April 18, 2016

Na Saleh Ally
KIKOSI cha Manchester United bado kinasuasua katika msimamo wa Ligi Kuu England ukilinganisha na namna timu hiyo ilivyokuwa awali.

Manchester United chini ya Kocha Alex Chapman Ferguson ndiyo walikuwa kikosi bora zaidi England, kikosi ambacho kilivunja utawala wa Liverpool.




Tangu ameondoka kocha huyo, Manchester United imekuwa ikisuasua, haina uhakika wa mambo mengi ikiwa ni pamoja na aina ya uchezaji wa kina nani ni wachezaji sahihi hasa kimfumo na mwenendo wa mafanikio.

Ndani ya makocha wawili, David Moyes na sasa Louis van Gaal bado Manchester United imeshindwa kurudisha sura yake ya enzi za Ferguson.

Sasa Manchester United imerudi katika sifa ya moja ya wapinzani wao Arsenal, inaonekana si timu ya kuwania ubingwa tena, badala yake inapigania kuhakikisha inacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Juhudi za kununua wachezaji mbalimbali kwa fedha nyingi na usajili wa kushitua England, bado Manchester ni timu inayosuasua na haina nafasi ya kutwaa ubingwa. Huenda msimu ujao na wasipoangalia huenda ikawa msimu ujao tena.

Wakati Manchester ikipigania hilo, imefanikiwa kumpata kinda Marcus Rashford ambaye ana umri wa miaka 18 tu, sasa ndiye tegemeo zaidi katika safu ya ushambuliaji kuliko hata wale walionunuliwa kwa fedha nyingi.

Kama hiyo haitoshi, Rashford ni muhimu na tegemeo zaidi katika safu ya ushambuliaji ya Manchester kuliko hata nahodha Wayne Rooney.




Kwa kifupi Rashford “amekamata nchi”, ndiye mshambuliaji anayeonekana kuipa uhai safu ya Manchester United na amefunga mabao mengi zaidi ukilinganisha na mechi alizocheza.

Juzi amefunga bao lake la 11 ambalo rasmi limeiteremsha Aston Villa kutoka Ligi Kuu England hadi daraja la kwanza, lakini bao hilo limeamsha matumaini ya Manchester United kupambana kupata nafasi ya Top Four.

Bao hilo ni la saba kwake tangu aanze kuichezea timu kubwa ya Manchester United, Februari, mwaka huu, tena ndani ya mechi 12 pekee. Utagundua kuwa kipaji kinaweza kuwa bora au zaidi ya fedha na mipango mingi.

Rashford ni mwanafunzi ambaye yupo chini ya akademi ya Manchester na anaendelea kuonyesha ni mtu sahihi kwa kufunga karibu kila mechi aliyocheza kwa hadi asilimia 86.

Mara ya mwisho alifunga mabao mawili wakati Man United ilipoitwanga FC Midtjylland kwa mabao 5-1 katika michuano ya Ulaya, lakini baada ya hapo ameendelea kuthibitisha yeye ni mchezaji mwenye kipaji cha juu kabisa unapozungumzia ufungaji.

Anthony Martial ni kati ya washambuliaji vijana bora kabisa duniani. Manchester United ililazimika kuipa Monaco kitita kikubwa cha pauni milioni 57.6 ili kumpata. Utaona wakati mwingine, Rashford analazimika kuanza huku Mfaransa huyo akiwa nje.

Rashford ana rekodi nyingine, ni ndogo lakini inathibitisha ubora wa kipaji chake ambacho hakika kinageuka na kuwa ukombozi au msaada wa kuikomboa Manchester United.

Kinda huyo ana uwezo mkubwa wa kulenga lango, huenda kuliko mshambuliaji mwingine yeyote wa Manchester United au Ligi Kuu England.


Kwani katika mashuti yake matano ya mwisho aliyopiga inaonyesha manne yalilenga lango na akafunga.

Pia ndiye amefunga mabao mengi zaidi kwenye Uwanja wa Old Trafford katika kipindi cha kwanza. Baada ya kufunga juzi dhidi ya Aston Villa, sasa ana mabao matatu ya kipindi cha kwanza ndani ya uwanja huo.

Uwezo mkubwa alionao ni utulivu na uamuzi wa haraka sana lakini uliojaa uhakika, hali ambayo inaongeza ubora wake.

Kidogo turudi nyumbani, lengo la kueleza yote hayo ya Rashford ni kutaka kuwakumbusha vijana pamoja na viongozi mbalimbali wa klabu zetu.

Kwa viongozi; Manchester United imemwaga mamilioni ya fedha kusajili wachezaji wa “world class” lakini utaona ili mambo yake yakae sawa inategemea kipaji ambacho hawajakinunua kwa kuwa Rashford alijiunga na Man United na kwenda moja kwa moja kwenye akademi yake akiwa na umri wa miaka 7 tu.

Pamoja na fedha zao, lakini Manchester wamekuwa wataalamu na wanaonyesha ni wanaotoa nafasi kwa vipaji vyenye nafasi ya kukua haraka.

Kwenye timu zetu za madaraja tofauti, kuna akina Rashford wengi sana. Lazima tutoe nafasi badala ya kuamini waliosajiliwa kwa fedha nyingi ndiyo wanaojua sana na wanapaswa kuwa msaada kuliko wale wa bei rahisi.

Kwa wachezaji; kama wewe ni mchezaji kinda, haupaswi kuwa mwoga au kurudi nyuma ukiamini mchezaji bora ni yule aliyesajiliwa kwa fedha nyingi.

Kama una kipaji kionyeshe, lia upewe nafasi ya kukionyesha, ukiipata basi jiamini na uonyeshe kweli kama anavyofanya Rashford kwa kuwa amepewa nafasi na kweli ameonyesha anaweza.

Kumbuka, baada ya kuonyesha kipaji chako na kuonekana kinafanya kazi. Kumbuka suala la nidhamu namba moja kwa kuwa wachezaji wengi wazuri hapa nyumbani wamepotea siku chache baada ya kung’ara kwa kuwa walijisahau na nidhamu yao ikawa mbovu.


Hii ilikuwa Julai, 2014, Rashford (wa kwanza kushoto mstari wa katikati) akiwa na kikosi cha U-18 cha Manchester United


KOMBE LA FA
Mechi  2
Mabao  2

MICHUANO ULAYA
Mechi  3
Mabao  2


LIGI KUU
Mechi 7  
Mabao  4


JUMLA
Mechi   12
Mabao   8

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic