November 27, 2015


Straika nyota wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, imeng’aa nchini Afrika Kusini na tayari vigogo wa ligi kuu ya nchini humo, Mamelodi Sundowns FC wameonyesha nia ya kumuwania.


Taarifa hizo hazijamfurahisha hata kidogo Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm na tayari ameweka wazi msimamo na mikakati yake ya kuendelea kumbakiza kundini mshambuliaji huyo mpaka mwisho wa msimu.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Mamelodi wamekuwa wakifurahishwa na kiwango cha Ngoma na tayari kuna mazungumzo ya siri na uongozi wa Yanga yanaendelea kwa ajili ya kumuachia nyota wao huyo aliyefunga mabao nane ndani ya mechi tisa katika Ligi Kuu Bara, lakini suala la maelewano ya bei bado halijawekwa mezani rasmi.
 
PLUIJM AKIWA NA NGOMA
“Bado mambo hayajaiva sawasawa lakini muelekeo ndiyo kama huo, Mamelodi wameonyesha nia na kama kutakuwa na nguvu kubwa basi lolote linaweza kutokea ingawa mauzo yake yatahusisha pande mbili, za uongozi na benchi la ufundi, wakiafikiana kunaweza kuwa na biashara,” kilisema chanzo kwa sharti la kutotajwa jina.

Upande wa Pluijm alipoulizwa na gazeti hili alisema: “Ni jambo zuri kwa mchezaji kuhitajika kwingine lakini kwa kipindi hiki, siwezi kumuachia, siwezi kusema kwamba naweza kumzuia moja kwa moja kwa sababu kila mtu ana akili yake lakini bado namhitaji mpaka mwisho wa msimu.”

Taarifa za wachezaji wa Yanga kuhitajika zaidi Sauz si mpya tena, kwa kuwa hivi karibuni Mrisho Ngassa alisajiliwa Free State Stars na Mliberia, Kpah Sherman akatua Mpumalanga Blac Aces na ikumbukwe kuwa kabla ya hapo Simon Msuva alifanya majaribio kwa vinara wa ligi ya Sauz, Bidvest Wits.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic