April 6, 2016



Kikosi cha timu ya Simba kwa sasa ndiyo kinaongoza Ligi Kuu Bara kikiwa na pointi 57 ikibakiwa na michezo sita tu kuhitimisha msimu huu ambao ambao wamedhamiria kufanya kweli kuliko misimu miwili nyuma.

Simba iliuanza msimu huu kwa kasi ikiwa chini ya Kocha Muingereza, Dylan Kerr, mpaka sasa inanolewa na Mganda, Jackson Mayanja inaonekana kasi yao hiyo imekolea kwani tangu kocha huyo akabidhiwe timu hiyo amefanikiwa kuiongoza kushinda mechi 10 za ligi na kupoteza moja pekee.

Inaonekana hivi; misimu miwili nyuma kipindi kama hiki cha mwezi Aprili, Simba haikuwa katika harakati za kuwania ubingwa huku ikiziachia Yanga na Azam zikitamba.

Msimu wa 2013/14, mwezi na tarehe kama hizi Simba ilikuwa imecheza 24, ilijikusanyia pointi 37, ikishika nafasi ya nne, huku ikifunga mabao 40 na kuruhusu kufungwa mabao 25.

Huku Simba ikiwa katika hali hiyo, wapinzani wake, Yanga na Azam, walikuwa wanakimbizana nafasi mbili za juu, Azam ilikuwa kileleni na pointi zao 56, huku Yanga ikishika nafasi ya pili kwa pointi 52. Mbeya City iliingilia kati na kushika nafasi ya tatu kwa pointi zao 46.

Mwisho wa msimu huo, Simba ilimaliza ikiwa nafasi ya nne ikiwa na pointi 38, ikifunga mabao 41 na kuruhusu mabao 27, bingwa alikuwa Azam.

Msimu uliofuata nao kipindi kama hiki, Simba ilikuwa imeshacheza mechi 19 ikiwa imejikusanyia pointi 32, ikifunga mabao 25 huku ikifungwa mabao 14 na kushika nafasi ya tatu.

Ndani ya msimu huo pia Simba ilikuwa chini ya Azam na Yanga. Yanga walikuwa wakiongoza ligi wakiwa na pointi 40, Azam ikishika nafasi ya pili na pointi 37.

Mwisho wa msimu huo, Simba ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 47, ikifunga mabao 38 na kuruhusu mabao 19, bingwa alikuwa Yanga.


Utaona tofauti ya pointi kwa kipindi hicho ilivyokuwa baina ya Yanga na Azam dhidi ya Simba, lakini kwa sasa Simba ndiyo imeziacha timu hizo licha ya kuwa mbele kwa michezo miwili, lakini hata kama Azam ikishinda mechi zake hizo haiwezi kuishusha Simba, angalau Yanga kama ikishinda inaweza kuipita Simba pointi mbili tu.

Kutokana na takwimu hizo, msimu huu unaonekana kuwa Simba ilikuwa ikijiuliza tangu awali ilikuwa inakosea wapi na tayari imelibaini tatizo hilo kwani kasi yao inazitishia Yanga na Azam.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic