July 30, 2015


BAADA ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Kagame, Kamati ya Utendaji ya Yanga, imepanga kukutana na kocha wao Mholanzi, Hans van Der Pluijm kwa ajili ya kupitia ripoti yake ya michuano ya Kombe la Kagame.

Timu hiyo, imeondolewa juzi Jumatano kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kufungwa na Azam FC kwa njia ya matuta kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Katika penalti hizo, Yanga walikosa penalti yao kupitia kwa beki wao mpya wa pembeni, Haji Mwinyi, aliyejiunga na timu hivi karibuni, akisaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la shilingi milioni 10 akitokea KMKM.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, alisema mara baada ya kupoteza mchezo huo, kamati na benchi hilo lililo chini ya Pluijm, watakutana kupitia ripoti ya michuano kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

Muro alisema kikubwa wanataka kujua kipi kilichosababisha wao watolewe katika hatua hiyo ya robo fainali ya michuano ili kuhakikisha wanakiimarisha kikosi chao kabla ya kuanza ligi kuu.

Aliongeza kuwa, kikubwa mashabiki wanatakiwa kutulia na kupunguza jazba zao huku viongozi na benchi la ufundi likijipanga kwa ajili ya ligi baada ya kuondolewa kwenye Kagame.

“Kama ilivyokuwa kawaida yetu, kila mashindano yanapomalizika lazima Kamati ya Utendaji ya Yanga na benchi la ufundi kwa pamoja wanakutana kwa ajili ya kupitia ripoti ya kocha.

“Basi ndivyo tutakavyofanya kama tulivyotolewa na Azam kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Kagame, hivyo viongozi na benchi la ufundi watakutana kwa pamoja kwa ajili ya kupitia ripoti ya michuano hiyo.

“Hivyo Wanayanga wanatakiwa kuwa watulivu katika kipindi hiki huku wakisubiri mambo mazuri kwenye ligi kuu, ikiwemo kutetea ubingwa wa ligi tunaoushikilia,” alisema Muro.
   


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic