May 23, 2016



Na Saleh Ally
MABASI ya Mwendo Kasi na wengine wanayaita Mwendo Haraka yameanza kazi katika sehemu mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam.

Ni mradi ambao umegharimu mabilioni ya fedha hadi kukamilika na unahitaji mamilioni ya fedha ili kuuendesha.
Mradi huo, faida kuu ni wananchi wa Tanzania ambao wataweza kufika haraka waendako na pia kurahisisha au kupunguza ukubwa wa foleni za jijini Dar es Salaam.

Kila siku zinavyosonga mbele, utaona kuna kila aina ya vipingamizi ambavyo vinatangulia mbele ya mradi huo.
Mfano watu kutoelewa maana yake, wako wanaochora viti na sehemu za ndani ya mabasi hayo, wakiandika majina yao, rafiki zao au wapenzi wao, ili mradi tu. Wako wanaovunja utaratibu na wengine hata wamesababisha ajali.

Tumesikia baadhi ya watu wakipinga kuwepo kwa mradi huo kwa kuwa wanaamini uwepo wake ni kuwapunguzia au kuwaondolea kabisa maslahi yao.

Kwa kifupi, mradi huo sasa umegawanyika kwa kuwa kipenzi na adui wa Wanadar es Salaam ambao wako waliulilia na wengine leo hawautaki, mfano wamiliki wa mabasi ya daladala.

Yako mengi sana ukizungumzia mradi huo, lakini ukweli lengo ni kusaidia wananchi na kurahisisha masuala ya usafiri.

Katika mchezo wa soka, waamuzi ni watu muhimu sana kwa kuwa wanategemewa kufanya mambo yaende sahihi. Unaweza kuwaita sawa na askari wa soka, maana ndiyo watu wanaozilinda sheria na kusisitiza zifuatwe.

Soka bila mwamuzi, unajua kitakachofuatia. Kila mmoja atafanya lake, itakuwa ni shaghalabaghala na kila mmoja atakuwa na sheria yake kichwani au mkononi. Mambo hayawezi kwenda kwa mpangilio.

Hata waamuzi wenyewe, wamepewa mafunzo maalum ili kuhakikisha wanapewa nafasi hiyo. Hii ni kuonyesha jambo hilo ni muhimu na linasimamiwa kwa ubora sahihi. Wako wanaoonyesha kweli ni waamuzi na wamelenga kuifanya kazi yao kwa kufuata weledi.

Kwangu asilimia kubwa ya waamuzi si watu wanaofuata weledi kwa maana ya kucheza mechi, mfano za Ligi Kuu Bara au Ligi Daraja la Kwanza kama inavyotakiwa.

Huwezi kusema kwamba si wazuri kimafunzo ndiyo maana wanakosea. Lakini tamaa, ushabiki au matakwa binafsi yamekuwa ni tatizo kubwa kwa waamuzi wa soka hapa nyumbani kushindwa kufikia kiwango sahihi au bora kinachotakiwa.

Hadithi zilizopo ni kwamba waamuzi wamekuwa wakitumika kuzisaidia timu nyingine na kuzikandamiza nyingine. Hili lina ukweli kwa kuwa wanaohusika ni watu walewale walio ndani ya mpira.

Vitendo vya utoaji na kupokea rushwa ni sawa na uzinzi, kila kitu hufanyika kwa siri kubwa. Ndiyo maana wengi wamekuwa wakifanikiwa kukwepa au kuhoji wakitaka wapewe uhakika.

Inajulikana wazi kuhusiana na matumizi ya mitandao ya simu kutumia fedha na namna ambavyo baadhi ya waamuzi wamekuwa wakiwatumia ndugu au rafiki zao wa karibu kuwapokelea fedha ili wao wazibane timu fulani. 

Wala si siri, inajulikana hadi bei za uhongaji fedha ambavyo imekuwa ikitolewa kwa ajili ya kuzisaidia timu fulani na fulani. Na huu si mtindo wa klabu moja au mbili za Ligi Kuu Bara au Daraja la Kwanza. Ukweli ni asilimia 90 kwenda mia, huu ndiyo mtindo, labda utoaji unaweza kupishana kwa kiwango pekee.

Najua juhudi kubwa za ‘mficha maradhi’. Lakini kumbukeni kila hali inavyokwenda, itafikia siku ‘maradhi yatawaumbua’ katika hili.

Waamuzi mnalalamika, lakini mnajua miongoni mwenu kwa asilimia kubwa mnapokea rushwa na kusababisha ukwamishaji wa maendeleo ya soka.

Ndiyo maana naufananisha mkasa wenu na mabasi yaendayo kasi kwani pamoja na kuingia kusaidia maendeleo, watu wanayapinga wakiwemo wanaohusika na usafirishaji. Nyie pia, mkiwa ndani ya mchezo wa soka, mnapinga maendeleo yake kwa makusudi kabisa ili kufaidisha nafsi zenu, oneni aibu na mbadilike.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic