April 22, 2016

Na Saleh Ally, Coruna
MTEMBEZI ambaye anatafuta kujifunza si sawa na aliyekaa tu nyumbani akiamini vitu vitakuja na kumfuata mahali alipo.



  Kila ninapopata safari hasa zinazohusiana na masuala ya soka au burudani, nimekuwa nikipenda kujifunza na wadau wa tasnia husika. Ninajua haitakuwa rahisi kila mmoja kupata nafasi anayoipata mwingine.
 Ikitokea mwingine akapata nyingine, basi inakuwa rahisi kushirikiana nao kwa kuwaeleza aliona nini na kujifunza kipi ili awasaidie na wengine.


 Nilipotua katika Mji wa Coruna ambao upo Kaskazini Magharibi mwa nchi ya Hispania, nimejifunza mengi likiwemo moja ambalo sikuwahi hata kulisikia.

Wakati tukiwa katika ziara ya kutembelea Uwanja wa Raizor unaomilikiwa na Derpotivo la Coruna waliokuwa wanatarajia kuwakaribisha Barcelona katika mechi ya La Liga, kesho yake, yaani juzi, niligundua jambo moja la ajabu kidogo kuhusiana na vyumba vya kubadilishia nguo.


    tJambo hilo lilifanya niamini kweli mpira ni fitna hata kama inaweza kuwa ni halali. Pia mpira ni kuwachanganya wapinzani kisaikolojia. Hivyo kujiandaa kimwili ili kuwa fiti ni sehemu moja tu, lakini saikolojia ni muhimu sana.


  Wakati tunazunguka katika vyumba vya kubadilishia nguo ndani ya uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 43,600 tulianzia katika vyumba vya wageni. Yaani timu itakayofika pale kucheza dhidi ya wenyeji wake, Derpotivo la Coruna.

Hakika nilishangazwa kidogo, mazingira ya uwanja huo yalikuwa mazuri sana katika kila sehemu tulizopita, lakini vyumba vya timu mgeni yalionekana ni ya hovyo kabisa. Ajabu zaidi waliweka msisitizo si sahihi kupiga picha.

Basi, nikaona huenda kwa timu za Hispania, zimefeli katika kuweka mazingira mazuri vyumbani. Tukaendelea na ziara sehemu ya upande wa pili yaani kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya wenyeji.

Hapo nikashangazwa zaidi hadi nikaona ni wakati wa kujifunza. Hakika vyumba vilikuwa vizuri kama nilivyotarajia mwanzo.


 Sehemu nzuri kwa ajili ya masaji na matibabu kwa wachezaji. Hata vile viti vya kulaza wagonjwa na vile vya watu kwa matibabu, pia vilikuwa bora ukilinganisha na vile tulivyoviona kwa upande wa timu mgeni.

Nilipouliza, jibu kutoka kwa Armando Pelleiro wa Gazeti la DXT Compeon ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Msemaji wa Derpotivo la Coruna, lilikuwa hivi;

“Hii nenda kwenye uwanja wowote duniani, imekuwa ni utamaduni kwa vyumba vya wageni kuwa na hali ambayo si nzuri sana. Utaona hata choo kinatoa harufu kwa mbali.

“Sehemu ya kuogea pia si nzuri, mabenchi yao ni mabaya na hii tunafanya makusudi kabisa. Ukiingia Camp Nou au Santiago Bernabeu iko hivi na wenyewe wanajua.

“Mgeni ni mtu mzuri, lakini mgeni anayekuja kwako kukunyima raha na familia yako kwa kukufunga lazima uhakikishe hana raha kabla hajafanya hivyo.

“Timu zote za Hispania zinafanya hivi. Huu ni utamaduni wa soka la Hispania. Hatuwezi kwenda Camp Nou, halafu Barcelona watuweke kwenye sehemu ya hovyo halafu waje hapa sisi tuwape nafasi ya kutulia kisaikolojia,” anasema Pelleiro.

Hakika vyumba hivyo viwili vilikuwa ni vya aina tofauti utafikiri haviko katika uwanja mmoja. Nilijiuliza mara mbili kama kweli wachezaji wakubwa na maarufu kama Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar nao watakuwa kwenye vyumba hivyo juzi Jumatano.

Kumbe kumfanya adui asitulie si jambo baya katika soka ili mradi isiwe haramu na Pelleiro anasema, hakuna anayezoea shida au maisha mabaya na kila siku anapambana kuimaliza.

“Unaweza kusema timu ikipita kwenye viwanja vibaya inazoea, si kweli. Wachezaji wakubwa wanateseka sana. Unajua Lionel Messi au Cristiano Ronaldo wanaishi kwenye sehemu za kifahari. Kuwaweka kwenye vyumba vyenye hali mbaya vinawachanganya, hata kama wajikaze vipi hawawezi kuzoea.”

Umeisikia hiyo? Yanga na Simba wanaweza vipi kufanya fitina ya namna hiyo wakati wote wanaazima viwanja?

Azam FC wenyewe uwanja wao ambao tunawapongeza wanalijua hili? Au ndiyo ule mfumo wa Kitanzania wa “kumkarimu mgeni”. Tena mgeni anayekudhuru. Tujifunze.






0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic