May 24, 2016



Na Saleh Ally
MSEMAJI wa Yanga, Jerry Muro leo amesema wanataka kukutana na timu za Waarabu kwanza kabla ya TP Mazembe.

Yanga inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, iko hatua ya robo fainali na Muro anataka wakutane na TP Mazembe hatua ya fainali.

Lakini hakuna anayeweza kujua nini kitatokea wakati wa upangaji wa matokeo leo.

Yanga sasa ni mwakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho akiwa amefanikiwa kusonga katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Haitakuwa sahihi hata kidogo kubeza juhudi zao kama timu ya Tanzania iliyofanya vizuri. Pia haitapendeza kwao kuona safari waliyoianza inalingana na waliyopita.

Yanga wameingia kwenye ile hatua sasa wanaweza kujipima kweli kama wao ni ‘Wa kimataifa’ wa kweli, maana wanakutana na vigogo hasa.

Wanakuwa kati ya timu nane zinazosubiri kupangwa katika makundi mawili ya timu nne nne, kazi itakayofanyika Jumanne ijayo.

Timu wanazokutana nazo Yanga, tano zinatokea Kanda ya Kaskazini ambazo ni Mo Bejaia ya Algeria, FUS na Kawbab Marrakech (zote Morocco), Al Ahli (Libya) na Etoile du Sahel (Tunisia).


Moja inatoka Afrika Magharibi ambayo ni Medeama ya Ghana na TP Mazembe wa DR Congo ambayo ni Afrika ya Kati.

Hakuna timu kutoka Kusini mwa Afrika, Yanga pia ni pekee kutoka Afrika Mashariki na huenda itawakilisha Ukanda wa Kusini.

Hii pekee utaona namna Yanga ilivyopiga hatua kubwa kwa maana ya mabadiliko ya soka hapa nchini. Lakini lazima ijiandae kisaikolojia na mwili kwa ujumla kwa kuwa hakuna ujanja katika hatua iliyofikia.

Hii ni hatua ya timu bora za Afrika zimekutana, hakuna uchaguzi na kinachotakiwa ni kila timu kuwa tayari dhidi ya timu nyingine.

Yanga haina ujanja, kama itaiepuka TP Mazembe katika kundi itakalopangwa, inaweza ikakutana na timu tupu za Waarabu. Hakuna timu ya kubeza kutoka kwa Waarabu hao.
Kama haitakuwa hivyo, maana yake lazima itapangwa na Mazembe, Madeama ya Ghana na timu moja ya kutoka kwa Waarabu hao wa Kaskazini mwa Afrika.


Yanga lazima wajue hawana cha kukwepa tena. Maandalizi yao hayaangalii tena watakutana na nani. Badala yake wanatakiwa kujiandaa kwa uhakika na kuwa tayari kwa yeyote.

Presha ya Yanga kufikiria itakutana na nani ni kupoteza muda. Badala yake inapaswa kujiandaa tu maana ukikwepa Magharibi, utaangukia Kaskazini au TP Mazembe.
Ukiangalia katika timu saba inazotarajia kukutana nazo, nne zimeshabeba makombe ya Afrika.

Ukiangalia hatua hii ya makundi, msimu uliopita timu tano zilitoka Kaskazini mwa Afrika, moja Magharibi na moja Kusini ambayo ilikuwa ni Orlando Pirates.

Huu ni wastani sahihi wa utawala wa soka kupitia klabu kwa ukanda barani Afrika. Yanga wanakuwa wakombozi tena wa Ukanda wa Mashariki, ndiyo maana lazima wakubali ushindani wa Kaskazini na Kati bila ya kuangalia nani watakutana naye.


MSIMU ULIOPITA:
Al Ahly (Misri), Esperance (Tunisia), AC Leopards (Congo), CS Sfaxien (Tunisia), Stade Mallen (Mali), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Zamalek (Misiri) na Etoile du Sahel ya Tunisia.

Etoile:
Hawa ni mabingwa mara mbili wa Kombe la Shirikisho (mwaka 2006 & 2015), pia walikuwa washindi wa pili 2008. Etoile ni timu kubwa, walibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2007.

Uzoefu wao Afrika unaonyesha walikuwa mabingwa wa Kombe la Washindi (1997 & 2003). Wakachukua Super Cup Afrika 1998 na 2008.

Mo Bejaia:
Mouloudia Olympique de Bejaia, maarufu kama Mo Bejaia, hawa ni ng’e kutoka Jangwa la Sahara au ng’e wa Algeria. Bado hawana rekodi nzuri ya makombe Afrika. Wanaweza kufanana na Yanga, lakini ni timu iliyopania kuleta mabadiliko makubwa. Hivyo kuibeza, haitakuwa sahihi hata kidogo maana inatokea Ukanda wa Kaskazini.

Medeama:
Hawa ni watu wengine wenye njaa, unaweza kusema wako chini kisifa kama utawalinganisha na rekodi za Yanga. Lakini kumbuka wanatokea Ghana, ambako kuna maendeleo kisoka.

Medeama si timu kali sana ukitafuta historia au rekodi za nyuma, lakini si timu ya kubeza kama utazungumzia wakati mwafaka.

Ahli Tripoli:
Mwaka 2008, Yanga iling’olewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Timu ya Al Akhdar ya Libya. Awali wengi waliidharau, lakini ikawaduwaza na hapo imani kwamba Libya kuna watu wa soka, kila mmoja alianza kuamini.

Ahli ndiyo timu bora zaidi Libya, hivyo utaona hakutakuwa na lelemama na timu hiyo iliyokuzwa chini ya Rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi itataka kufanya vizuri na kuanzisha rekodi mpya kwenye michuano ya Caf.

FUS
Sasa ni kati ya timu vigogo nchini Morocco, ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho mwaka 2010, mwaka uliofuata wakaishia 16 bora, walifika robo fainali ya Kombe la Caf mwaka 1996 lakini walitinga fainali ya Super Cup ya Caf mwaka 2011. Hii si timu ya kubeza hata kidogo.

Kawbab Marrakech:
Timu nyingine kutoka Morocco, inajua utamu wa makombe ya Afrika. Mwaka 1996 walikuwa mabingwa wa Kombe la Caf, mwaka uliofuata wakaingia fainali. Walipoteza mwelekeo kitambo, miaka ya 2000 haikuwa safi kwao. Sasa wamerejea na lazima kutakuwa na umakini mkubwa maana tayari wapo robo fainali.

TP Mazembe:
Hawa ni wazoefu na wakali zaidi, huenda ungeona saizi yao ni Ligi ya Mabingwa Afrika. Imeanza kuchukua ubingwa tangu ikiwa Klabu Bingwa Afrika, ubingwa wa kwanza 1967 na 1968. Lakini wakalibeba kama Ligi ya Mabingwa mara tatu 2009, 2010 na 2015.


Si heshima ya ubora, lakini kuheshimu walipofikia ingawa kwenye ushindani kila kitu kinawekwa kando na mapambano yanachukua nafasi ya juu ili kupata ushindi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic