July 6, 2015


Na Saleh Ally
NIANZE na pongezi kwa kikosi kizima cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda, The Cranes katika mechi ya kuwania kucheza michuano ya Chan ambayo tayari tumetolewa.


Hakika kwa hali tulitokuwa nayo, sare si jambo la kujivunia. Lakini kutokana na hali tuliyokuwa tumefikia, hatuna ujanja zaidi ya kujipongeza kwa maana ya kuamini mabadiliko waliyoyataka Watanzania, yana ahueni.

Kutoka timu ya kufungwa hovyo, timu ya kuonewa hata na kila mnyonge na angalau kuonekana ni timu inayoweza kujitutumua na kuonyesha kuwa ina makali au inaweza kupambana.

Mechi tano za nyuma, sema dakika 450, Stars chini ya Mzungu mwenye mbwembwe nyingi, Mart Nooij ilikuwa haijafunga hata bao moja. Jana, ndani ya dakika 90 za Charles Boniface Mkwasa angalau ilipata bao moja tena ikiwa imetangulia kufunga.


Sasa ni njia au mwanzo mzuri kuwa Stars inaweza kufunga hata kama ugenini. Unaweza kusema Taifa Stars imeanza safari yake vizuri na kinachotakiwa kufanyika sasa ni kuendelea kuiunga mkono.

Angalia wachezaji walicheza katika kikosi cha juzi pale Nakivubo jijini Kampala, si Yanga na Simba pekee. Angalia washambuliaji walioongoza mashabilizi, au mabeki wa pembeni, si wa Yanga na Simba kama ilivyokuwa hapo awali kwa makocha wa kigeni.

Hii inaonyesha Charles Boniface Mkwasa na benchi lake la ufundi wanaweza kufanya jambo kubwa na kuisaidia timu. Lakini, moja lazima tukubali wanahitaji muda.

Pamoja na kuwaunga mkono kuanzia Mkwasa na wenzake, nimeanza kuona kuna kosa kubwa linafanyika kupitia sehemu mbalimbali kuanzia kwenye mitandao ya kijamii, mitaani na hata katika vyombo vya habari.
 
MKWASA KAZINI STARS...
Hisia za kwamba Mkwasa ndiye kocha sahihi, alichelewa kupewa nafasi na kwa mijadala na mazungumzo inaonekana Mkwasa ndiye kila kitu kama vile sasa Watanzania tumeokoka kutoka katika sehemu tuliyokuwa tumekwama.

Wako ambao wameanza kuamini kabisa kwamba Mkwasa ndiye kila kitu na huenda matumaini ya kuzishinda Misri na Nigeria yamerejea. Jambo hili si sahihi na tukiendelea kulipa nafasi litatuangusha na mwisho tutarudi tena kwenye kulaumina.

Lazima tukubaliane, Mkwasa si mtu sahihi kwa leo na kesho ya Taifa Stars. Mkwasa ni mtu sahihi katika kipindi hiki cha kuleta mabadiliko na maendeleo na mwisho lazima tumuunge mkono.

Kumbukeni Mkwasa ndiyo amepewa timu hiyo ya taifa, ni mara ya kwanza kwake. Hatuwezi kuutaja ubora kupindukia kuhusiana nay eye kama kocha bora kuliko wote na tuamini kwamba tutafanikiwa kila kitu.
 
MKWASA KAZINI YANGA MSIMU ULIOPITA...
Kupewa kwa Mkwasa, tukubali bado ni jukumu zito kwake na kuna mambo kadhaa analazimika kuyabadilisha kwa kujaribu na kupata uhakika kwa vitendo. Lazima tukubali unaweza usiwe wakati wa furaha kuu kwa Taifa Stars kufanya vizuri kwa kiwango cha asilimia mia.

Lakini kuna uwezekano kwa Taifa Stars kufanya vema tofauti na ilivyokuwa chini ya Nooij ambaye alikuwa na maneno mengi kuliko vitendo. Tukubali kuuunga mkono Mkwasa lakini tukubali, si mtu sahihi wa baadaye ambaye atatuvusha kila sehemu tunayotaka.

Tunahitaji kucheza Kombe la Mataifa Afrika, tunahitaji kuvuka hadi Kombe la Dunia. Tunataka kuwa vinara wenye heshima kubwa Afrika Mashariki na kati, heshima ambayo tumeipoteza kabisa na kuonekana hata Rwanda wana nafuu kuliko sisi.

Mkwasa anaweza kututoa tulipo, lakini bado tunatakiwa kupitia sehemu zenye uwezo wa juu zaidi hapo baadaye ili kutimiza tunachokitaka. Kingine muhimu ni lazima Mkwasa na wenzake akina Abdallah Kibadeni, Hemed Suleiman Morocco na wengine wakubali kupokea maoni, halafu wayafanyie kazi kwa njia zao wenyewe. Wasijisahau Stars ikifanya vizuri mara mbili, wavimbe vichwa, wawe wasioambilika wala kushauri. Tutarudi kulekule.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic