May 11, 2016



KIIZA

Na Saleh Ally
Wachezaji  sita wa kigeni wa Klabu ya Simba wamegoma kwenda mjini Songea kuichezea timu hiyo kwa kuwa hawajalipwa mshahara wa mwezi uliopita!

Hadi wanagoma ilikuwa ni tarehe 9, yaani siku tisa tangu mwezi mpya uanze, si wao tu, wachezaji wote wa Simba hawakuwa wamelipwa.

Wageni hao sita ni Hamisi Kiiza, Juuko Murshid na Bryan Majegwa kutoka Uganda, Justice Majabvi wa Zimbabwe, Emiry Nimubona raia wa Burundi na Vincent Angban wa Ivory Coast.
Mkenya, Raphael Kiongera, alikuwa majeruhi ingawa inaelezwa alikuwa kati ya walioshikilia mgomo huo!

Lakini wale wazalendo wameamua kwenda na timu kuitumikia katika mechi dhidi ya Majimaji licha ya kwamba hawajalipwa mishahara yao.

JUUKO

Wanajua jukumu lao kuu ni kucheza dhidi ya Majimaji, kazi yao ni kuitumikia Simba na wanajua watakuwa wanadai haki yao.

Uongozi wa Simba, mwisho umelazimika kufanya ujualo na kulipa mshahara huo. Baada ya hapo, wachezaji hao wa kigeni wakaanza safari ya kwenda Songea juzi, kwenda kuisaidia Simba.

Suala hilo limezua gumzo kubwa. Huenda swali la msingi kwa uongozi wa Simba, vipi ulishindwa kulipa mshahara mapema? Halafu ukatoa wapi fedha hizo kwenda kulipa.

Nilielezwa kwamba baadhi ya viongozi Simba walilazimika kukopeshana, kukopa sehemu ili walipe. Wamefanya hivyo kwa kuwa mara kadhaa, wadhamini wao ambao hulipa mshahara wamekuwa wakitoa fedha hizo baada ya wiki ya kwanza.

MAJABVI

Kuchelewa kwa mshahara, si jambo geni au jipya. Ninaamini hata wewe kama ni mfanyakazi au umewahi kuwa mfanyakazi umewahi kuidai ofisi yako kutokana na kuchelewa kwa mshahara.
 Wachezaji wa kigeni wameamua kutokwenda kazini kwa kucheleweshewa mishahara yao kwa siku tisa pekee?

Wachezaji wanaopewa nyumba, mishahara mikubwa kuliko wa wazalendo ambao wengi wao mishahara yao midogo na hawapati huduma bora kama wanaopata hao wageni.
Angalia katika wageni hao, yupi hasa anayetokea katika nchi ya maziwa ambaye anaweza kusema alichezea timu ambayo haijawahi kuchelewesha mshahara?

 Nakutajia nchi hizo, Burundi, Uganda na Zimbabwe? Hizi ni nchi unaweza kuamini suala la kucheleweshwa mshahara kwa siku nane au 10 halijawahi kutokea? Nimebahatika kufika katika kila nchi, tena zenye ligi isiyokuwa na malipo makubwa kama wanavyolipwa na kutukuzwa hapa nyumbani.

AGBANI
Kweli, kuna kati yetu amewahi kugoma kwa kuwa mshahara ulichelewa kwa siku tisa? Utasema wachezaji wa nje au Ulaya wanajitambua sana. Unakumbuka mkasa wa Portsmouth ya England waliocheza zaidi ya mechi sita za ligi bila kulipwa mishahara yao, lakini wakaendelea hadi mwisho wa ligi. Hiyo England, unataka kuniambia wapi kwingine?

Tunajua Simba na hata Yanga wamekuwa wakilalama wadhamini wao kuchelewesha mishahara. Lakini pamoja na kusikika mara mojamoja, lakini wamekuwa wakiendelea kupambana hadi mwisho na wanapolipwa mambo yanaendelea.

Nitapishana nanyi wote, lakini nataka niwaambie Simba walisajili wachezaji wengi kutoka nje walio na uwezo wa chini, na wenye uwezo nafuu, walikuwa si wenye mapenzi na timu hiyo na imechangia kuwaangusha.

NIMUBONA
Hebu jiulize, eti hata Nimubona anagoma kufanya kazi baada ya mshahara kuchelewa kwa siku 9, kaifanyia nini Simba? Juuko ambaye alianza vizuri, mwisho amegeuka kuwa tatizo kubwa na beki anayepitika kwa ulaini huenda kuliko wageni wote, naye anaona anaonewa kwa mshahara kuchelewa kwa siku hizo?

Kiiza amefunga mabao mengi kweli, mwisho unagundua alikuwa amewekewa ahadi na kiongozi mmoja wa Simba, akifunga mabao 19 atanunuliwa gari. Hivyo hayakuwa mapenzi ya dhati ya kazi yake au kuipenda Simba kutoka moyoni. Jiulize isingekuwa hiyo gari, kweli angefunga hayo mabao?

Bado hata Majabvi hakuwa na kiwango cha juu hivyo. Jiulize mara ngapi walicheza chini ya kiwango na kuiponza Simba na wakawavumilia. Vipi washindwe kuvumilia kwa huo, vipi wasuse kuitumikia Simba kwa kucheleweshewa mshahara mmoja?

Katika wote, kipa Angban unaweza kusema alifanya kazi yake vema zaidi. Lakini ninaamini, naye Simba walimvumilia wakati fulani.


Inawezekana kuna mengi na sikatai wachezaji hao kudai haki yao. Lakini kuna namna ya kudai, askari kukataa mapambano kwa kisingizio cha njaa ya siku moja ni tatizo kubwa.

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. mpira kazi wewe hakuna mpira wa bure zama hizi,wavumilie nn hawakuja hapa kuvumilia walikuja kufanya kazi na kupata fedha kwa ajili ya familia zao,mpira wa mapenzi ilikuwa zamani zama za akina Dilunga wakulaumiwani viongozi wa Simba na sio wachezaji wanashindwaje kuendesha timu kisasa wanaongoza mpira kiujanjaujanja na bado unawatetea nyinyi ndio mnarudisha nyuma mpira wa nchi hii kwa kuleta ujanja ktk maisha ya wachezaji

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic