November 27, 2015


Beki nyota wa kati wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, siku kadhaa zilizopita alivamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kujaribu kuiba fedha.


Beki huyo, aliyevamiwa nyumbani kwake Mapambano, Sinza jijini Dar es Salaam, anakumbukwa kwa kuweka rekodi ya kuwatoa Zamalek katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.

Simba iliwatoa Zamalek kwa njia ya penalti baada ya mechi ya nyumbani kuwafunga bao 1-0 kabla ya kwenda kurudiana Cairo, Miri na kufungwa bao 1-0 kabla ya kwenda hatua ya penalti na kuwatoa baada ya Juma Kaseja kupangua penalti kisha marehemu Christopher Alex kufunga tuta la ushindi.

 Pawasa alisema majambazi hao watatu walimvamia saa 11:30 alfajiri nyumbani kwake na kumtaka atoe fedha alizonazo.

Pawasa alisema, majambazi hao inavyoonekana kama walipewa taarifa za yeye kuwa na fedha nyingi alizopewa akaweke benki na mmoja wa wafanyabiashara wenzake aliyemtaja kwa jina moja (linahifadhiwa) siku moja kabla ya tukio hilo.



“Inavyoonekana kama dili vile limechongwa na watu flani waliokuwa wanajua nina fedha nyingi nilizotoka nazo ofisini na kurudi nazo nyumbani kwa ajili ya kuzihifadhi.

“Kwa sababu hao majambazi walipovamia tu nyumbani kitu cha kwanza kuniambia ni tumefuata fedha zetu, kwa maana ya zile nilizopewa na jamaa yangu ninayefanya naye biashara, kitu ambacho ni cha kweli lakini tayari nilikuwa nimeshazipeleka fedha hizo benki.

“Majambazi hao walikuwa watatu, kati ya hao wawili nilikuwa napambana nao mlangoni wakitaka kuingia ndani.

“Wakati napambana na majambazi hao wawili, mmoja alitoa bunduki na kunipiga na kitako chake na kunipasua usoni, bila kujali nilijaribu kupambana nao hivyohivyo kuhakikisha ninaokoa uhai wangu.

“Baada ya kuona nimewashinda walitoka nje na kukimbilia bodaboda waliyokuja nayo iliyokuwa imeegeshwa nje, mmoja alidondoka, nikafanikiwa kumkamata, muda huo tayari majirani walikuwa wameshasogea baada ya kusikia makelele.

“Tulivyomkamata majirani walimshambulia na baadaye kumpeleka kituo cha polisi kabla ya kupelekwa mahabusu Gereza la Segerea huku wenzake wakitafutwa.

“Baada ya purukushani hizo kumalizika nilienda Hospitali ya Palestina, Sinza kwa ajili ya matibabu, nimeshonwa nyuzi tatu ambazo nimetolewa juzi,” alisema Pawasa.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic