November 25, 2015


Kiungo Mganda wa Azam FC, Brian Majwega ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumpa ruhusa ya kuitumikia klabu ya Simba ili kulinda kipaji chake.


Kiungo huyo raia wa Uganda alipeleka barua TFF akiilalamikia Azam kwa kushindwa kumlipa mshahara kwa miezi sita lakini anashangaa sasa inamwekea kauzibe ili asijiunge na Simba.

Mganda huyo mwenye uwezo wa juu wa kupiga mipira iliyokufa amekuwa akifanya mazoezi na Simba kwa siku kadhaa hali iliyozua mtafaruku mkubwa kati ya Simba na Azam.

Majwega ambaye anadaiwa kusajiliwa na Simba kwa dau la Sh milioni 40, lakini bado kuna figisufigisu kwani Azam ambayo ilimpeleka kwa mkopo KCCA ya Uganda kudai bado ni mchezaji wake.

 Majwega alisema kuwa ni vyema, TFF ikaliwekea uzito suala lake hilo kwa kulisikiliza kwa haraka kabla ya dirisha la usajili kufungwa ili kuondokana na tatizo alilonalo.

“Lengo langu ni kucheza soka na nimejipanga kuhakikisha nakuwa mchezaji mzuri na kuleta ushindani katika timu yangu na hata katika timu tutakazokutana nazo.

“Nawaomba TFF kuhakikisha wanalisikiliza suala langu kwa haraka zaidi ili niweze kuwa huru na kujiunga na timu nyingine,” alisema Majwega.

Aidha, kwa upande wa Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassoro, alipoulizwa juu ya mchezaji huyo, alisema Majwega bado ni mchezaji wao kwa kuwa aliondoka huku akiwa bado na mkataba.


Kiungo huyo alisaini mkataba wa miaka miwili na Azam na unatarajiwa kumalizika mwakani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic