIFA zinazohusiana na usajili wa msimu mpya wa 2015-16, ndizo zimetawala kila sehemu, hasa vyombo vya habari.


Kila timu inajitahidi kujiimarisha na jambo la kwanza ni kusajili wachezaji bora kabisa, hakuna anayetaka mambo ya kubahatisha.

Ubaya wa usajili, mara zote huwa hauna uhakika wa asilimia mia, maana unayemsajili naye ni binadamu. Anaweza kufanya vizuri au akaboronga na kukuingiza matatizoni.
AJIBU.
Lakini kama kunakuwa na umakini, basi suala la kutokea hofu ya kubahatisha linakuwa dogo pia kwa kuwa wanaofanya hivyo wanakuwa wanakwenda katika kitu sahihi.

Wachezaji wamekuwa wakitaka fedha nyingi, mfano mzuri ni Malimi Busungu, amewaambia Simba anataka Sh milioni 40, mimi nikajiuliza za nini sasa?

Sifa nzuri ya mshambuliaji ni kufunga mabao. Akiwa na Mgambo FC, Busungu amefunga mabao 9. Najiuliza mabao hayo yanatosha kwake kuona ana thamani ya Sh milioni 40? Ningekuwa najijibu, ningesema hapana.

Inawezekana ningekubali kumuongezea mshahara wake hata mara tatu au nne. Hasa kama analipwa Sh 400,000 au chini ya hapo. Lakini lazima tukubaliane, washambuliaji wengi Watanzania wamefeli, lazima wakubaliane na hilo.

Tathmini nzuri ni Ligi Kuu Bara msimu uliopita kwa kuwa ukiangalia tano bora ya wafungaji, kinara ni Mtanzania, Simon Msuva aliyefunga mabao 17. Baada ya hapo hutapata Mtanzania!

 Wa pili ni Amissi Tambwe wa Yanga, raia wa Burundi mwenye mabao 14, anafuatiwa na Mnigeria anayecheza Stand United, Abasrim Chidiebere ambaye ana 11, Emmanuel Okwi wa Simba kutoka Uganda ana 10, sawa na Didier Kavumbagu wa Burundi.
 
BOCCO
Hata ukisema kumuingiza Rashid Mandawa wa Kagera Sugar, basi lazima agombee nafasi kati yake na Kavumbagu na Okwi.

Lengo si kulaumu, lakini kutoa changamoto kwamba wachezaji wengi wa Kitanzania hawana mwendo bora katika kazi zao.

Mfano mzuri ni wafungaji bora wa miaka miwili au mitatu, Mrisho Ngassa wa Yanga na John Bocco, wameporomoka kabisa.  Msimu uliopita, Ngassa amemaliza akiwa na mabao manne tu na Bocco ana mawili tu, anaweza kusema majeraha, lakini tumo humohumo.

Angalia Ame Ali wa Mtibwa Sugar, alianza mzunguko wa kwanza vizuri sana, akionekana tishio, lakini amemaliza akiwa na mabao 9. Ilionekana angemaliza ligi akiwa na 23 au zaidi lakini wapi.

Tambwe ambaye alikuwa mfungaji bora msimu mmoja nyuma kwa mabao yake 19, aliondoka Simba msimu uliopita tena akiwa ameshaifungia bao moja. Amejiunga Yanga katikati, timu ambayo hajaizoea, kapiga 13. Sasa ameshika nafasi ya pili.
 
MANDAWA (KUSHOTO) AKIPEWA TUZO YA MCHEZAJI BORA WA MWEZI NA WAZIRI WA MAJI, AMOS MAKALLA.
Msimu mmoja alikuwa mfungaji bora, tena ukiwa wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara. Uliofuata akashika nafasi ya pili, utaona kuwa huyu ni mshambuliaji wa aina yake kabisa!

Watanzania wanashindwa nini? Aliyetamba msimu uliopita, atakuwa hovyo kabisa msimu ujao, wanasumbuliwa na ugonjwa gani? Kuvimba vichwa? Kujisahau? Au nini?

Ukweli ni kuwa wamefeli msimu uliopita, tena wengine wakajitangaza majina wakitaka walipwe mamilioni hata yasiyo ya uwezo wao kitu ambacho ni tatizo kubwa.
Kuna kila sababu ya kuangalia msimu ujao.

Maana washambuliaji wengi wa Tanzania wamefeli katika ligi yao ya nyumbani, sehemu pekee ambayo wangeweza kujidai angalau, maana Tanzania haina wachezaji wengi wa kulipwa!

Nyumbani hawapo, wageni wanatamba. Ugenini hawapo kwa kuwa hawawezi kutamba, sasa wanaweza kutamba wapi hawa washambuliaji wa Kitanzania? Lazima watafakari.

Hata wasifiwe vipi, bado haukuwa msimu mzuri kwao kwa kuwa hata mfungaji bora mwenyewe, hakuwa na mabao mengi. Ni chini ya 20, tena chini ya wafungaji bora wa misimu mitatu nyuma. Hivyo kama ingekuwa ni simu wanapiga, basi wrong number. Wajaribu tena msimu ujao.


1 COMMENTS:

  1. Akina Serrunkuma wamelipwa sh ngapi na wamefanya nini!!? Tuache kubeza vya nyumbani!! Kama Okwi na Niyonzima wanachukua zaidi ya mill 80, kwa nini leo Busungu asipate hata nusu yake

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic