October 12, 2015


Katika kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji inafunga mabao mengi kwenye mechi, Kocha Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, ameanza kutengeneza mbinu mbalimbali zitakazowapa ushindi wa mabao mengi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo, hadi hivi sasa imefanikiwa kufunga mabao saba pekee katika mechi tano za ligi kuu, kati ya hayo matano yamefungwa na mtu mmoja, Mganda, Hamis Kiiza. Lakini Ijumaa iliyopita, Kerr aliamua kuwapa wachezaji wake mazoezi ya kufunga mabao ya mashuti ya umbali wa mita 20, ili wawe na wigo mpana wa kufunga.
  
Zikiwa ni siku mbili kabla ya kusafiri kwenda Mbeya kutafuta pointi sita katika michezo dhidi ya Mbeya City na Prisons, Muingereza huyo alionekana kuwa bize akiwafundisha wachezaji wake kufunga mabao ya umbali wa kuanzia mita 18 hadi 20 kwenye mazoezi yaliyofanyika katika Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam, yaliyotumia saa mbili kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 5:00.

Kerr kwa kuanza mazoezi, aliwataka wachezaji hao kukimbia mbio fupi wakizunguka nusu uwanja kabla ya kufanya programu ya kupigiana pasi kwa wachezaji wawili na baadaye kuhamia katika kuwapa mbinu wachezaji wake jinisi ya kufunga mabao.

Kocha huyo alianza na programu ya kutengeneza mabao kwa kutokea pembeni akiwataka mabeki wa pembeni, Hassan Kessy, Emily Nimubona na viungo wa pembeni Simon Sserunkuma na Awadh Juma kuwapigia krosi wachezaji wenzao zilizofika ndani ya mita 18 kwa ajili ya kufunga mabao.

Wakati mazoezi hayo yakiendelea, wachezaji wake walionekana wakifanya kwa ufanisi mkubwa kwa kufunga mabao, akiwemo Msenegali Pape Nd’aw aliyefunga mabao manne, Joseph Kimwaga matano na Mussa Mgosi matano.

Mara baada ya kuwapa mbinu za kufunga mabao hayo ya mita 18, alihamia kwenye mabao ya mita 20 akiwatumia viungo kutuliza mipira mirefu iliyopigwa na mabeki kwenye umbali huo uliowekewa alama za koni kabla ya washambuliaji kupiga mashuti.

Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, Kerr alisema: “Ndiyo maana leo (juzi) kama ulivyoniona programu yangu ilikuwa ya kuwapa mbinu mbalimbali za ufungaji mabao katika mechi kwa njia tofauti ili mechi zijazo tupate ushindi wa mabao mengi kwa kuanzia mechi na Mbeya City.”


Simba jana Jumapili asubuhi iliondoka Dar kuelekea Mbeya kwa ajili ya mechi dhidi ya Mbeya City Jumamosi hii, kabla ya kuivaa Tanzania Prisons Jumatano ijayo. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic