May 18, 2016


Na Saleh Ally
LIGI Kuu England imemalizika kwa Leicester City kuchukua ubingwa. Wengi wanaona ni mshangao au wameshitukizwa, maana waliotegemewa hakuna aliyeupata.

Manchester United, Arsenal, Chelsea waliokuwa mabingwa watetezi au wakongwe wengine Liverpool. Wote wameshindwa na Leicester City ndiyo wakaibuka mabingwa, hii ni baada ya kuwa mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza.

Kuchukua ubingwa kwa Leicester City kumefanya wengi wanaofuatilia soka kuamini msisimko wa Ligi Kuu England umeporomoka. Hasa kwa kuwa vigogo wameonekana kupoteza mwelekeo.

Kiushabiki hilo linaweza kuwa sahihi kwa kuwa gumzo lilikuwa ni kwenye timu mbili hasa katika mechi 10 za mwisho. Leicester City walionekana wanachuana na Tottenham Hotspur kuchukua ubingwa. Timu hizi hazikuwa kwenye listi ya zilizokuwa zinapewa nafasi.
Kigogo pekee aliyeonekana ana nguvu, alikuwa ni Arsenal, mwishoni wakati zimebaki mechi saba tayari alishapoteza mwelekeo. Ingawa “Mungu saidia”, ameishia katika nafasi ya pili.

Wakati wengi wanafikiri hivyo, takwimu za mwisho za Ligi Kuu England zinaonyesha msimu huu, pamoja na vigogo kupoteza mwelekeo lakini ligi hiyo imepiga hatua kwa maana ya ushindani.


Ligi Kuu England msimu wa 2015-16 ambayo Leicester City amekuwa bingwa, imekuwa ni bora zaidi kuliko ya msimu uliopita wa 2014-15 ambayo Chelsea alibeba ubingwa.

Takwimu ndizo zinazoeleza hivyo, uzuri ni hesabu ambazo hazina hadithi wala upendeleo kwa kuwa zinajengwa kutokana na uchezaji wa timu zote 20 za ligi hiyo.

Msimu uliopita, baada ya kucheza mechi 38, Chelsea ilitwaa ubingwa kwa pointi 87, Man City ikakaa nafasi ya pili ikiwa na 79. Msimu huu bingwa ni Leicester akiwa na 81, Arsenal anafuatia akiwa na 71 na Tottenham namba tatu kwa kupata 70.


Ukiangalia msimu uliopita Chelsea walipata pointi 87, msimu huu pamoja na bingwa Leicester City kuwa na kasi ameishia pointi 81. Angalia msimu uliopita, Man City alifikisha pointi 79 akiwa nafasi ya pili, msimu huu Arsenal ana 71.

Ukiangalia katika ufungaji wa mabao, bingwa msimu uliopita Chelsea, alifunga mabao 73, safari hii kazi ilikuwa ngumu, Leicester wakafunga 68 tu. Hii inaonyesha ugumu wa kuta za timu mbalimbali.

Ubora wa ukuta wa timu fulani hasa zinapokuwa nyingi, inaonyesha ligi ilikuwa na ushindani wa juu au ulipanda.

Angalia msimu uliopita, Arsenal ilishika nafasi ya tatu na kufunga mabao 71, lakini msimu huu imeshika nafasi ya pili na kufunga mabao 65 tu. Imepanda kwa nafasi kwenye msimamo, lakini idadi ya mabao imeporomoka.
Kawaida katika msimu mzima wa Ligi Kuu England, mechi 380 huchezwa. Hadi jana mchana mechi 379 zilikuwa zimechezwa baada ya ile mechi ya Manchester United dhidi ya Bournemouth kuwa imeahirishwa. Iliwagharimu Man United kitita cha pauni milioni 3 ili ichezwe jana.


Lakini takwimu za msimu uliopita, bado zinaonyesha kwamba ugumu wa ligi hiyo msimu huu ulikuwa juu zaidi ya ule wa msimu uliopita. Msimu uliopita, wastani wa ushindi ulikuwa 45% lakini msimu huu ni 41%.

Kizuri ambacho kimeongezeka kwa msimu huu ni idadi ya ufungaji mabao mengi. Msimu uliopita jumla ilikuwa ni mabao 975 hadi mwisho wa msimu. Lakini msimu huu yamefungwa 1022, tena kwa mgawanyiko mkubwa. Hii pia inaonyesha timu nyingi zilikuwa na uwezo wa kufunga kuliko mwaka jana, kwa maana ya ufungaji wa mgawanyiko na si timu chache pekee.

Hili linathibitishwa na wastani wa timu zote kufunga bao katika mechi moja. Msimu uliopita, ulikuwa 49% na msimu huu umekuwa 52%. Maana yake, hakukuwa na timu iliyokuwa inaihofia nyingine na hakuna timu iliyokuwa nauhakika wa kuzuia isifungwe hata bao moja katika mechi.


Utaona ligi ya msimu huu, huenda haikuwa na mvuto kwa wengi kwa maana ya maneno ya kishabiki kwa kuwa timu zilizotegemewa kuwa gumzo mwanzo hadi mwisho, zilifeli.

Chelsea waliokuwa mabingwa watetezi, waliteleza hadi kuanza kutajwa katika nafasi ya kuteremka.
Lakini mambo yamekuwa magumu kwa wakongwe kama Manchester United, hata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, nayo imekuwa ni sehemu ya hadithi.


Hata wafungaji bora wanaonekana si wale waliozoeleka, hawakuwa wachezaji walionunuliwa kwa bei mbaya. Hii inaonyesha kweli msimu huu ligi ilikuwa ngumu kwa vigogo kuanzia timu hadi wachezaji. Lakini haikuwavuta wengi kwa maana ya ushabiki kwa kuwa waliowapenda, hawakuwa na nafasi ya kutamba.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic