April 13, 2016



Na Saleh Ally
SIMBA imetolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA Cup) katika hatua ya robo fainali baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union.

Coastal Union wameing’oa Simba kwa kuichapa, tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, sehemu ambayo haikuwa rahisi mtu kuamini ingekuwa hivyo.

Katika mechi hiyo, Simba ilionyesha mchezo wa kuvutia, pasi nyingi na mbwembwe lakini vyote havikuwa na faida kwenye timu.

Utaona uchezaji wa Simba ulionyesha si waliokuwa wakicheza mechi ya mtoano. Ilikuwa kama wanasaka pointi katika mechi ya Ligi Kuu Bara, jambo ambalo halikuwa sahihi.

Mwisho, Coastal waliibuka mashujaa wa mchezo huo. Coastal inayoongozwa na wachezaji wanaoishi maisha magumu, mishahara ya tabu, waliweka moyo wa kutaka kuona wanasonga mbele na kweli wamefanikiwa kukatiza ndoto ya Simba ambayo ina kiu kuu ya kutaka kushiriki michuano ya kimataifa.

Bingwa wa michuano hiyo, atashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Simba haijashiriki michuano ya kimataifa sasa ni msimu wa tatu. Imekubali ndoto hiyo ‘ibebwe’ na Coastal ambao hakika hakuna aliyewatarajia.

Tayari Simba wameanza kuangushiana lawama za chinichini. Jambo ambalo si sahihi lakini wapo ambao walikuwa chanzo cha kuua umoja katika mechi hiyo au kutokuwa makini, kukachangia wao kung’oka.

Kiiza&Juuko:
Kocha Jackson Mayanja, alilazimika kuwaweka benchi beki Juuko Murshid na mshambuliaji Hamisi Kiiza kutokana na kuchelewa kwao kurejea kambini.
Mayanja aliamini hawakuwa fiti, akafanya hivyo, jambo ambalo kocha yeyote mwenye kuijua kazi yake angefanya hivyo.


Wachezaji hao wawili ambao wote ni tegemeo, wamechangia kwa kiasi kikubwa Simba kufungwa kwa kuwa kukaa kwao nje, kulichangia Simba kushindwa kufanya vema. Kiiza aliingizwa kipindi cha pili akafunga.
Huenda angekuwa fiti, angesaidia kuanzia kipindi cha kwanza. Wanapaswa kulaumiwa kwa kuwa walijua Simba ipo kambini kwenye maandalizi muhimu ya mechi ya mtoano, vipi walibaki Uganda?

Wachezaji wengine:
Kweli Kiiza na Juuko ni tegemeo. Lakini wameonyesha si wanaofuata weledi na huenda wameanza kulewa sifa, sawa. Lakini vipi waliokuwepo uwanjani hasa waliopata nafasi wakashindwa kuisaidia timu?
Maana yake kama Simba inacheza bila Kiiza wala Juuko haiwezi kushinda? Lazima wachezaji wajipime na wanapopata nafasi wazitumie na kuisaidia timu yao. Wao pia ni sehemu ya chanzo.

Viongozi:
Viongozi waliona mapema Kiiza na Juuko walikuwa “wakiwazingua”. Ajabu walitumia muda mwingi kulalamika badala ya kuchukua hatua.

Inawezekana bora kukosa kuliko mtu kuleta mchezo kazini tena kwa wao wanaolipwa mishahara minono.

Hawakupaswa kuwa kimya muda mrefu badala yake walitakiwa kuwabana mapema akina Juuko na Kiiza na hata adhabu ingekuwa mapema zaidi, huenda ingesaidia.

Sasa Simba, imetolewa katika michuano hiyo lakini Simba hawana wa kumlaumu badala ya wao wenyewe kuvurugana.



Vizuri zaidi kwao itakuwa ni kujipanga na kukubali wameboronga na kutolewa na sasa ni kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na wasirudie kosa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic