May 16, 2016



Na Saleh Ally
TULIAMBIWA Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanza kulishughulikia suala la kashfa ya rushwa inayowakabili viongozi wawili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Viongozi hao ambao kwa kuwasikiliza wala hauhitaji akili ya ziada kujua huyu ni fulani na yule ni nani, walikuwa wakizungumza kupanga matokeo.

Walisikika wakiomba rushwa ya wazi kabisa, tena wakitaja baadhi ya vyeo vya viongozi wengine wa TFF. Walionekana walitaka fedha hizo tena kwa idadi ya juu kabisa.

Kiongozi mmoja anajaribu kuzungumza kuonyesha namna ambavyo wahusika wanaweza kusaidiwa baada ya kutoa kiasi cha fedha.

Raha zaidi, hadi wale viongozi sauti zao zinasikika na inajulikana wanatokea katika klabu gani ya Ligi Daraja la Kwanza.

Tangu Takukuru imelichukua suala hilo, sasa ni takribani mwezi au zaidi. Nilielezwa walianza kufanya mambo kadhaa ya mahojiano.

Kwanza, nianze kwa kusema sitaki kuingilia utendaji wa kazi yao, lakini kuhoji ni haki yangu tena hata bila ya woga. Kuna mtu alinieleza kwamba, nikiendelea kuliuliza hili mwisho na mimi ninaweza kuhojiwa au wanaohusika ambao wanaonekana wanataka kuona haliendi mbali watanimaliza.

Kwangu huo ni ujinga wa juu kabisa na kamwe siwezi kuwa kwenye aina ya kundi la watu waoga wa namna hiyo. Takukuru ni chombo cha serikali na tuna haki ya kukihoji kama kitaonekana hakifanyi mambo yake kwa usahihi.

Kwa sasa ninaamini wanaendelea, lakini naona kama inachukua muda mwingi bila kusikia nini kimefanyika. Ndiyo maana ninahoji, na ninawaahidi kuendelea kuhoji tena kwa kuwa tunachotaka ni kuona haki inatendeka na ikiwezekana mpira wa Tanzania kuondoka kwenye njia iliyojaa magugu unakopita.

Rushwa ya kupindukia ipo katika mpira wa Tanzania. Wanaohusika wala wasijaribu kutaka kuwatafuta wale wanaohoji kutaka kuwachafua ili kupunguza kasi yao ya kuhoji.

Kikubwa na msisitizo, Takukuru ifanye kazi yake na mwisho ni vizuri tukajua. Kwani pamoja na kwamba vitu vinakwenda kwa uchunguzi, mimi bado naona ni taratibu sana.

Waamuzi wamekuwa wakilaumiwa kwa kuboronga, kweli inajulikana kwa kuwa rushwa inatembea. Lakini wapo ambao wamekuwa wakiamrishwa na baadhi ya viongozi kuzisaidia timu fulani.

Inawezekana mlolongo huohuo tuliousikia kwenye zile sauti ndiyo uliochangia kwa kiasi kikubwa waamuzi au Kamati za TFF kufanya maamuzi ya kipwagu, kizandiki, kibazazi na kizabizabina ambayo ndiyo adui mkubwa wa mpira wa Tanzania ambao umekuwa unatambaa tangu miaka ya 1960 hadi leo.

Nimepiga sana kelele kuhusiana na watu wanaoufanya mpira wetu kutambaa. Nimegombana na wengi na wengi hawanipendi hadi leo hii, lakini kama wewe umenyamaza, mimi ninyamaze, mwisho wetu utakuwaje!

Mimi naendelea kusema tena na tena kwa kuwa nataka kuona mabadiliko na kumalizika kwa mabazazi hao ambao tabia zao ni za kizandiki.

Kuna methali inasema: “Mti ukifa shinale, tunda zake hukauka”. Nani anaweza kukataa leo kuwa shina ya mchezo wa soka na hata mingine imekufa kabisa. Na ubinafsi ndiyo chanzo, rushwa ni sehemu ya ubinafsi kwa kuwa ni unyang’anyi wa maendeleo kwa kundi kubwa na kuwagawia wachache wafaidike tena wakiendelea kutamba kwa kuwa wana nafasi ambazo pia wanazipata kupitia wananchi.

Nani hajui kama viongozi wa juu wa soka ni tatizo, wengi wamegombea ili wafaidike kifedha. Wapo wenye uwezo mdogo wamebebwa na mabwanyenye wao kwa kuwa walikuwa watumishi waaminifu kwao na si waaminifu wa mpira au michezo ya Tanzania? Najua mnajua, lakini mmekuwa waoga kwa kuwa haya au aibu ndiyo haki yenu.

Nakuachia methali hii: “Mchelea haki hatendi ukweli.” Hii ndiyo maana yake, (anayeona haya kuzungumza au kusimamia haki, hawezi kuwa mtenda haki.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic