May 30, 2016


Na Saleh Ally
KAMA itafanyika tathmini ya kutosha, basi klabu ya Simba inawezekana ndiyo itakuwa na rekodi ya juu zaidi ambayo ilijumuisha uhusiano mbaya kati yake na wachezaji wake.
Uhusiano huo, haukuwa mbaya wa kurushiana maneno lakini vitendo vilivyotokea vingi vilionyesha hakukuwa na mapenzi kati ya wachezaji na uongozi, wachezaji na wachezaji lakini pia wachezaji na klabu yenyewe.

Wako waliowaunga mkono wachezaji waliocheleweshewa mshahara kwa siku tisa tu, wakaweka mgomo, jambo ambalo linaonyesha kuwa wale waliogoma, yaani wachezaji wa kigeni hawakuwa na mapenzi hata kidogo na Simba.

Asikudanganye mtu kuwa hata kama ni shabiki wa timu nyingine, halafu unaichezea Simba na hauna mapenzi nayo, kamwe hauwezi kujitoa na kuisaidia badala yake utacheza “itakavyokuwa” mwisho uchukue mshahara. Huenda hiki ndicho walichokuwa wanakihitaji wachezaji hao wa kigeni.

 Lakini wachezaji wenyewe kwa wenyewe pia hawakuwa wanapendana kwa kuwa kuna baadhi walijipambanua kuwa wao ni watu bora au maarufu zaidi ya wengine. Hii ikajenga makundi.

Naweza kuulaumu uongozi wa Simba kushindwa kulidhibiti hili. Huenda kubadilika mara kwa mara kwa benchi la ufundi lilichangia baadhi ya wachezaji kujiona wao ni maarufu au muhimu kuliko wengine na hawakudhibitiwa.

Ndani ya kikosi cha Simba kumekuwa na matukio mengi sana yakiwemo yale ya wachezaji kununiana au kutosalimiana. Baadhi walikuwa wakionyesha dharau hata kwa baadhi ya viongozi huenda tu amefunga sana au anategemewa kwenye safu ya ulinzi.

Naweza kutoa mfano wa mapenzi au urafiki bora kati ya bata na minyoo au chambo. Hata uwe wa namna gani, lazima utaharibika na kuangukia katika vita. Mwisho wake, lazima bata atamla mshikaji wake.
Ndicho kilichokuwa kikitokea ndani ya Simba. Wachezaji walikuwa wana urafiki wa minyoo baina yao kama ambavyo ilikuwa kati yao dhidi ya uongozi ambaye ni kama mzazi wao.

Umeusikia uongozi wa Simba ukilalama kuhujumiwa na sehemu ya mifano ya wazi ni zile kadi walizopata Hassan Kessy ambaye amejiunga na Yanga na Ibrahim Ajib ambaye alitoroka na kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio.

Rekodi za Simba zinaonyesha ni timu ambayo imekuwa ikitoa ruhusa kwa wachezaji wake kwenda kucheza nje. Jiulize vipi Ajib anatoroka siku moja baada ya kulambwa kadi ya nyekundu tena ya kipuuzi?

Jibu ni kwamba hana mapenzi na Simba, huenda wao wanajaribu kumlazimisha. Pili hana uhusiano mzuri na uongozi, ndiyo maana anaona kutoroka ndiyo njia sahihi ya mkato.

Kessy analambwa kadi nyekundu ya kipuuzi pia, Simba ikiwa katika mbio za kuwania ubingwa. Siku chache anasajiliwa Yanga, hata kama si kweli, bado hofu au tuhuma haziwezi kuzuilika kwa asilimia mia.

Uongozi wa Simba unapaswa kujifunza kupitia yaliyotokea kwamba hayakuwa mambo ya kuvutia na ambayo kama yataendelea yataendelea kuwa tatizo kubwa.
Huu ni msisitizo, sidhani kama Simba watafanikiwa kwa kuendelea kuilaumu Yanga au kulia inabebwa. Badala yake ni vizuri kulenga katika kuweka mambo yake ya ndani sawa na kurekebisha vitu ambavyo vinaonekana kuwa tatizo.

Suala la mapenzi kati ya wachezaji na klabu, wachezaji na viongozi na hata wao kwa wao kupendana na kuoneana huruma haliwezi kukwepeka.

Kati yao lazima kuwe na mapenzi ili kujenga umoja wa dhati unaolenga wote kwa pamoja kufanikisha wanachokitaka. Makundi na madaraja hayawezi kuwasaidia wachezaji wala viongozi na klabu kwa ujumla.

 Kama uongozi hautalirekebisha hilo kabla ya kuanza kwa msimu ujao na wakati wa usajili. Basi wajue, wataendelea kuwa watu wa kulalamika na mafanikio yakiwa ni hadithi kwao.

4 COMMENTS:

  1. Wewe nawe ni pumba kama hans Poppe,unataka wachezaji waipende timu inayowaambia kuwa Simba si mama yako!?Wewe vipi au ndio ukanjanja huo?

    ReplyDelete
  2. Kwa kiasi fulani sikubaliani nawe kwenye suala la Kessy. Mkataba unaisha baada ya msimu, anapewa kadi nyekundu na club inamfungia mechi zote zilizobaki. Kwa maana nyingine hakutegemea kucheza hadi mkataba unaisha, kwahiyo mlitaka akae tu nyumbani wakati club yake imeishaonyesha dhahiri haimuhitaji na offer imetokea asisaini!? Pili lazima tuwe wakweli, mchezaji hawezi kutoka nje ukasema eti ana mapenzi na simba au yanga, alizijulia wapi!? Siku hizi mpira pesa, Delima alikuwa na mapenzi na RM japo aliichezea barca kwa mafanikio!! Kitu cha kumpa mapenzi mchezaji ni treatment ya washabiki, benchi la ufundi na viongozi. Kuna wakati CR7 alijihisi kutokuwa mwenye furaha RM hadi mambo ninayoyasema yalipobadilika na kupewa thamani yake tena kwa kupewa mkataba mnono!! Mtu hawezi kuja ugenini eti mapenzi, mlipe chake kwa wakati then mdai matokeo

    ReplyDelete
  3. kweli kabisa, na ndio maana halisi ya kuitwa timu kwasababu watu kwenye hutegemeana nje na ndani ya uwanja na huo ndio mwanzo wa matokeo bora ya timu kwasababu wachezaji wanakuwa hawaishi kama wafanyakazi bali kama ndugu wa damu moja

    ReplyDelete
  4. Nadhani kwa swala la Kessy ingekuwa vizuri ungeweka na swala la kupigwa na golikipa wa Simba baada ya mchezo huo uliosema kuliko kuishia kusajiliwa kwake Yanga. Hivi wewe ungekuwa ni Kessy na shutuma zote alizokuwa anapata toka alipofungisha mechi ya Yanga ungeweza kweli kucheza kwa amani kwenye hiyo timu?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic