April 29, 2016



JUMAMOSI iliyopita niliandika na kuelezea namna safari yangu ya kwenda Hispania ilivyokuwa na namna nilivyowaza kama ningepata nafasi ya kuhojiana na wachezaji nyota kabisa duniani kama Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

Wako wengi nilitamani kuwapata kama Dani Alves, Iniesta, Sergio Bosquet na wengine ambao kila mwandishi au kila chombo cha habari kingependa kuzungumza nao mawili matatu na kuandika au kuripoti.

Nilieleza namna hata wenyeji wetu ambao ni La Liga ambao ndiyo wanaongoza Ligi Kuu ya Hispania, walionekana kuzungumzia ugumu wa kuwapata watu hao wenye ulinzi mkubwa kupita unavyojua.

Nimeripoti kwenye Michuano ya Kombe la Dunia, Kombe la Mataifa Afrika na mechi kadhaa za kimataifa. Sijawahi kuona ulinzi mkali kama wa wachezaji hao.


Mfano nilielezea namna wachezaji kama Messi, Neymar, Iniesta, Suarez walivyoongozwa na mabaunsa hata walipopita kwenye Mixing Zone (hii ni sehemu maalum ya waandishi wa habari kwa ajili ya kuwahoji wachezaji wakati wakiondoka kwenda kwenye basi lao). Nilishangaa, yaani kwa Messi, Suarez, Iniesta na Neymar hata waandishi hawaaminiwi!

Pamoja na yote hayo, juhudi zilifanyika, waliulizwa maswali, baadhi walijibu na wengine la. Hakika haikuwa rahisi kutokana na mazingira yake.


Kabla ya hapo, nilifanikiwa kujifunza namna wachezaji wa timu za La Liga wanavyoingia uwanjani, namna mashabiki wanavyoonyesha hamu kuu ya kuwaona na ulinzi mkali unaowekwa kuhakikisha tuko salama.

Mimi ninaposafiri, ninakwenda kwa niaba ya chombo cha habari ninachokitumikia. Kama ni rekodi mpya, Gazeti la Championi ndiyo limefika katika hatua nyingine mpya ambayo itakuwa mfano na changamoto kwa wengine.

Kama unakumbuka, miaka zaidi ya mitano iliyopita, nilifunga safari hadi Malawi kumfuata Didier Drogba aliyekuwa nchini humo ambapo nilifanya naye mahojiano ya ana kwa ana kabla ya kurudia tena jijini Dar es Salaam.

Mahojiano na Drogba, yaligeuka kuwa chachu ya waandishi wengi kuamini inawezekana, wakatamani kusafiri na kufanya mahojiano sehemu mbalimbali. Ilikuwa ni rekodi mpya na mapinduzi mapya yaliyofanywa na Championi na kubadilisha aina uandishi, kuachana ule wa kusubiri kila kitu na sasa kuanza kusaka mambo mapya ikiwezekana kwa safari ndefu na ngumu ili kutimiza ndoto.


Safari hii, Championi limefika mbali, karibu na Messi, lakini mambo hayakuwa mazuri. Karibu na Suarez na mahojiano mafupi kwa kuwa alijibu swali kama Alves, Neymar akaeleza hisia zake kwamba Kingereza hakipandi.

Inabaki palepale, bado wasomaji wetu wanahitaji zaidi ya pale. Ugumu wake hakika uko juu, lakini bado tunahitaji kupambana kwa ajili yao.

Najua hili nalo litakuwa changamoto kwa wengine na sasa wanaweza kutamani kufika mbali zaidi ikiwezekana England, Ujerumani na kuwapata wachezaji wa Manchester United, Arsenal na wengine au wale wa Bayern Munich, Dortmund na wengine.

Hakuna anayeweza kukataa tena kwamba Championi limeandika rekodi nyingine mpya ya ubunifu, uanzilishi na hii ni kwa niaba ya wasomaji.

Wasomaji wa Championi lazima wajue, huenda tunalala kwa shida lakini tukiwaza nini cha kuwapa sahihi. Safari yangu kwenda Hispania ilikuwa ndefu, yenye maumivu ya uchovu na ratiba ndefu iliyopandana, lakini kila nilipowafikiria wasomaji, nilisema; “Sitaki kuwaangusha”.

Huenda sijafanikiwa kwa kiasi kitakachowaridhisha wote kwa asilimia mia japokuwa bado tunaendelea kubuni, kuwazua na kujipanga kuweka rekodi kibao na kuwapa wasomaji heshima yao ya kupata wanachotaka.

Niwashukuru Azam TV kwa ushirikiano wao wa juu katika safari yangu ya Hispania. La Liga pia ambao waliniamini na kunipa nafasi ya kufanya mengi ikiwa ni pamoja na kwenye runinga na mtandao wao.

Kwa wasomaji, ninawaomba waendelee kutuamini na tunaendelea kupambana kwa ajili yenu.

Kwa waandishi wengine, hii ni changamoto mpya kwenu, ushindani wetu utaongeza ubora. Kwa wale mliokubali tunachofanya nanyi mkafanya vyenu, ni vizuri sana. Wengine pia mnaweza kufuata ili tuifanye tasnia hii yenye ushindani na mambo mapya na mazuri zaidi kwa wasomaji.

Kwa upande wetu Championi, sasa ndiyo asubuhi na mapema, wasomaji wetu shukurani kwenu.

Saleh Ally

Mhariri Kiongozi-Championi

2 COMMENTS:

  1. Hongera sana hata mimi kama muandishi wa habari ambae ndio kwanza nimegraduate chuo kikuu Dar es salaam,ndoto zangu ni kufanya aina hiyo ya uandishi na sio kusubiri BBC AU CNN watoe habari ni sisi kuwa booster media.Kwa wale wajasiriamali msisahau pia kupitia MUKEBEZI BLOG au bonyeza shareinfogrouptanzania.blogspot.com. Najua kufanya hii back link sio kosa kwasababu pia ni muendelezo uleule wa kuwasaidia wa Tanzania.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic