June 8, 2016



Na Saleh Ally
WALIOKUWA wanafuatilia soka kwa ukaribu mwanzoni mwa miaka ya 2000, wanakumbuka namna ambavyo kulikuwa na ushindani mkubwa na ubora wa viungo wakabaji na mfano mzuri alikuwa ni Selemani Matola wa Simba.

Kabla ya hapo, Tanzania ya kizazi cha kati katika soka ilikuwa na viungo wengi kama Ramadhani Reny, Said Mwamba ‘Kizota’ (wote marehemu), Hussein Marsha, Method Mogella, Nico Bambaga au Hamisi Gaga (pia marehemu) ambaye kama Kizota, waliweza kung’ara namba nyingine kama kiungo mchezeshaji.

 Matola alionekana hana mpinzani katika namba sita wakati wa enzi zake ingawa mafundi kama Mwanamtwa Kihwelo, Salvatory Edward bado walikuwa ni gumzo na uwezo ulikuwa juu sana.

Baadaye aliibuka Athumani Iddi maarufu kama Chuji ambaye alichipukia kama kijana tegemeo akiwa katika kikosi cha timu ya Polisi Dodoma.


Chuji alicheza kama mlinzi wa kati akiwa Polisi Dodoma, walipomchukua Simba akapewa jukumu la kiungo mchezeshaji baada ya kuonekana sanaa yake ya uchezeshaji ilikuwa juu zaidi, hivyo kumuacha abaki namba nne ni kama matumizi mabaya ya sanaa aliyonayo.

Labda nianzie katika kipindi cha karibu zaidi ili wengi wanielewe. Nizungumzie kipindi cha Salvatory aliyekuwa nahodha wa Yanga na Taifa Stars, Matola, nahodha wa Simba pia Mwanamtwa. Uchezaji wao, baada ya Chuji, hakuna anayeweza kucheza hivyo tena!

Tanzania leo, haina namba sita wa uhakika na utaona ukiwahesabu, wanaonekana ni wa shida kabisa na kama wapo, basi ni matatizo matupu isipokuwa wachache sana.
Mwanamtwa au Bambaga, Matola au Salvatory walikuwa viungo namba sita wanaokaba na kupandisha timu. Viungo wanaofanya maamuzi ya nini kifanyike na kwa wakati upi.

Viungo hao walikuwa ni watu wanaojiamini, waliotumia maelekezo ya kocha na uamuzi wao na ukiona kati ya hao, wengi wao angalau walicheza nje ya Tanzania kama Matola aliyechukuliwa Afrika Kusini bila majaribio na kadhalika.

Ukifanya tathmini, ndani ya kikosi cha Simba, namba sita ni tatizo, nenda Azam FC ni tatizo pia na hata kwa Yanga waliochukua ubingwa bado kuna tatizo kubwa kwa kuwa wazalendo waliopewa nafasi hiyo wanaonekana hawaiwezi na ili kupata ufumbuzi, ni kuangalia wageni.

Unataka kuniambia au kuniaminisha Tanzania sasa haina namba sita wa uhakika? Kwangu angalau unaweza kumzungumzia Jonas Mkude ambaye tokea ametulia, angalau anaweza kucheza katika nafasi hiyo ukasema ndiyo, lakini kwa kufananisha uwezo aliouonyesha Chuji hadi mwaka 2014 wakati anaondoka Yanga utasema hakuna mtu.


Angalia kikosi cha Stars, mimi naona kuna tatizo la kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kukaba na kuanzisha maamuzi ya timu ifanye nini kwa wakati husika. Jaribu kufananisha uchezaji wa viungo wa sasa wa timu nilizokutajia au unazozijua na ile aina ya Chuji kama unamkumbuka. Waliopo sasa ni nafuu.

Wakati huo, Chuji ambaye aliingia Yanga mwaka 2006 hadi 2011, kabla ya kujiunga na Simba msimu mmoja tena, halafu akarudi Yanga hadi 2014, alikuwa anakaba, anachezesha timu na bado anasaidia mashambulizi.

Mara ya mwisho pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam unakumbuka umeona lini mashuti makali kama yale ya Chuji ambaye alikuwa hata hasubiri kuingia kwenye 18. Lakini makipa wakiwemo wale wa kimataifa, mikono yao iliwaka moto.

Aina ya uchezaji wa morali, uchezaji wa mtu ambaye anaonekana anataka kitu. Sasa viungo namba sita wanacheza wakionekana hawana tofauti na namba nane, mpira unaopakwa rangi na pasi za ‘skwea’.

Inawezekana leo ni mwaka wa pili sasa tokea Chuji akiwa haonekani katika soka la ushindani lakini hakuna tena mwenye uchezaji wa aina yake. Tanzania hakuna namba sita kama Chuji tena?

 Tujiulize, Chuji alikuwa kizazi cha mwisho cha viungo wakabaji nchini na baada yake hatuna na tukitaka bora inabidi tukatafute nje?


Yanga imemsajili Andrew Vicent, kwangu naamini kama akipewa nafasi hiyo huenda akaleta mabadiliko kwa kuwa ni mchezaji anayeonyesha anacheza akiwa anahitaji kitu. 

Lakini tusubiri kwanza na waliobaki, bado wanapaswa kujifunza kwamba Chuji alikuwa shule yao ya mwisho kiuchezaji na wakiendelea hivi, mwisho namba sita itakuwa namba ya wageni milele, maana kawaida, namba sita bora hawezi kuwa nalenale au bishoo badala yake mtu wa kazi kweli.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic