November 30, 2015


Na Saleh Ally
KATIKA makala zangu Sita, nilizungumzia mambo mbalimbali kuhusiana na timu ya taifa  ya Tanzania, Taifa Stars nikigusa sehemu kadhaa na nyingi nilijifunza baada ya kuwa katika kamati ndogo iliyokuwa ikifanya uhamasishaji wa watu kwenda uwanjani kuishangilia timu ya taifa ikicheza mechi ya kuwania kucheza Kombe la Dunia dhidi ya Algeria.


Niliomba leo ndiyo iwe sehemu ya mjumuisho wa yale niliyoyazungumza kutokana na nilivyojifunza kwenye kamati, niliyoyaona nikiwa na kambi ya Taifa Stars kule Afrika Kusini.

Wakati najumuisha, nitarudi ninapita sehemu nilizoanza kupita mwanzo, lakini safari hii nitakuwa nikieleza ninachoamini kifanyike, kama kweli hasa tuna nia ya kuukomboa mpira wa Tanzania.

WAKOSOAJI:
Nilieleza njia ambazo walipita baadhi ya wakosoaji, waliokuwa wakiipinga kamati ya kuihamasisha Taifa Stars. Tena kamati ikageuka kuwa gumzo kuliko chochote kile, jambo ambalo nilieleza wazi kwamba lilikaa kimaslahi zaidi.

Nilitoa mifano kadhaa kuhusiana na namna ambavyo wakosoaji walionyesha wazi (hasa kama ungetulia na kuzipitia hoja zao) kwamba, kuhubiri soka la vijana wiki moja kabla ya Taifa Stars haijacheza dhidi ya Algeria, kilikuwa ni kichekesho kikubwa.

Sikuamini kama wachezaji wangekuzwa ndani ya siku mbili na kuanza kuisaidia Stars baada ya wiki.
Kamwe siwezi kupinga kuhusiana na soka ya vijana, huenda nimeililia au kuipigia kampeni vilivyo kuliko mwingine yoyote. Lakini najua wakati wake ni upi lakini si wakati timu ya taifa inakwenda kupambana mimi naanza kulia kuhusu vijana.

Kikubwa, hata kunapokuwa na maslahi, lazima tukubali suala la uzalendo libaki namba moja. Kama kila mmoja akiangalia maslahi yake akiamini yeye ni “mfanyabiashara”. Kamwe hatuwezi kuukomboa mpira wa Tanzania.

Kukosoa ni sahihi, kuwa huru ni haki lakini kulikandamiza taifa, bado haiwezi kuwa sahihi hata kama wengine si wepesi kuelewa na kujua unachokosoa ni kwa ajili ya maslahi yako.

Viongozi TFF:
Hakika nilieleza mengi kuhusiana na TFF, shirikisho ambalo ndani yake limeoza na watu wengi sana walio ndani yake kama watendaji, niliwaona si watu wanaotaka maendeleo kwa ajili ya mpira wa Tanzania.

Wengi walio katika nafasi nyeti wanaonyesha si wenye uwezo wa kutusukuma kwenda mbele. Lakini wamezipata nafasi hizo kwa kuwa tu ni washkaji wa bosi au wamekuwa wakimsaidia bosi na wako tayari ‘kufa naye’ kwa lolote.

Tanzania si mtu mmoja, bosi wa TFF hawezi kuwa kila kitu katika maendeleo ya mpira na anapaswa kukubali kuingiza watu wenye uwezo ndani ya shirikisho hilo ili kuleta changamoto.

Kama Jamal Malinzi atakuwa mwoga kukosolewa, kuwa mwoga kupewa changamoto za kiungozi au kuwa na watu walioamka wanaoweza kuona anakwenda taratibu, basi hata mchezo wa soka hauwezi kuwa na mabadiliko.

Viongozi wengi walio katika nafasi nyeti, kamwe hawana uwezo, huenda siku moja nikasimama na kuwachambua zaidi. Lakini TFF lazima ikubali kwamba wanapaswa kukaa kando na kuacha watendaji sahihi wasimame na kuusaidia mpira wetu.

TFF si ya mtu binafsi, ni taasisi ya umma, inawakilisha Watanzania wote kwa kila kitu. Hivyo tabia ya “Umwinyi” ife. Malinzi akubali kubadilika na kuangalia njia sahihi na watu wenye uwezo ili tuisaidie Tanzania.
Hata kama analenga kukuza vijana au vinginevyo, basi lazima kuwe na wataalamu sahihi wenye uwezo wa kusaidia hasa mbio hizo. La sivyo tutaendelea kupoteza miaka rundo huku tukishauriana na kulaumiana halafu hakutakuwa na lolote.

Wachezaji:
Hili ndiyo lilikuwa jambo la mwisho ambalo nililigusa, hii pia ni sehemu nyeti sana. Kwani kama wachezaji watapata kila kitu, halafu mwisho wao wakawa hawajitambui, hakika tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu.

Wale wakosoaji niliowamba kuwa wazalendo wa nchi yetu, wakaamua kuwa wazalendo. Malinzi akaamua kunisikiliza na kufanya mabadiliko kwa kupata watendaji sahihi ndani ya TFF, lakini kama tukawa na wachezaji wasiojitambua, hakuna kitakachofanikiwa.

Kama ingekuwa ni utengenezaji wa bidhaa, basi wachezaji ndiyo wanaopeleka bidhaa sokoni kwa mnunuzi. Maana ndiyo inakuwa mwisho baada ya kila kitu, pale uwanjani, ndiyo wanaotupa majibu.

Wachezaji lazima watambue umuhimu wa timu ya taifa, waitofautishe na klabu na ikiwezekana mioyo yao iwe wazi na si kufanya mzaha au kuamini mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na mingine ni kitu muhimu hata kuliko kazi ambayo wametumwa na Watanzania.

Wachezaji wengi wa Taifa Stars wanaanza kuonyesha hawajui lolote kuanzia machoni mwao. Wanaoamini hata wakifeli kwao si hofu na haiwaumizi.
Binadamu mshindani ni yule anayeumizwa au kukerwa vibaya na kufeli. Lakini hakuna aliyefanikiwa bila nidhamu ya anachokifanya na ikitokea amebahatisha kufanikiwa, basi hatadumu siku nyingi, lazima ataporomoka.

Lakini bado nilipata picha kwamba makosa mengi ya wachezaji walio Taifa Stars, yanatoa picha ya malezi mabovu na ya hivyo kabisa kutoka katika klabu zao.
Hata klabu nazo zinahitaji watu sahihi wa kukaa na wachezaji. Meneja awe mtu sahihi katika nafasi yake. Viongozi, sijui waratibu wa timu wawe watu ambao watawapa malezi bora wakienda katika timu za taifa wawe wanajitambua.

Tunaona malezi ya TP Mazembe yalivyowabadilisha au kuwafanya wawe bora kabisa Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta. Wanakuwa bora kinidhamu, ni kwa kuwa wanaishi katika malezi bora.

Malezi ya kupeana vyeo kishikaji katika klabu au waliopewa uongozi kuishi kishikaji na wachezaji kuliko kikazi, ni tatizo jingine kubwa.

Ubora na nidhamu ya wachezaji haiwezi kutengenezwa katika timu ya taifa. Klabu zinapaswa kujua utovu wa nidhamu au kufeli kwa wachezaji wao katika timu ya taifa ni picha mbaya kwao.

Najua wachezaji wataumia kwa kuwa wasingependa kuelezwa. Lakini lazima wakumbuke, kama tunataka mafanikio lazima kubadilika kutoka hapo tulipo. Kumbukeni, ukililia nguvu za tembo basi lazima ukubali kuwa na mkonga.

Mabao 7-0 waliyofungwa Taifa Stars yalimuumiza kila Mtanzania mzalendo. Wachache waliotamani iwe hivyo, walisuuzika mioyo yao. Kwa wale walioumia, wenye mapenzi ya dhati na hasa wanaohusika na mpira kweli na si maslahi tu, huu sasa ndiyo wakati mwafaka. Zile 7-0 za Algeria, basi ziwe na faida hapo baadaye kwani kama hatutaanza kujirekebisha leo, huko mbele, siku moja zitafika 10 na mwisho tutashindwa kuwaeleza watoto na wajukuu zetu, “vipi kizazi chetu kilishindwa kiasi hicho kulipigania taifa letu!”

MWISHO.


 





1 COMMENTS:

  1. Hongera kwa mchango wako wa fikra nzito kwa hatima nzima ya Taifa Stars. Malinzi analea urafiki na unazidi kumpotezea heshima. Hajifunzi kwa sababu ya arrogance ya kuzaliwa aliyonayo.

    Ni mimi,
    Philemon Muhanuzi shabiki wa Taifa Stars.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic