March 21, 2016



Na Saleh Ally
GUMZO la fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, rasmi limeanza hasa katika hatua hii ya robo fainali pale zinapobaki timu nane ambazo zinachujwa hadi nne na mwisho mbili.

Ubishi utamalizwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Giuseppe Meazza katika Jiji la Milan nchini Italia, lakini gumzo limepaa zaidi, baada ya kupangwa kwa ratiba, nani atakutana na yupi!

Kwa namna mwendo unavyokwenda, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kukutana kwa timu ambazo zilitegemewa kucheza fainali hiyo kama ambavyo imeanza kuonekana mapema katika hatua ya robo fainali.

Timu ambazo hazikupewa nafasi hata kidogo, sasa zimefika robo fainali. Mfano mzuri ni Benfica ya Ureno, Wolfsburg ya Ujerumani na hata Manchester City.

Pia unaweza kuona robo fainali haihusishi tena timu kama Man United, Arsenal, Borussia Dortmund, Valencia, Sevilla ambazo hazikuwa na nafasi kabisa. Angalau Arsenal, lakini nao wamekwama njiani.

Kawaida, kuanzia hatua hiyo huwa ni vigogo pekee, timu hizo tatu bado zina nafasi ya kufanya vema na kubadilisha mambo na hasa kwa kuwa kuna mechi ambazo zinaonyesha vigogo watakuwa katika wakati mgumu na lazima wajichunge.

Mfano, mechi ambayo inazikutanisha timu mbili za Hispania, Barcelona na Atletico Madrid. Kwa mtazamo wa haraka utaipa nafasi Barcelona ambayo inalindwa na rekodi kwa wingi ambazo ni nzuri lakini haifuti kuwa Atletico imewahi kuing’oa Barca katika michuano hiyo.

Kiasi fulani, Bayern Munich wanapewa nafasi kubwa kwa kuwa Benfica kwao wanaonekana kuwa ni mchekea, lakini bado kama wamefika robo fainali bila ya kutegemewa wangefanya hivyo, basi wanaweza kuingia kwenye nusu fainali bila kutegemewa pia.

Benfica wako katika kipindi cha kurejea tena, pia kutafuta heshima ya michuano hiyo ambayo nchini Ureno inawahusisha FC Porto pekee ambao ni wapinzani wao.

Lazima tukubali mpira unadunda, pia hupaswi kwenda na matokeo yako mkononi kwa kuwa soka ni mchezo unaohusisha makosa ya binadamu mmojammoja. Hivyo lolote linaweza kutokea.


Real Madrid pia hawapaswi kuidharau Wolfsburg kwa kuwa inaonyesha inatokea Ujerumani, nchi ambayo mara nyingi Bayern Munich pekee ndiyo imekuwa na uhakika wa kufika hapo. Safari hii Wolfsburg nayo imekuwa ‘sumbufu’ kama ilivyokuwa kwa timu nyingine Ujerumani kupindi cha nyuma.

Kama unaikumbuka VfB Stuttgart, kabla ya hapo ilikuwa ni Bayer Leverkusen na sasa Wolfsburg. Madrid pia hawawezi kuisahau Borussia Dortmund ambayo ilikuwa chini ya Jurgen Klopp na mshambuliaji wao hatari, Robert Lewandowski.

Kwa timu kubwa kama Real Madrid, kama itafanya mchezo na Wolfsburg, basi watajilaumu baadaye. Ligi ya Ujerumani maarufu kama Bundesliga ina kiwango cha juu ingawa haina matangazo ya kutosha. 

Ndiyo maana timu inayotokea katika ligi hiyo kucheza michuano ya Ulaya mara nyingi imekuwa ikifanya vizuri na mfano mzuri utaona timu za Bundesliga mara nyingi zinaingia robo, nusu fainali au fainali yenyewe na si jambo gumu kwao.

Aprili 5, kazi itaanza na si mbali sana. Kila timu lazima itataka kujiandaa vema kwenda fainali. Barcelona inaweza kuwa na nafasi ya kusonga kwa kuwa inakutana na timu ngumu kutoka Hispania. Hapa atakuwa makini zaidi lakini kama wataruhusu presha iwachukue, basi mpira utaangukia kwa Atletico.

DONDOO MUHIMU:
• Wolfsburg na Real Madrid hawajawahi kukutana kabisa. Ila nyota wao, Julian Draxler, alikuwa mchezaji wa Schalke 04 wakati ilipokutana na Madrid na kufungwa hatua ya 16 Bora msimu wa 2013/14.

• Bayern wameshinda mechi nne kati ya sita walizokutana na Benfica. Mbili ni sare na timu hizo hazijakutana tangu mwaka 1995.

• Barcelona wameshinda mechi zao sita za mwisho walizokutana na Atletico, Lionel Messi kafunga mabao matano.

• Messi amefunga mabao 25 katika mechi zote 27 dhidi ya Atletico. Pia amepiga ‘hat-trick’ tatu.

• Barcelona na Atletico walikutana robo fainali ya msimu wa 2013/14. Atletico wakashinda kwa bao 1-0 nyumbani, hiyo ilikuwa ni baada ya sare ya bao 1-1 ugenini.

• Huu ni msimu wa tatu mfululizo, Atletico inakutana na timu ya kwao Hispania katika hatua ya robo fainali. Mara ya mwisho waliondolewa na Madrid miezi 12 iliyopita.

• Paris Saint Germain na Manchester City walikutana kwenye hatua ya makundi msimu wa 2008/09 UEFA, matokeo yao yalikuwa ni sare, sasa ni kazi ya uthibitisho nani zaidi.

APRILI 5 & 13
Bayern Munich v Benfica
Barcelona v Atlético Madrid

APRILI 6 & 12
Wolfsburg v Real Madrid
Paris v Manchester City

 NCHI:
Hispania (3)
Ujerumani (2)
Ureno
Ufaransa
England


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic