May 9, 2016


COASTAL UNION

Na Saleh Ally
MEI 21, mwaka huu itakuwa ni siku 10 tu tangu leo. Wananchi wa Mkoa wa Tanga hasa kwa wale wapenda soka, watakuwa wamepata jibu kamili kuhusiana na “wako wapi”.

Siku hiyo ndiyo itakuwa ni mwisho wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-16. Hofu kuu ya Wanatanga ni timu zao zote tatu kuteremka daraja zikitokea Ligi Kuu Bara hadi daraja la kwanza. Panga hilo, kweli lipitie timu zote za Tanga tu?
Bahati mbaya kabisa, tayari timu moja huenda ndiyo kubwa na yenye jina kuliko nyingine, Coastal Union imeteremka daraja.

Wakubwa kabisa, wameteremka daraja tayari, hofu inazidi kwa kuwa nyingine mbili za African Sports na Mgambo Shooting nazo ziko katika hali inayofanana na hakuna anayeweza kujisifia nafuu kwa kuwa “msiba unanukia”.

Coastal Union ambayo ina mechi moja tu ya mwisho dhidi ya Prisons, hii itakuwa ni ya kujiburudisha tu kwa kuwa wao tayari ni timu ya daraja la kwanza, hata kama Prisons watachezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano.

Hiyo ni mechi moja, utaona pointi hizo tatu za mwanzo hazitakuwa na faida yoyote kwa Coastal Union au Wanatanga hata kama timu yao itashinda katika mechi hiyo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mechi nne zilizobaki, mbili za Mgambo na mbili za African Sports, zitazaa pointi 12 ambazo huenda ndiyo Wanatanga wanazihitaji zaidi kuliko zile tatu za Coastal Union zinazoonekana ni sehemu ya kujiburudisha tu. 

Mgambo wana mechi mbili dhidi ya Azam FC ambayo watakuwa wageni Azam Complex jijini Dar es Salaam halafu watamaliza ligi wakiwa nyumbani dhidi ya JKT Ruvu ambao wana wakati mgumu na watapambana kuhakikisha wanashinda na haitakuwa mechi rahisi hata kidogo.

Lakini unaona ugumu kwa Mgambo katika mechi ya kwanza pia kwa kuwa wanakutana na Azam FC ambayo hata kama haijapata ubingwa, ni timu kubwa yenye wachezaji ghali na wanaolipwa vizuri, bado itataka heshima ya kuwa katika nafasi ya pili.

MGAMBO VS SIMBA

Bado Azam FC watakuwa katika nafasi ya kufuta makosa yao na kuwaridhisha mashabiki na mabosi wao. Kama unakumbuka wamepokonywa pointi tatu baada ya kumchezesha Erasto Nyoni aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Ukirudi kwa African Sports, unaweza kuona hakuna tofauti yoyote na Mgambo kwa kuwa nayo iko katika nafasi ileile, ngumu.

Imebakiza pia mechi mbili dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo watakwenda kucheza Manungu, Turiani. Kwa wenyeji mechi hii haitawapeleka kokote lakini kwa maana ya heshima na rekodi ni bora kwao na huenda wangehitaji kushinda nyumbani.

Ukirudi katika mechi ya pili na ya mwisho kwa African Sports ni ile itakayopigwa ugenini Azam Complex dhidi ya wenyeji wao Azam FC ambao inabaki palepale wanataka kurudisha imani na heshima kwa mashabiki na mabosi wao hata kama wameshakosa ubingwa.
Sports wana pointi 26 katika nafasi ya 13 katika timu 16. Ukiangalia timu tano zinazojikomboa kuteremka daraja zote zina pointi zinazokaribiana na kufanana. Toto Africans ina pointi 30, JKT Ruvu (29), African Sports (26), Kagera Sugar (25) na Mgambo wana 24.
Maana yake ukiteleza mchezo mmoja ndiyo unaweza kuwa mwisho wa Ligi Kuu Bara. Hivyo ugumu bado ni wa juu kabisa kwa African Sports na Mgambo.

MASHABIKI KWENYE UWANJA WA MKWAKWANI...

Hisia kwamba timu zote tatu za Tanga zinaweza kuteremka daraja, hilo bado linawezekana kabisa na likitokea litakuwa jambo baya kuliko lolote katika mpira wa Tanga.
Wakati tunakwenda huko, huu ndiyo wakati mwafaka kwa watu wa Tanga kujipima na ikiwezekana kuungana hata kama ni mwishoni, basi waikomboe hata timu moja au mbili zilizobaki zikiendelea kupambana.

Katika pointi 15 walizobakiza za timu zao, tayari tatu zimeonekana hazina maana tena kwa kuwa Coastal Union watakuwa wakijifurahisha tu. Pointi 12 kwa Mgambo na African Sports, ni zaidi ya muhimu na wanapaswa kuzipigania.

Nimezungumza sana kuhusiana na namna ambavyo viongozi wa timu za Tanga walivyojaza watu wengi wenye maneno kuliko vitendo. Wanaoamini wanajua sana kumbe hawajui lolote.

Ukiachana na hivyo, wengi wao ni watu wenye chuki na husuda na hili ni jambo kubwa ambalo linawaangusha na kwa kuwa si wasikivu na walalamishi, basi wamekuwa wakiendelea kuporomoka na huenda itaendelea hivi milele, timu za Tanga zitakuwa ni za kupanda na kushuka kila wakati.

Angalia Mgambo iliyobaki angalau zaidi ya misimu mitatu ikiwapa nafasi Wanatanga kuona ligi kuu nyumbani, leo imeambukizwa “kaugonjwa ka Tanga”, nayo inapambana kwelikweli kujikomboa, jambo ambalo ni aibu hata kama mtakataa.

Hakuna mafanikio bila ya upendo hata kama kundi husika litajumuisha watu wenye fedha nyingi na akili nyingi pia. Iko haja mkubali kufungua mioyo yenu na kubadilika.

Mwisho, nawakumbusha zile vurugu za Mkwakwani kwamba kweli zimepitwa na wakati. Ubabe inawezekana ni sehemu ya usela wa Tanga, lakini kubalini kwamba ujanja wa kutaka kupigana kila wakati umepitwa na wakati.

Mnaweza kusingizia ile mechi ya Kombe la FA Coastal Union ilipoivaa Yanga na waamuzi wakaboronga ile mbaya. Lakini rekodi zinaonyesha Mkwakwani kumekuwa na vurugu hata kama ni mechi kati ya timu za Tanga dhidi ya nyingine, yaani si Simba na Yanga. Sasa kama ugomvi ungekuwa unalipa, basi sasa Tanga isingekuwa inasumbuka na wokovu wa timu zake zisiende na maji. Badilikeni mashabiki wa Tanga, mnaishi kwenye ulimwengu wa 1980, dunia imewaacha.

MECHI ZILIZOBAKI:
Coastal Union:
Coastal                Vs           Prisons          Mkwakwani

Mgambo:
Azam                  Vs           Mgambo       Azam Complex
Mgambo              Vs           JKT Ruvu              Mkwakwani

African Sports:
Mtibwa                Vs           Sports             Manungu
Sports                  Vs           Azam              Mkwakwani



2 COMMENTS:

  1. Kinachoigharimu Coastal Union ni ujuaji hasa wanapocheza katika uwanja wao. Mashabiki wao wanahitaji kuelewa kuwa vurugu zao zinaididimiza timu badala ya kuisaidia.
    Mbona hatusikii vurugu kama hizo kwenye timu kama Majimaji ya Songea? Wameweka akili zaidi kwenye mpira na namna ya kujinusuru sio kufanya vurugu zisizo na maana yoyote.
    Inawekezana mwamuzi hakuwa fair kwenye mechi yao na Yanga. Je hizo mechi zote nyingine ilikuwaje?

    ReplyDelete
  2. hujaandika kitu hapa.ni kwanini unawabebesha na kuwafanya mashabiki ndio wanashusha timu.hujaingia ndani zaidi kutuelezea sababu za kiufundi kwanini timu hizo zinashuka,wewe unabaki na mashabiki ndio wameshusha timu,je hakuna sababu nyingine funguka.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic