March 30, 2016

PLUIJM


Na Saleh Ally
MABINGWA watetezi wa Tanzania Bara, Yanga SC, wana jukumu la kuivaa Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi ya kwanza inatarajiwa kupigwa Aprili 9 jijini Dar es Salaam, halafu zitarudiana jijini Cairo katika mechi ambayo kama hakutakuwa na dira ya nani aliyefanya vizuri, majibu yatapatikana katika mechi hiyo.

Yanga imefikia hatua ya pili baada ya kuvuka ile ya awali na ya kwanza kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius na baadaye APR ya Rwanda. Sasa inakutana na wababe wa Afrika ambao wamekuwa katika kipindi cha mpito. Sasa angalau wanaonekana kuanza kukaa sawa.

Hakuna ubishi haitakuwa kazi rahisi kwa Yanga na kocha wake mkuu, Hans van der Pluijm, anakiri kwamba wana kazi kubwa na wanatakiwa kufanya kazi kwa ubora wa juu zaidi ya mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika walizocheza.


Pluijm, raia wa Uholanzi, anaamini mechi mbili zijazo ni ngumu zaidi. Lakini anaona kama hakuna uzalendo wa kuhakikisha Yanga inafanya vizuri. Pia anaamini huenda Watanzania wataiongezea Yanga ugumu wa kufanya vizuri, anasema watakuwa wamekosa uzalendo na wanapaswa kulitafakari hilo.

Katika mahojiano maalum na SALEHJEMBE, Pluijm anasema Yanga ina kipindi kigumu lakini ugumu unaongezeka zaidi kutokana na mabadiliko ya ratiba yanayoikandamiza yenyewe.

SALEHJEMBE: Ratiba inakupa ugumu upi?
Pluijm: Umeona yamefanyika mabadiliko ya mechi za Ligi Kuu Bara. Ndani ya takriban siku 14 tutacheza hadi mechi tano, hasa ukijumlisha na ile ya Kombe la FA na ile dhidi ya Al Ahly.

SALEHJEMBE:  Unafikiri kikosi chako hakina uwezo huo?
Pluijm: Hata timu nyingine yoyote ya Ulaya isingekuwa na uwezo huo. Hapo unatengeneza uchovu na wachezaji wengi kuwa majeruhi.


SALEHJEMBE:  Kuwa majeruhi kwa namna gani?
Pluijm: Sikiliza nikuambie, unapocheza mechi nyingi mfululizo ni rahisi sana wachezaji kupata maumivu au kuumia. Ndiyo maana Al Ahly kabla ya kukutana na sisi watacheza mechi moja tu. Shirikisho lao linalijua hilo na linataka kuwarahisishia kazi, hapa kwetu imekuwa tofauti.

SALEHJEMBE:  Unaweza kuwatumia wachezaji kwa kuzunguka. Najua Yanga ina wachezaji zaidi ya 25, tatizo ni nini?
Pluijm: Mechi za mwisho za ligi zina presha zaidi. Kumbuka tuna viporo, kila pointi ina umuhimu zaidi ya mwanzo wa ligi. Hatuwezi kufanya majaribio katika hatua hii. Wachezaji haohao wakicheza mechi zote hawataweza.

SALEHJEMBE:  Labda umewasiliana na uongozi wako ili uwasilishe suala lako TFF?
Pluijm: Tayari, lakini hata wao TFF walipaswa kujua Yanga inakwenda kupambana na Al Ahly kwa ajili ya taifa. Sasa haiwakilishi Wanayanga pekee, wangetoa nafasi ya maandalizi ya uhakika. Yanga si timu kubwa kama Al Ahly inabanwa kwenye maandalizi wakati Al Ahly ambao ni wakubwa wamepewa nafasi kubwa wajiandae kwa nafasi.

SALEHJEMBE:  Ikitokea TFF hawatakubaliana na Klabu ya Yanga, utachukua uamuzi gani?
Pluijm: Nitapeleka timu ikapambane katika mechi zote, lakini nikuhakikishie kutakuwa na madhara kwetu na si sawa hata kiafya ukizingatia tutasafiri sana na pia kuna suala la viwanja vibovu pia.

SALEHJEMBE:  Kama hilo linawezekana, si bora kulifanya kwanza, kuogopa kufeli si sahihi wakati uwezo unao!

Pluijm: Nani kasema naogopa kufeli? Nimeiongoza Yanga kwa muda wote bila kugusa mambo ya TFF, lakini sasa naona napaswa kuweka wazi lakini haitaizuia Yanga kupambana. Kikubwa niendelee kusisitiza kwamba TFF wanapaswa kuliona hilo, timu hii inawakilisha timu kimataifa. 

Hii ni kwa ajili ya faida ya taifa letu, tafadhali waeleze kwamba waache ushabiki wa mambo ya siasa za Simba na Yanga, tutaanguka. Michuano ya Afrika katika makundi mbalimbali ni tatizo katika soka hapa nchini. Vizuri kulimaliza ili Tanzania nayo ipige hatua.

2 COMMENTS:

  1. Kweli,TFF waangalie kwa kina maana ni kama wanaiadhibu yanga bila sababu,pamoja na kwamba mimi si mpenzi wa YANGA lakini naangalia utaifa kwanza.

    ReplyDelete
  2. Nyie si wakimataifa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic