February 12, 2016


COASTAL

Na Saleh Ally
COASTAL Union na African Sports si vibaya kama utaziita ni timu ndogo na za kawaida kabisa linapofikia suala la kuzungumzia Ligi Kuu Bara.

Wakisikia wale wanaojua historia ya mchezo wa soka nchini, hakika watajisikia vibaya na watakuwa na kila sababu ya kupinga kuhusiana na hilo.

Hawataona sawa kwa kuwa wanapitia katika historia kwamba timu hizo za Tanga zilikuwa bora, moja ilitwaa ubingwa wa Tanzania Bara na nyingine ubingwa wa Muungano.

African Sports ‘Wana Kimanumanu’ na Coastal Union, ukipenda waite Wagosi wa Kaya ni timu kubwa kihistoria.

Hilo linakuwa kazi sana kulifafanua kwa kina wa miaka 18 hadi 25 ambaye anafuatilia mpira kwa sasa. Ataona unampa hadithi za kale ambalo hazina mashiko kwa kipindi hiki.

Wachezaji bora na hatari, tegemeo walitokea Tanga. Walikuwa African Sports na Coastal Union, lakini sasa timu zote hizo mbili zinapigana kuokoa ‘roho’ zao ili zisiteremke daraja hadi la kwanza.

Katika msimamo wa timu 16 za Ligi Kuu Bara, Coastal Union iko katika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 13 sawa na African Sports yenye pointi hizohizo lakini zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga.

AFRICAN SPORTS ILIYOPANDA DARAJA
African Sports wako katika nafasi ya 15 na kama ligi ndiyo ingekuwa mwisho, basi timu zote mbili za Tanga zingeporomoka daraja na kuiacha moja tu ya Mgambo Shooting ambayo ina pointi 17 katika nafasi ya 10.

Mgambo ni mjukuu unapozungumzia African Sports na Coastal Union. Inaonyesha tofauti kubwa kuliko timu hizo kongwe ambazo zimejaza watu wengi wabinafsi, wanaoamini wanajua sana kumbe hawajui, wenye roho mbaya na wasiopendana.

Wanachama na mashabiki wa Coastal na African Sports hawana umoja, maana yake hawapendani. Viongozi wanalumbana kila mara, wako ambao wamegeuka timu kama za ukoo na si watu wanaosikilizana.

Kitu kibaya zaidi wao ndiyo wanaozikwamisha klabu hizo, lakini wepesi kulalamika wanaonewa au wanahujumiwa. Wanajua kila baada ya kukosea wana nafasi ya kumuangushia mtu mzigo kwamba amewaonea au vingine.

Watu walio kwenye uongozi wa timu hizo si wabunifu, si walio tayari kupambana kwa dhati kwa kuwa nguvu nyingi iko mdomoni katika ulalamikaji kuliko utendaji.

Coastal na Sports zinaongoza kwa malumbano, mizozo na si mipango ya maendeleo ndiyo maana hujawahi kusikia hata siku moja viongozi wakakaa na kuwatangazia wamepanga kujenga uwanja, kutengeneza na kuingia kwenye biashara ya jezi na vifaa mbalimbali vya klabu au kwa ujumla, kuzungumzia masuala ya kibiashara kwa ajili  kuifanya klabu kujiendesha na kuepukana na utegemezi.

Wakati ilipopanda African Sports msimu huu, wadau wengi wa soka waliamini ule wakati wa ushindani mkubwa wa akina Razack Yusuf ‘Careca’, Kassim Napili, Kassa Mussa na wengine umerejea tena.

Inachezwa mechi ya watani hao, utafikiri timu za mchangani. Hata mashabiki hakuna na hii ni kwa kuwa muonekano, ushindani na nguvu ile ya miaka ya 1980 na 1990 haipo tena. Je, viongozi wanaoziongoza timu na klabu hizo wanalijua au wanaliona hilo?

Maisha hayawezi kwenda kwa historia, watu wa Tanga lazima waungane na kubadilisha hali ilivyo sasa na aibu inayowakuta ambayo hakika itawafanya waonekane ni watu wanaobahatisha katika mambo yanayowezekana.

Mimi msisitizo wangu unabaki uleule, Coastal na Sports ni timu zinazobeba hisia na mapenzi ya watu. Zinabeba heshima na hisia za watu wa Tanga. Viongozi wanaoongoza, kama wanaona wamefeli, basi lazima wajue wamefeli, wakubali na wakae kando kwa kuwa klabu hizo si mali yao binafsi au mali za familia zao.


Hauwezi, kaa kando. Tanga ina watu wengi wenye ujuzi, elimu, vipaji na hamu ya mafanikio wanaweza kusaidia mabadiliko. Achaneni na yale mambo ya “Tulikuwepo tokea enzi zile”, huku mkiwa hamfanyi lolote la maana!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic