September 5, 2015


Na Saleh Ally
MWISHONI mwa Machi, mwaka huu Barcelona ilifanikiwa kuibuka na ushindi kwa kuifunga Real Madrid kwa mabao 2-1 ikiwa inacheza nyumbani Camp Nou jijini Barcelona.


Ushindi wa Barcelona ulikuwa muhimu sana ili kuiacha Madrid kwenye uhakika wa kubeba ubingwa.
Mechi hiyo ya El Clasico ilikuwa ni ya kuua ndege wawili kwa jiwe moja, kuifunga Madrid ghali pia kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

Shukrani ya mabao ya beki Jeremy Mathieu na Luis Suarez. Barcelona ikaibuka na ushindi huo muhimu sana.

Kabla ya mechi na hata ilipoanza, mashabiki wa Barcelona walibeba vipeperushi vilivyokuwa vikionyesha namba 12, huenda wengi hawakujua ni kwa nini.


Mashabiki zaidi ya 95,000 wa Barcelona waliweka rekodi ya kupiga kelele kwa nguvu kuliko wakati mwingine wowote wa mechi za La Liga huku wakiishangilia timu yao kwa nguvu za ajabu na kuwazomea Madrid, hali iliyoelezwa kuchangia kuwavuruga Cristiano Ronaldo na Gareth Bale waliokuwa tegemeo la Madrid siku hiyo.

Leo Watanzania wanashuka uwanjani wakiwa na kazi moja tu kubwa, ‘kucheza’  na kuisaidia Taifa Stars kushinda mechi ngumu dhidi ya Nigeria ‘Super Eagles’ ikiwa ni kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika.

Mashabiki wa Tanzania wanaiweza kazi ya kuwa mchezaji wa 12 uwanjani. Ndicho walichokuwa wakimaanisha mashabiki wa Barcelona siku ile kwamba wao wanaifanya Barcelona icheze na mtu mmoja zaidi uwanjani kwa kuwa wanawapa wachezaji wao nguvu ya kufanya vizuri huku wakiwavuruga Madrid na kuwasababisha wacheze utafikiri wapo pungufu.


Swali, mimi, wewe na wengine tunaweza kucheza nafasi ya mchezaji wa 12 uwanjani na kuisaidia Taifa Stars kuibuka na ushindi kesho?

Jibu ni ndiyo ingawa kuna mawili kwa kila atakayekwenda uwanjani anaweza kuchagua, kucheza namba 12 upande wa Taifa Stars au Super Eagles.

Kwani kama utakwenda uwanjani na kukaa kimya tu au kuizomea Taifa Stars eti kwa kuwa wachezaji wamekosea, basi utakuwa unaishambulia Taifa Stars na huenda ukawa upande wa Nigeria bila ya kujua.

Kikubwa ambacho wanapaswa kukumbuka mashabiki wote wanaokwenda Uwanja wa Taifa kutakapochezwa mechi hiyo ni kwamba wachezaji wa Taifa Stars lazima watakosea kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa.

Ikitokea wamekosea, kushangaa si vibaya. Lakini ni muhimu sana kuwapa moyo na kuwaonyesha mpo nao kwa dakika zote 90.


Kwa haki, lazima tukubali Nigeria wamepiga hatua kisoka kuliko sisi. Wana fedha kuliko sisi lakini hawawezi kuwa na mioyo imara na yenye nguvu ya ushindi kuliko Watanzania wote watakaokuwa uwanjani leo.

Taifa Stars ni timu yangu, yako wewe na Watanzania wengine. Huenda hukuwahi kupata nafasi ya kuwa mzalendo, leo nafasi unayo kubwa na hasa ukijua Taifa Stars inapambana na timu kubwa katika soka la Afrika.

Hakuna kisichowezekana,  Taifa Stars kutafuta ushindi na kufanikiwa dhidi ya timu kigogo kama Nigeria na kufanikiwa kushinda haiwezi kuwa mara ya kwanza.

Wanaoweza kuunganisha nguvu ya kuhakikisha mchezaji namba 12 anacheza kwa kiwango kizuri ni Watanzania wenyewe.

Kutoka uwanjani tumefungwa kutatuumiza sana. Kutoka tukiwa na ushindi, itakuwa ni sherehe yenye furaha isiyokuwa na mfano.



Haya yote yapo ndani ya mikono ya Watanzania. Kikubwa ni kuamini, mchezo wa soka hauwezi kuchezwa bila ya makosa na lazima mambo yaharibike na kurekebishwa hadi ushindi utakapopatikana.



Hivyo tusiende uwanjani na kuwaachia Taifa Stars wachezaji kama kikosi kilicho ugenini sawa na Nigeria walio ugenini.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic