February 8, 2016



Na Saleh Ally
SAYANSI ya mwili wa binadamu inaweza kuwa na mambo mengi sana yanayoweza kuwa mfano katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Mfano huu hapa; sayansi ya mwili wa binadamu inasema hivi; katika mwili wa binadamu, kucha inayoongoza kukua haraka ni ile ya kidole kirefu kuliko vingine, najua hukulijua hili.

Ukuaji wa kucha za binadamu, kasi yake inategemea urefu wa kidole. Kile ambacho ni kirefu zaidi hasa kidole cha kati cha mkono, kucha yake ndiyo inayokua haraka, kifupi, inakua taratibu.

Sayansi hiyo ya mwili wa binadamu huenda ingependeza sana kama ingefanana na sayansi ya makuzi ya soka nchini, iko tofauti kabisa na haifanani hata kidogo.

Kutofanana kwake, huenda kunachangia ukuaji wa mchezo huo kwa kuwa wale wakubwa waliokuwa wanaonekana wanahitajika kuwa na kasi kimaendeleo, kasi yao ya ukuaji ni ndogo sana.

Pamoja na sayansi ya mwili wa binadamu, Mwenyezi Mungu atukuzwe maana ndiye muumba. Anajua na ana maana na utaona inaleta maana. Kama mkubwa, ukue haraka zaidi ili uwe mfano.

Simba na Yanga zimekuwa hazina hata viwanja bora vya mazoezi, lakini zinafurahia na zinaona zinastahili sifa ya kuitwa klabu kongwe nchini, hili sawa.

Kama zitabaki kuwa kongwe kihistoria, lakini wakati husika unazimeza na zinaendelea kuwa klabu kubwa au kongwe zisizokuwa na kasi kubwa ya ukuaji kimaendeleo.

Nimelipigia sana kelele suala hili, lakini kuna taarifa uongozi wa Simba umeishafikia uamuzi wa kutengeneza uwanja wa mazoezi, tayari wameagiza nyasi bandia kwa ajili ya uwanja wao wa Bunju jijini Dar es Salaam. Unaweza kusema, Simba inaenda kuwa klabu yenye malengo kama zilivyo timu za Ulaya au nyingine zenye mafanikio barani Afrika.

Kama kweli Simba wamefanya hivyo, hakika naona wanataka kurejea kwenye usahihi wa kile kidole kirefu kuwa na kasi zaidi ya ukuzaji wa kucha zake.

Wao na Yanga wanapaswa kuwa mfano, Yanga wanao uwanja, bado wanaendelea kusukumana na serikali kuhusiana na kupewa sehemu ya kiwanja ili wajenge uwanja pale Jangwani.

Simba nafasi yao ipo na wana kila sababu ya kujenga angalau uwanja wa mazoezi. Baada ya hapo mambo mengine yatafuatia. Simba haiwezi kuwa klabu kubwa, inayotegemea mapato yake kupitia mchezo wa soka, halafu haina hata uwanja wa mazoezi!

Kama viongozi wameliona hili na kufikia kukata shauri la kuagiza nyasi bandia, hii ni hatua moja kubwa katika kuingia ndani ya mapinduzi ya kuwa klabu ya kweli yenye malengo ya kufika mbali kimichezo na hasa katika mchezo wa soka.

Ninajua, wapo ambao hawatafurahia, huenda hata fedha walizokuwa wakilipa Simba kwenye viwanja mbalimbali zikiwemo shule za sekondari, zilikuwa miradi kwao kwa ajili ya matumbo yao. Hakika hawatafurahia.

Simba haihitaji kumfurahisha mtu mmoja-mmoja. Badala yake inastahili kufanya jambo la maendeleo kwa ajili ya Watanzania bila ya kujali wako mkoa gani au nchi ipi duniani.


Ianze na uwanja, hili lifanyike kweli baada ya hapo, mengi yatawezekana zaidi. Kila la kheri.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic