October 12, 2015


Hatimaye uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa timu ya Toto African ya Mwanza inayoshiriki Ligi Kuu Bara umefanyika jana Jumapili  jijini humo.


Uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, ulikuwa ni wa kumchagua mwenyekiti pamoja na wajumbe ambapo ulifanyika kwa takriban saa sita huku ukigubikwa na mvutano mkubwa kutoka kwa wanachama na kamati utendaji ya timu hiyo.

Godwin Aiko ndiye aliyetangazwa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 37 akimpita mpinzani wake, Octavian Komba aliyepata kura 16.

Kwa upande wa wajumbe ambapo nafasi mbili zilikuwa zikiwaniwa, Timothi Kilumila alipata kura 52 na Lushingo Lushingo alipata kura 23 na kuibuka washindi.

Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Toto African ya jijini Mwanza, Mjerumani, Martine Grelics, ametamka wazi kuwa, kama vijana wake hawatapewa fedha wanazodai klabuni hapo, basi hataipeleka timu uwanjani kucheza mechi za Ligi Kuu Bara.

Mjerumani huyo ametamka hayo ikiwa ni siku chache tu baada ya wachezaji wa kikosi hicho kugoma kufanya mazoezi kutokana na madai mbalimbali ya fedha wanazodai klabuni hapo ambazo zinakadiriwa kufikia milioni 12.

Fedha wanazodai wachezaji hao ni za usajili, mishahara na posho za safari za michezo yao ya nje ya mkoa.

“Vijana wangu bado hawajapewa fedha wanazodai na nimewaambia viongozi mpaka ikifika Jumatatu (leo) kama hawajapewa basi mimi pamoja na benchi zima la ufundi hatutasafiri na wachezaji kwenda kucheza mechi zetu jijini Mtwara dhidi ya Ndanda na ile ya Dar es Salaam dhidi ya Yanga, viongozi wanapaswa kutatua tatizo hili haraka,” alisema Grelics.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic