May 11, 2016



MURO
Tayari Yanga wameshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara lakini wameendelea kuonyesha tambo kuwa wanataka kufanya kweli kwa kuwa wao ni wa kimataifa, baada ya kumsajili Ramadhan Kessy kutoka Simba, sasa wamepiga dongo jingine kwenda Msimbazi.

Habari ni kuwa Yanga wamedai kuwa wanajiandaa kumsajili mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib ambaye kwa sasa hayupo nchini ikidaiwa kuwa amesafiri kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa licha ya kuwa huko nyuma kumekuwa na utata mwingi.

Ajib alimchezea faulo ‘tata’ Hassan Kabunda wa Mwadui FC katika mchezo kati ya Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuonyeshwa kadi nyekundu, kesho yake alfajiri akaondoka kwenda Sauz huku uongozi wa Simba ukipata kigugumizi juu ya safari hiyo, hivyo kutokana na upepo huo unaoendelea, bila shaka presha inazidi kuwa kubwa kwa Wanasimba kwa kuwa Ajib ni mchezaji muhimu kikosini kwao.


Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo haukuridhia suala la Ajib kwenda Sauz, hivyo presha hiyo inaweza kufanya hofu iwe kubwa kama kweli majaribio hayo ni ya kweli au kuna mipango mingine.

Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro amethibitisha juu ya kumsaka Ajib wakati akizindua Tawi la Wanachama wa Yanga la Yanga Uswazi Mbeya, jana maeneo ya Sokomatola, ambapo alisema baada ya Kessy sasa wanamtaka Ajib.

“Tumeshafanikiwa kunasa saini ya Kessy, watakuja wengi tu kutoka kwa wa mchangani, kama Ibrahim Ajib na wengine wengi tu watakuja, hivyo msiwe na hofu sisi tutaendelea kufanya vema kwenye michuano mbalimbali tunayoshiriki,” alisema Muro huku akishangiliwa na wanachama hao.

Katika hatua nyingine, taarifa kutoka Sauz zinasema Ajib amenaswa mitaani nchini humo akiwa amevaa jezi ya kijani, hatua ambayo imesababisha sintofahamu kutoka kwa Wanayanga na Wanasimba waliomuona.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Simba ilimpoteza aliyekuwa beki wake Ramadhan Wassso ambaye alikwenda nje ya nchi kufanya majaribio na aliporejea alisajiliwa na Yanga. Huenda ishu ya Ajib ikawa kama hivyo.

Hata hivyo, Ajib bado ana mkataba wa mwaka mmoja, hivyo kuna ugumu wa usajili wake endapo Simba haitaridhia kumuuza kwa Yanga.

Baada ya kauli hiyo Muro alidai kuwa Kessy alikuwa akidumazwa Simba kwa kutopewa mahitaji mazuri kama mchezaji ikiwemo kutosafiri kwa ndege, hivyo amejiunga na Yanga maisha yatakuwa safi kwake.

Aidha, wanachama wa tawi hilo walimuomba Muro kuwa mlezi wao ombi ambalo lilikubaliwa, mlezi mwingine wa tawi hilo ni Omary Chuma.


Wakati huohuo, Muro aliwaahidi Wanayanga kuwa mara baada ya kukabidhiwa kombe la ligi kuu, watajipanga kurejea jijini hapa kwa ajili ya kucheza mechi moja ya kirafiki ya kimataifa na timu kutoka Malawi ikiwa ni sehemu ya kuwaonyesha Wanambeya kombe hilo na kuwashukuru kwa kuwaunga mkono.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic