March 14, 2016


Na Saleh Ally
SIMBA ilishuka uwanjani kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons ya Mbeya. Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jiji Dar es Salaam ni ya 23 kwake.

Wakati Simba imecheza mechi ya 23, Azam FC inaendelea kubaki na mechi 20 wakati Yanga imecheza mechi 21 tu.

Ukiangalia timu ambazo zinashinda kileleni ni Simba, Yanga na Azam FC. Hizi mbili za Azam na Yanga zinashiriki michuano ya kimataifa ya Caf. Huenda ndiyo kigezo TFF wanataka kukitumia timu moja kuwa na viporo vya mechi tatu na moja viporo vya mechi mbili.

Yanga wakati wanarejea, watakuwa na mechi mbili kibindoni wakati Azam FC wana mechi tatu ambazo hawajacheza. Hili suala limeanza kuzungumzwa takriban wiki tatu zilizopita na TFF ilikuwa ikijikanyaga kutaka kuiangushia mpira Bodi ya Ligi ambayo ilikiri TFF inahusika. Hili ni lile sakata la kuiruhusu Azam FC kwenda kushiriki michuano kule Zambia na kuacha ligi ikiendelea.

Kinachoonekana hapa ni umakini wa chini kabisa wa TFF na Bodi ya Ligi katika suala la upangaji wa ratiba kwa kuwa zinatengeneza mazingira kwa timu fulani kuwa na nafasi ya kufanya inavyotaka, nitaeleza kwa nini.

Wakati TFF inapanga ratiba, kawaida inakuwa inajua michuano yote ya Caf inatakiwa kuchezwa lini. Ninamaanisha Ligi ya Mabingwa kwa Tanzania wawakilishi ni Yanga na Kombe la Shirikisho ambalo tunawakilishwa na Azam FC.

Kama TFF inakuwa inajua, hakika si vibaya kuwepo kwa kiporo cha mechi moja. Hii unaona inatokea hadi Ulaya. Lakini hakuwezi kuwa na mechi tatu kwa timu moja haijacheza.
Mfano kama Azam FC ina mechi tatu, vipi Yanga ina mechi mbili kibindoni? Bado utaona wazi kabisa kuna hali ya uzembe au figisu na inawanyima haki Simba na timu nyingine.

Utaona, Azam FC imefikisha viporo vya mechi tatu, eti kwa kuwa ilitakiwa kwenda Afrika Kusini mapema. Lakini Yanga ikacheza mechi moja kwanza halafu ndiyo ikaondoka kwenda Kigali. Tofauti ya safari zao, Yanga inatumia karibu saa mbili hadi Kigali, Azam FC inatumia saa tatu na dakika ishirini. Kipi kilifanya Azam wasicheze mechi yao moja?


Lakini vipi kwingine wanaweza na tofauti ya kiporo inakuwa ni moja tu! Vipi hapa TFF inashindwa na hili ndilo tatizo kubwa linaloendekezwa na mwisho litakuwa matatizo.

Timu moja inapobakiza mechi nyingi mkononi, hii hujenga hisia ya hofu ya kupangwa kwa matokeo. Hili limekuwa likihofiwa duniani kote, ndiyo maana timu hutakiwa kucheza mechi kwa wakati mmoja ili kuliepusha.

Sisemi Yanga au Azam wamepanga matokeo, lakini bado si haki kwao kuwa na mechi tatu mkononi na hili hauwezi kuona linatokea katika nchi yoyote. Kwenye nchi nyingine, wanaohusika na upangaji ratiba pamoja na wasimamizi wake kama TFF, hauwezi kuona wanafanya kama inavyofanyika hapa nyumbani.

TFF wanapaswa kuwa makini, kwani hali inavyokwenda wanaonekana kufanya mambo mengi ya kubahatisha na bahati mbaya wanakuwa na uhusiano mwingine nje ya ligi, jambo ambalo linaweza kupelekea hisia ambazo si sahihi. Kwamba wanaipendelea Azam FC kwa kuwa kampuni yao nyingine inadhamini ligi.
Mimi niende moja kwa moja bila ya kona, kwamba wanachofanya TFF katika suala la ratiba si sawa, ni ubabaishaji wa mambo na wanapaswa kujipanga vizuri.

Natuma salamu zangu tena kwa Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, kwamba katika kipindi chake mambo yanazidi kwenda shaghalabaghala na hili niliwahi kuzungumzwa kuhusiana na uwezo wake kwa maana ya kuwa na uzoefu mdogo kabisa katika nafasi hiyo, akakasirika.

Lakini sasa mambo yanafeli yeye akiwa dereva, hivyo lazima akubali kwamba anapaswa kubadilika. La sivyo, hisia za timu fulani zinatengenezewa mazingira ya ubingwa, haziwezi kuisha na mwisho zitazaa ukweli.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic